Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar

Wadau wa habari wanasubiri kwa hamu kubwa kuona Serikali ikitimiza ahadi yake ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari bungeni ili kusaidia kupunguza changamoto wanazokabiliwa nazo sekta ya habari.

Akifungua mkutano wa wadau wa mawasiliano na TEHAMA (Connect to Connect) Afrika jana,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Baraza la Mawaziri limeridhia kutungwa kwa sheria ya kulinda taarifa binafsi ambapo kwa mara ya kwanza sheria hiyo itasomwa Bunge la mwezi huu wa Septemba huku akiwataka wadau watakaokuwa na nafasi za kutoa maoni wafanye hivyo.

Akizungumzia hatua hiyo Wakili wa kujitegemea James Marenga amesema kuwa pia wadau wa habari, wangefurahi zaidi kuona Waziri Nape akitimiza ahadi yake ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria za Habari katika Bunge la mwezi huu wa Septemba.

“Wadau wangependa kuona ahadi ya Waziri Nape ya kupeleka Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yanafanikiwa kwenye Bunge hili la mwezi Septemba ili mchakato wa mabadiliko hayo ukamilike,” amesema Wakili Marenga.

Amesema, mjadala wa Serikali na wadau wa habari ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016 na kwamba, kuna baadhi ya vipengele tayari wamekubaliana.

“Mjadala wa Serikali na wadau ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016, na yaliyojadiliwa ni mapendekezo ya wadau na yale ya serikali, kuna vipengele tulikubalia na vingine bado vipo kwenye mjadala,” amesema Marenga.

Marenga ameongeza kuwa sheria ya kulinda taarifa binafsi za kimtandao si ya wadau wa habari pekee, inahusu watu wote.

“Halafu hii sheria ya data protection (ulinzi wa taarifa binafsi ) sio kwa ajili ya wadau wa habari pekee, ni sheria muhimu kwa watu wote,” amesema.