Mwanzoni mwa wiki iliyopita nilikuwa miongoni mwa watu waliojitokeza kuitumia haki yao ya msingi ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kwa mfumo wa kielektroniki (BVR), lakini kutokana na vituko vinavyoendelea haikuwezekana kuandikishwa.
Kituo nilichokuwa nimepewa namba ya kuandikishwa kipo jirani kabisa na ninapoishi, ni ofisi ya serikali ya mtaa wa Mivumoni, Tegeta – Wazo jijini Dar es Salaam.
Nilipewa namba 627 na kupewa ratiba, baada ya siku nne ndipo nifika katika kituo hicho cha kuandikisha, huo ndio utaratibu uliowekwa na baadhi ya waandikishaji na wenyeviti wa mitaa na maofisa watendaji. Hata hivyo nilipofika kituoni hapo kama nilivyopangiwa lakini ilishindikana kabisa kuandikishwa. Kwani hadi Julai 28 mwaka huu idadi ya watu waliokuwa wameandikishwa ni 144 tu.


Majibu hayo ya wahusika yalinikera mno. Kama kwa siku sita kituo kimeandikisha watu 144,  je  itachukua muda gani kufikiwa idadi hiyo ya watu 600 tena kwa uzembe wa aina hiyo ambao unaonekana kufanywa kwa makusudi na nia chafu ya watendaji wa tume?
Sikuweza kutulia baada ya kuona makundi makubwa ya watu ambao baadhi yao walinieleza kwamba wamelala katika vituo kwa zaidi ya siku nne kuanzia saa sita usiku bila kuandikishwa, hivyo ikanilazimu kuwasiliana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva na kumweleza udhaifu wa kazi hiyo ya uandikishaji wapiga kura.


Jaji Lubuva alipotambulishwa tu kwamba mimi ni mwandishi wa habari, hakutaka kunipa nafasi zaidi ya kuelezea udhaifu ambao unafanywa kwa makusudi na baadhi ya waandishi wa wapiga kura kwa kushirikiana na watendaji wa kata na mitaa kwa kukidhi matakwa yao kisiasa na pengine kujenga mianya ya rushwa; aliishia kunielekezea shutuma kwamba “ Waandishi wa Habari wote mko UKAWA, hamtaki kuandika mazuri ya NEC, ninyi ni mabaya tu kila siku karibu vyombo vyote.”
Kutokana na shutuma hizo nilimjibu maana ya habari ni kuripoti matukio yasiyokuwa ya kawaida miongoni mwa jamii na hili la tume kuonekana wazi ina nia ya kuharibu uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kukithiri kwa vituko katika vituo vya uandikishaji wapiga kura nchini tangu kazi hiyo ilipoanza nchini kwamba ndio habari zenyewe.


Baada ya kutoa majibu hayo kwa Jaji Lubuva, alikubaliana nami kwamba kweli kuna uzembe na ubabaishaji katika zoezi hilo na kuhamishia tuhuma zake kwa wasimamizi wa majimbo ambao ni Wakurugenzi wa Manispaa za Dar es Salaam (Kinondoni, Ilala na Temeke) na kwamba wakazi wa jiji hili wote ni wajuaji.
Amekiri kuwa uzembe mkubwa uko Manispaa ya Kinondoni. Katika maeneo ambayo ni ngome za upinzani, jimbo la Kawe na Ubungo ubabaishaji umetawala kwa kiwango kikubwa kutokana na baadhi ya vituo vyenye wapinzani wengi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), utaona imewekwa mashine moja tu ambayo “inazimia na kuzinduka” baada ya muda mrefu. Vituo vingine wenyeviti wa mitaa wa CCM na maofisa watendaji wa kata wanawaandikisha watu kwa upendeleo hasa wale ambao ni makada wa chama hicho kinachotawala sasa napengine kinaweza kuanguka mwaka huu katika uchaguzi mkuu, wengine wanaohitaji kupatiwa nafasi hiyo huelekezwa kwa watu maalumu waliowekwa kwa ajili ya kukusanya rushwa ya Sh. 10,000/- kwa kila mtu anayetaka kuandikishwa haraka au kuuziwa nafasi za mbele.


Nilijiuliza maswali mengi na kujumuisha na maswali mengine kutoka kwa wananchi mbalimbali niliowahoji kutoka katika vituo vya uandikishaji nilivyovitembelea ni madudu kila kona hivyo NEC ya Jaji Lubuva, haiwezi kujinasua katika njama hizi za kuvuruga uchaguzi kwa hofu ya kifo cha CCM.
Haiwezekani kuona kila eneo ndani ya serikali hii kuendelea kukithiri kwa rushwa, hata kuandikisha wananchi ili waitumie haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao wanatozwa rushwa, halafu tume ya uchaguzi inakuja na hoja dhaifu kwamba wanahabari ndani ya nchi hii wanatumiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kuripoti madudu yanayojitokeza kila siku tangu uandikishaji ulipoanza nchini.
Hapa nathubutu kusisitiza tena Jaji Mstaafu, Lubuva anajipambanua wazi kuwa yeye ni kada wa CCM hivyo hawezi kuwa mwamuzi mzuri katika uchaguzi wa mwaka huu na badala yake atakipendelea chama chake kilichompa nafasi hiyo ya kuongoza tume ya uchaguzi. Chonde chonde Lubuva na NEC yako msituletee balaa nchini. Tendeni haki ili amani yetu iendelee kudumu.