Nianze hoja yangu kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na amani ndani ya mioyo yetu, na hatimaye kuweza kuyafanya mengi tuyafanyayo kila kukicha likiwamo hili la ujenzi wa barabara za kuwezesha mabasi kwenda mwendo kasi.
Kwa mantiki hiyo ni vema na haki na kila wakati kumshukuru Mwenyezi Mungu aliye mwingi wa rehema na mwenye kutujali muda wote wa maisha yetu.
Basi, inatupasa kumshukuru na kumpa Mungu heshima na utukufu anaostahili kupewa na sisi binadamu tuliobahatika kuwa hai hadi leo.
Baada ya kuyasema hayo naomba pia nitumie fursa hii kusema machache kuhusu barabara za mabasi ya mwendo kasi (rapid bus transport) ambazo sasa zinajengwa katika Jiji la Dar es Salaam kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na Serikali yetu.
Kwa suala la barabara hii, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inajenga barabara kuwezesha mabasi kwenda kwa haraka kutoka kituo kimoja hadi kingine. Ujenzi umeanza katika Barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Feri, lakini pia kipande cha Barabara ya Kawawa kutoka makutano yake na Barabara ya Morogoro hadi Morocco kwenye makutano na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Vilevile, inajengwa Barabara ya Msimbazi, eneo la Kariakoo kutoka makutano ya Fire-Barabara ya Morogoro hadi Kamata. Pamoja na kuiita barabara ya mabasi mwendo kasi (rapid transport) ukiangalia umbali kati ya kituo na kituo; inaonekana kuwa vituo vipo karibu-karibu mno.
Katika harakati za kutatua tatizo la msongamano wa magari katika barabara karibu za Dar es Salaam, ndipo watunga sera na wanaofanya uamuzi kwa niaba ya Watanzania wakaja na wazo ili kujenga barabara maalum za kuwezesha mabasi ya mwendokasi kutoa huduma ya usafiri wa haraka.
Kusema kweli hili ni wazo zuri. Naliunga mkono, lakini tatizo langu liko katika mfumo wa utekelezaji wake. Ni kweli tunahitaji kuwezesha usafari katika Jiji la Dar es Salaam na pengine katika majiji na miji mingine nchini kote kuweza kuwa na usafiri wa uhakika ili kupunguza misongamano. Mathalani, kutumia saa mbili hadi saa tatu kutoka Kimara hadi Posta au Kariakoo ni changamoto kubwa. Kwa hali kama hiyo, rasilimali muda na rasilimali fedha vinatumika isivyostahili na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa letu na kwa watumiaji wa barabara.
Lakini pia magari mengi yanapokaa muda mrefu barabarani yanachafua hewa kwa kuzalisha gesiukaa nyingi. Kwanza, magari mengi ni machakavu hivyo utumiaji wa mafuta ni mkubwa.
Kwa bahati mbaya gesiukaa inaishia angani na kuchanganyika na gesi nyingine katika mfumo wa hewa. Hii inaleta madhara makubwa kwa afya zetu maana tunavuta gesi ya oksijeni iliyochanganyika na gesi nyingine zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.
Kwa bahati mbaya Jiji la Dar es Salaam limejaa nyumba tu na maeneo yenye miti au misitu inayotakiwa kuiondoa gesiukaa kutoka angani haipo ya kutosha. Maeneo ya Pugu na Kazimzumbwi yalihifadhiwa tangu miaka ya 1950; ambayo yanatarajiwa kuwa na misitu au miti mingi yenye uwezo wa kunyonya gesiukaa kutoka hewani na kuitumia kulingana na mfumo wa kiikolojia. Lakini maeneo hayo yamezongwa na binadamu na kuzidi kuharibiwa kila kukicha kwa kutaka kujenga nyumba na kuendesha shughuli nyingine za kibinadamu kama kilimo na ufugaji. Kwa hali hiyo Dar es Salaam inazidi kuzongwa na athari za gesiukaa na kuwafanya wakazi wake kuwa na afya zisizoridhisha na maendeleo duni.
Sasa suala la kujenga barabara za mabasi mwendokasi linalenga kutatua kero ya msongamano wa magari. Je, ni kweli msongamano wa magari utaisha au kupungua? Barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi katikati ya jiji ilikuwa na njia mbili za magari kupita kwa wakati mmoja. Ilikuwa nzuri tu yenye kiwango cha lami. Hata hivyo, ilifumulia na kutengenezwa upya bila ya kujali gharama kwa kutumia fedha tulizopata kutoka Benki ya Dunia (kama ni mkopo nafuu au msaada; yote heri).
Kilichoongezeka hapo ni njia mbili kwa mabasi ya mwendokasi. Magari binafsi na malori yamebaki na njia mbili kama ilivyokuwa hapo awali. Je, kwa hali hiyo tutaweza kupunguza msongamano wa magari kama inavyokusudiwa? Nauliza hivyo kwa sababu bado huduma nyingi za kiofisi, kijamii na kibiashara zitaendelea kupatikana na kutolewa katika maeneo ya Posta na Kariakoo na sehemu nyingine katikati ya jiji hivyo kulazimisha magari mengi kwenda kwenye maeneo hayo.
Baadhi ya watu wanasema tusubiri hayo mabasi ya mwendokasi yaanze kutoa huduma na tuangalie hali itakuwaje. Iwapo wengi wanaotumia magari binafsi kwenda katikati ya jiji watayaacha magari yao nyumbani na kutumia mabasi ya mwendokasi, pengine foleni za barabarani zinaweza zikapungua. Sina hakika kama hali itakuwa hivyo, lakini tusubiri matokeo.
Kusema kweli hali bado itakuwa ngumu maana wenye magari binafsi watayaacha au kuyaegesha wapi (packing) hapo Kimara Mwisho ili wapande mabasi ya mwendokasi? Naona bado itakuwa kitendawili kwa maana miundombinu katika eneo la Kimara haitoi nafasi ya mahali pa kuyaegesha ili kutumia mabasi ya mwendokasi.
Nikiri kwamba katika harakati za kutafuta ufumbuzi wa changamoto za misongamano ya magari katika Jiji la Dar es Salaam, hapakuangaliwa vizuri visababishi vya msingi kwa misongamano ya magari.
Kwa mtazamo wangu, kwanza tungeanzia sehemu za makutano ya barabara kuu ambako kuna taa za kuongoza magari kama sehemu za Ubungo, Magomeni, na Fire. Vilevile, na kuangalia maeneo mengine ya Morocco, Tabata Relini, Buguruni na Tazara. Kwa kuwa magari hulazimika kusimama yanapofika maeneo hayo, ilitakiwa suluhisho kwa misongamano ya magari lianzie sehemu hizo. Hii ni kwa sababu hali hiyo husababisha magari kusimama na kuwa chanzo cha misururu mirefu barabarini.
Uamuzi ungefanyika kwamba kwanza tujaribu kutatua tatizo la msongamano wa magari kwa kujenga miundombinu ya kuwezesha magari kupita juu na chini (fly overs) bila kusimama. Iwapo maboresho yangeanzia sehemu hizo na ikaonekana kuwa bado kunakuwapo na foleni ndefu barabarani, hapo tungefikiria kuongeza njia zaidi za kupeleka na kutoa magari katikati ya jiji.
Lakini kwa kufumua barabara iliyokuwa nzuri na kuijenga upya kwa minajili ya kuingiza sehemu ya kupitisha mabasi ya mwendokasi; huku tukifahamu kuwa msongamano wa magari unatokana na taa za kuongoza magari barabarani kwenye sehemu za makutano ya barabara kuu, kidogo uamuzi huu unakuwa na walakini.
Kwa kuwa hakuna hatua iliyochukuliwa kuondoa changamoto ya taa za barabarani, ni dhahiri kuwa suala la mabasi ya mwendokasi halitatoa jawabu kamili la kuondokana na misongamano ya magari barabarani.
Kwanza, tukiri kwamba hiyo barabara inajengwa kwa gharama kubwa sana. Hii ni kutokana na hali halisi nilivyoiona kwa kufumua barabara ya zamani na kuijenga upya. Pili, vituo vya abiria kupandia na kuteremkia ni vingi na vimejengwa kwa gharama kubwa pia. Vifaa kama nondo, kokoto, mchanga, saruji na nguvukazi iliyotumika kwa kila kituo ni kubwa mno ukilinganisha na mahitaji.
Mwanzoni nilifikiri kwamba huenda zitafungwa mashine kubwa ambazo zikiwashwa zinakuwa na mtikisiko mkubwa kiasi kwamba lazima zijengewe sehemu imara (firm foundation) kwa maana kwamba mashime au mitambo itakapowashwa kusiwepo madhara yanayoweza kusababishwa na mtikisiko mkubwa.
Kama nia ni kuwezesha abiria ambao wengi wetu ni wenye uzito katika ya kilo 60 hadi 100; na abiria hawatakuwapo kwa wingi kwa wakati mmoja; vifaa vilivyotumika kujenga vituo na mfumo wake kiujumla ni matumizi ya fedha nyingi mno pasipo sababu za kuridhisha. Pengine waliofanya uchambuzi yakinifu katika masuala haya hawakuwatendea haki Watanzania.
Nasema hivyo kwa sababu hata wajazane watu wengi kwa wakati mmoja kwenye kituo kimoja na halafu warukeruke, bado uzito wao hautaleta madhara kama ambavyo ingekuwa na zile mashine zenye uzito mkubwa. Sisemi kwamba tungejenga vituo hafifu ambavyo baada ya kuvitumia kwa muda mfupi hali yake ikawa mabaya; hapana. Namaanisha kujenga vituo imara, lakini vyenye kugharimu walipakodi fedha kiasi, na siyo kituo kimoja kitumie mamilioni mengi ya shilingi wakati Taifa lina changamoto lukuki katika huduma za kijamii na kiuchumi pia.
Pengine kwa kutumia fedha hizo kutoka Benki ya Dunia tungeliweza kuboresha hata barabara nyingine kadhaa katika Jiji la Dar es Salaam na kuongeza chachu za kimaendeleo kwa maeneo mengi ya Jiji.

>>ITAENDELEA

Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti, Bodi ya Shirika la Kukuza na Kuendeleza Mipingo katika Maeneo ya Vijiji: Mpingo Conservation & Development Initiative (MCDI). Anapatikana kupitia simu 0783 007 400 au barua pepe: [email protected]