Mrema-2Hiki ni kipindi cha Uchaguzi Mkuu. Oktoba 25, wananchi watakwenda kwenye vituo vya kupigia kura. Wananchi watakuwa na jukumu la kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wake (mgombea mwenza). Kwa Wazanzibari, mbali na Rais na Makamu wa Muungano, watamchagua pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.


  Ukiacha ‘vingunge’ hao kwa nafasi mbili za juu, bado wananchi watafanya kazi ya kumchagua mbunge na diwani. Kwa Zanzibar sawa na ilivyo kwa urais, bado watapiga kura ya ziada, kwa maana ya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kwa ufupi, katika Uchaguzi huu Zanzibar wanapiga kura tano.
  Zanzibar wanamchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Mbunge, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Diwani, wakati Tanganyika nao wanapiga kura tatu, kwa kumchaguai Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mbunge na Diwani. Nikumbushe tu, kuwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa Bara na Visiwani tayari, na wakuu wa mikoa wa Zanzibar huteua masheha, ambao ni sawa na balozi wa nyumba 10.


  Sitanii, katika safu hii sasa kwa mfululizo naandika makala kuhusiana na mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu. Makala zilizotangulia nimeanza na kilichotokea ndani ya CCM na sasa kinachotokea kwenye vyama vya upinzani. Mwaka huu kutakuwa na vyama 11 vinavyosimamisha wagombea wanane. Cha kwanza kitakuwa CCM, ambacho mgombea wake ni Dk. John Magufuli.
 Naamini huenda mwaka huu tutakuwa na wagombea urais wanane. Jaji Damian Lubuva, amesema: “Tunaanza kutoa fomu kwa wale wanaogombea urais, kesho (Jumamosi), UPDP wataokuja kuchukua fomu saa tatu asubuhi wamesema hawana shamrashamra… TLP wao watakuja saa sita mchana, wanakuja kwa shangwe… DP wao wanakuja saa nane mchana pia nao wamesema watakuja kwa shangwe pia.


“Jumanne Agosti 4 watakuja CCM saa sita mchana, watakuja kwa shangwe kama wengine… Jumatano watakuja ADC saa tatu asubuhi, wao hakuna shamrashamra, baada ya hapo watakuja TADEA saa nne asubuhi pia wao hawana shangwe.
 “Agosti 17 watakuja ACT-Wazalendo saa tatu asubuhi, wanakuja kwa shangwe pia… muda wa kuandikisha wapigakura kwa mfumo wa BVR unaisha rasmi Agosti 8, 2015 na baada ya hapo ratiba ya Tume itaendelea kuruhusu Uchaguzi Mkuu.”
Ukisoma taarifa hii sanjari na taarifa ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa watafanya vikao mfululizo kwa nia ya kuteua jina la mgombea wa vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD katika wiki ya kwanza ya mwezi huu, basi utabaini kuwa wagombea huenda wakawa wanane.   


Hadi naandika makala hii sikupata majina ya wagombea wa vyama vingine isipokuwa CCM na Ukawa. Kwa CCM ni Dk. Magufuli kama nilivyomtaja hapo juu na kwa Ukawa kuna kila dalili kuwa atakuwa Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu (mstaafu) aliyeihama CCM na kujiunga na Chadema kwa alichokiita ‘mizengwe wakati wa mchakato wa uteuzi’.   
Viongozi wa Ukawa wamekaririwa na vyombo kadhaa wakisema hivyo, na sasa kuna kila dalili kuwa huenda zamu hii, ukiacha hivi vyama vilivyotangulia kuchukua fomu, huenda kusiwe na mgawanyiko kwa vyama vikuu vya upinzani vinavyounda Ukawa.
Ikumbukwe kuwa katika Bunge lililovunjwa, vyama vinavyounda Ukawa vilikuwa na jumla ya wabunge 89 kwa mchanganuo wa Chadema 49, CUF (35), NCCR-Mageuzi (5) na NLD hawana mbunge. Kwa wanaokumbuka, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema chama hicho kinahitaji wabunge 133 kupata wingi wa wabunge bungeni. Kwa idadi hii anazungumzia wabunge wa majimbo pekee.


  Sitanii, idadi hii ya wabunge 133 anaowasema Lissu ni ya wabunge wa jimbo. Kwa sasa idadi ya majimbo yote ni 239, ila yameongezeka na kufikia 265, hivyo nusu ya idadi hiyo ni 133. Chama kitakachopata idadi hiyo ya wabunge wa majimbo ndicho kitakachopewa fursa ya kuteua Waziri Mkuu wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 51(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotaka Waziri Mkuu ateuliwe kutokana na chama chenye wabunge wengi.
Kwa sasa vyama vinavyounda Ukawa vinao wabunge 51 wa majimbo kwa mgawanyo wa Chadema 23, CUF (24) na NCCR-Mageuzi (4). Idadi ya wabunge 89 niliyoitaja hapo juu inajumuisha wabunge wa Viti Maalum. Vyama vingine vilivyosalia vina wabunge wawili, kwa maana ya TLP mmoja na UDP mmoja. Idadi hiyo inapaswa kuondolewa wabunge watatu wa majimbo ambao ni Hamad Rashid (CUF) na Zitto Kabwe na Said Arfi (Chadema) waliohama vyama hivyo.


  Hii ina maana kuwa Ukawa wanayo majimbo 48 (ikiwa wataendelea kuyashikilia) na hivyo wanahitaji majimbo mapya 85 kuweza kupata idadi hiyo ya wabunge wa jimbo 133. Wapo wanaoamini kuwa kama Ukawa hawatafarakana ndani ya wiki ya mwisho kuelekea uteuzi, sawa na fukuto linaloelezwa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa, tayari anazengewa na wazito wa chama tawala na huenda akajiuzulu, idadi hii wanasema wanaweza kuipata.
  Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema “Lowassa si sawa na Mrema.” Nimewaza kuandika makala hii, baada ya kuona na kushiriki mijadala kadhaa inayoashiria kuwa Lowassa atapoteza umaarufu wake si muda mrefu kama alivyopotea kwenye ‘media’ ya siasa za urais Mzee Augustino Lyatonga Mrema. Mrema alikuwa maarufu kweli. Alikuwa anabebwa, ila hakushinda urais.
Mimi kwa uzoefu wangu, sitaki kuwapa watu kauli za kuwafurahisha.


Nilisema wakati wa mchakato wa ndani ya CCM kumpata mgombea urais kuwa yeyote atakayeungwa mkono na Lowassa ndiye atakayeteuliwa kuwa mgombea wa CCM. Sitaki kurudia makala ya wiki iliyopita, ila nilichosema kimetokea. Kwamba Lowassa aliamua kuwaangusha Bernard Membe na January Makamba, akawaelekeza wafuasi wake wampigie Magufuli kura na wakafanya hivyo, tujue hawa bado wapo ndani ya CCM.
  Katika hatua hiyo, sidhani kama kuna mwananchi yeyote bado anadhani hii ni nadharia. Wapo wanaosema katika siasa hakuna bahati mbaya, na kwamba hicho kilichotokea wakubwa walipanga ndicho kitakachokuwa. Mimi nasema, hewala. Kama walipanga Membe aangushwe na Lowassa, kisha Magufuli apite, basi walikosea mkakati kutumia maneno yaliyomuudhi Lowassa. Wangechagua mbinu nyingine ya kiungwana kukata jina lake, badala ya kutamka kuwa hawamtaki.   


Narudia, Lowassa kuondoka CCM siamini kuwa amepoteza nguvu zote ndani ya chama hicho kwa sasa. Hii ni tofauti ya kwanza kuu kati yake na Mrema. Mrema alikuwa na mashabiki, ila Lowassa ana wafuasi. Mrema alishabikiwa na watu kutokana na mhemuko wa kuona kuwa kumbe unaweza kukipinga chama tawala, baada ya muda mrefu wa kupiga kura za ndiyo na hapana.
Tofauti ya pili ni kuwa kwa karibu miaka 20, Lowassa amekuwa akifanya kampeni katika nchi hii. Hii inamaanisha nini? Kikwete alitwambia kuwa mwaka 1995 ulipoisha Uchaguzi Mkuu alianza kampeni za chini kwa chini. Mwenyekiti wa kampeni za Kikwete alikuwa Lowassa. Hii ina maana amefanya kampeni tangu mwaka 1995 hadi mwaka 2005.


  Sitanii, bila shaka kwa mtaji huo wa uzoefu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Lowassa alianza kampeni zake hadi mwaka 2015. Hii ndiyo iliyozaa mwaka 2012 kati ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) 378, alifanikiwa kuingiza wafuasi wake 316. Sina uhakika kama Mrema alikuwa na mtaji wa kimkakati kama huu.
  Inawezekana hawa wafuasi wa Lowassa baada ya jina lake kukatwa, kwa sasa wana hofu. Wanaweza kuogopa kupokea simu yake au kwenda nyumbani kwake kumsabahi, ila tukumbuke “Zimwi likujualo, halikuli likakwisha.” Hapo ndipo ninaposhuhudia mgogoro wa wazi katika kampeni za CCM. Wapo watakaokuwa wanatiliwa shaka. Mtu kama Hussein Bashe iwe ameshinda kura za maoni na kuteuliwa au la, hili nisemalo linamhusu.
Kinachoweza kutokea sasa ni kuwa zitakuwapo timu si chini ya tatu za kampeni. Kutakuwapo Kamati ya Wasira. Hii itaundwa na “Timu Magufuli” damdam. Itakuja Kamati ya Kampeni ya CCM, hii itahusisha wote. Itakuja Kamati ya “Timu Lowassa” itakayojihisi kubaguliwa wakati wa kampeni, na hivyo kwa njia moja au nyingine watakuwa na ‘tuvikao twao’ kujadiliana iwapo wanaaminika kweli au la.


Ni katika hatua hiyo, nasema hii ni tofauti nyingine kati ya Lowassa na Mrema. Enzi za Mrema, walioamua kuimwaga CCM, waliondoka moja kwa moja, na wale waliokunywa maji ya bendera, walibaki na wakawa wanampiga kutoka kwenye sakafu za mioyo yao. Ufuasi wa Lowassa ndani ya CCM ukoje, hili nililizungumza vyema wiki iliyopita. Hadi wauza baa wanaamini Lowassa atawaondolea umaskini na wako tayari kumuunga mkono.
  Sitanii, nafasi inazidi kuwa finyu. Nimekuwa nikilisema hili na narudia kulisema kuwa Magufuli kama Magufuli hana tatizo. Ni mtendaji mzuri, ila wengi wanachosema ni kuwa mfumo uliompitisha na wanaomnadi ndiyo wanaoweza kuzaa historia ya CCM kuondoka madarakani ikiwa wataendeleza vijembe na ubabe, badala ya kuomba kura na kueleza watawafanyia nini Watanzania wakishinda.


La mwisho, nguvu ya Mrema ilififishwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mzee Mwinyi anaheshimika, ila yeye alikwishatwambia mapema kuwa: “Mimi, nikilinganishwa na Mwalimu Nyerere ni sawa na Mlima Kilimanjaro na kichuguu cha mchwa.” Siijadili kauli hiyo. Mzee Benjamin Mkapa anaheshimika, ila akisimama watu watakumbuka – Tangold na Kiwira, hivyo kimamlaka (moral authority) hawezi kuwashawishi Watanzania sawa na alivyofanya Mwalimu Nyerere dhidi ya Mrema.
  Ombi langu ni kuwa katika maisha binadamu hufanya kosa kwa njia moja au nyingine. Kujuta ni sehemu ya ubinadamu, ila kukiri ni heri zaidi. Tuanze kujiandaa kisaikolojia. Naamini katika Uchaguzi huu Tanzania itaendeleza utamaduni wa miaka yote, ikiwa Lowassa na Magufuli hata kabla ya mchakamchaka kuanza, watatuahidi na wataheshimu ahadi yao kuwa watakubali matokeo yatakayotokana na sanduku la kura.
  Mungu ibariki Tanzania.