Ngoma inogile – wale wa kucheza wanacheza na wale wa kushangilia wanashangilia na sisi watazamaji tunaoona utamu wa ngoma tumekaa pembeni kushuhudia mirindimo ya ngoma na mashairi yaliyopangika, ni burudani sana lakini ngoma yaelekea haitakesha mwisho ni alfajiri ya Oktoba.
Sasa nchi yetu imeingia katika siasa ngumu ya kunadi kichama, kunadi sera zinazowezekana na zisizowezekana. Watanzania wengi wamekuwa ama wanachama ama washabiki wa hiki tunachoita mfumo wa vyama vingi na siasa ya vyama vingi.


  Ni jambo jema kwa sababu mwisho wa mchakato tutampata kiongozi ambaye anaweza kukidhi matakwa ya Watanzania wengi walioamua kumpa kura zao, na hakika ni wakati wa ukurasa mpya wa kisiasa ambao utaweza kuifungua Tanzania katika ulimwengu wa siasa mpya.
 Wiki kadhaa zilizopita chama tawala CCM kilimtangaza mgombea wao ambaye walijiridhisha kwamba ni mtu safi na hana dosari yoyote katika kumuuza kwa wapiga kura wao, wamejiamini na utendaji wake na wanasema hawana shaka na kumkabidhi sera ya chama chao aiongoze na kuitekeleza, hiki ni chama kikongwe ambacho kimeshika dola kwa miaka yote achilia mbali utaratibu wao wa kubadilisha jina la chama.
Wiki jana chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)kwa kushirikiana na vyama vingine vya kisiasa ambavyo vinaunda umoja maalum ujulikanao kama Ukawa, wamemsimamisha mgombea wao aliyekuwa mmoja wa wagombea wa CCM, ambaye hakuridhishwa na mchakato wa upatikanaji wa rais na kuamua kujiondoa kutoka chama hicho.


Mgombea huyo amechukua fomu ya kuutaka urais ili naye aweze kutekeleza kile kilichopangwa na CCM, lakini hakuweza kupitishwa na sasa anaingia kutekeleza sera mpya ya Chadema iliyoandaliwa kwa ajili ya mafanikio ya serikali yao, iwapo itapewa nafasi au ridhaa na wananchi kwa miaka mitano ijayo.
  Kuna sintofahamu kubwa iliyojitokeza kwa wananchi japokuwa wanaamini kuwa wagombea wao wapo na watawachagua, hivyo basi kipenga cha Tume ya Uchaguzi kitapopulizwa kuashiria kuanza kwa kampeni, naamini tutasikia mengi kutoka pande zote zinazowania urais katika mikutano yao ya hadhara.
 Itachukua muda kidogo kwa kila mgombea kutetea nafasi yao kwanini wameamua kumsimamisha mgombea huyo, ni kipindi cha machungu kwa mpigakura japokuwa mwishoni uamuzi wa kupiga kura kila mtu ana siri yake moyoni.
 Nimeamua kuandika hili wanangu ili mkae sawa msije mkapata mshtuko kusikia mambo ambayo hamkuyatarajia, mtayasikia kwa sababu chama tawala ni lazima kiseme kwanini walimwengua kipenzi cha watu kama wanavyodai Wanachadema, hali kadhalika Wanachadema watasema kwa nini wanamuuza mgombea wao kwa wapiga kura ili awe rais wetu wa awamu ya tano.


 Ni kipindi kizuri kisiasa na kipindi kibaya kwa wananchi ambao wana matarajio ya kila namna kutoka kwa kiongozi wao. Wapo watakaohoji utendaji wa wagombea wao wote kwa kuwa wamekuwapo katika nyadhifa za juu serikalini kwa muda mrefu na kwamba iweje waweze kuyaleta hayo mabadiliko kwa kipindi chao.
 Kila chama kina mtaji wa watu, kina mtaji wa wanasiasa, kina mtaji wa sera, kinachosubiriwa ni namna ya uuzaji wa sera na siyo mtu kama ambavyo watu wengi walivyo na mtazamo hasi. Tukifanya mambo kwa ushabiki na ufuasi tutaendelea kwenda shimoni ambako bado ni tatizo kwa Mtanzania wa leo.
 Nimewaandikia barua hii nikiwajulisha kuwa na amani na napenda maendeleo, sipendi vurugu na umaskini, sipendi siasa za matusi napenda sera, sipendi kukumbushwa kwanini ni maskini napenda kuoneshwa taswira ya mafanikio ya kweli, sipendi kuwa mpigakura tu napenda kuwa mshiriki wa maendeleo ya Taifa langu.


Vyama vitakufa lakini Tanzania itabaki, tofauti na kasoro za wagombea zisifanye Taifa kuwa nyuma ya vyama. Uzalendo ni muhimu kuliko vyama, amani ni muhimu kuliko vyama, tukiifanya ngoma ya siasa za chuki usiku kucha tukasahau amani na uzalendo basi hiyo ni ngoma ya kitoto haitakuwa imekesha.
  Naamini kila atakayepanda ulingoni kunadi sera atasema na sisi juu ya umaskini wetu, afya zetu, huduma zetu za jamii, maendeleo yetu ya elimu, na mambo mengine muhimu kwa sisi wapiga kura maskini. Sitarajii kusikia yule alikula sana juzi, yule ni mwizi, yule kabebwa na fulani, wale ndiyo walewale na kadhalika.
Siamini mipasho katika jambo makini kama la kuongoza nchi na watu wake. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Wassalaam,
Mzee Zuzu
Kipatimo.