Mradi wa kimkakati wa ujenzi wa bandari ya Ndumbi ziwa Nyasa wilayani Nyasa mkoani Ruvuma umekamilika.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyasa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangasongo amesema mradi huo umetekelezwa na Kampuni ya CHICCO ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 12.
Amesema mradi ulikuwa unatekelezwa kwa mkataba wa miezi 22 ambapo ujenzi wake ulianza Desemba 2019 na kukamilika Februari 2022.
“Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100,hata hivyo hivi sasa upo katika kipindi cha uangalizi cha mwaka mmoja na mradi upo tayari kwa ajili ya matumizi’’,alisema Mangasongo.
Amelitaja lengo la Mamlaka ya Bandari Tanzania kuanzisha mradi huo kuwa lilikuwa ni kwa ajili ya kusafirisha shehena ya makaa ya mawe kutoka mgodi wa makaa ya mawe Ngaka wilayani Mbinga hadi bandari ya Ndumbi ziwa Nyasa.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma nan chi jirani za Msumbiji na Malawi.
RC Thomas amesema uwekezaji uliofanyika katika utekelezaji wa ujenzi ya bandari ya Ndumbi ni mkubwa kwa sababu serikali imetumia mabilioni ya fedha kutekeleza mradi huo wa kimkakati.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kwa sababu mradi huo unakwenda kufungua fursa mpya za uwekezaji mkoani Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma