Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali wahakikishe wanazingatia uadilifu katika matumizi ya fedha ili uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Pia,Majaliwa amewaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara zote ambazo baadhi ya watumishi wake wake bado wako Dar Es Salaam wahakikishe wanahamia Dodoma kama ilivyoelekezwa na Serikali. “ Simamieni agizo hili kikamilifu.”
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Septemba 5, 2022) wakati akizungumza baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua maendeleo ujenzi wa Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma, ambapo amewashukuru na kuwapongeza wakandarasi wanaojenga mji huo.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ujenzi wa Makao Makuu unaendelea vizuri ni nzuri na lazima tujivunie maono ya viongozi na kazi nzuri wanayoifanya pamoja na kazi nzuri za wataalamu wetu.”
Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa mji wa Serikali utakuwa wa kisasa kwa kuwa utaendeshwa kidijitali “fedha za kutekeleza haya zipo na ninawahakikishia kila kitu kitakamilika, dhamira ya Rais Mheshimiwa Samia ni kufanya makao makuu kuwa bora zaidi.”
Kadhalika, Majaliwa amewasisitiza vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi katika mradi huo waendelee kufanyakazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na waendelee kuzingatia maelekezo wanayopewa viongozi wao ili wawe na uwezo wa kujenga na kusimamia kazi zao.
Majengo ambayo yamekaguliwa ni Jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu linalojengwa na Suma JKT kwa gharama ya shilingi bilioni 22.8. Ujenzi wake ulianza Oktoba 11, 2021 na unatarajiwa kukamilia Aprili 17, 2023. Jengo hilo lenye sakafu sita, ujenzi wake umefikia asilimia 46.
Jengo lingine ni Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu linalojengwa na Suma JKT kwa gharama ya shilingi bilioni 18.62. Ujenzi wake umefikia asilimia 47, ulianza Oktoba 18, 2021 na unatarajiwa kukamilia Aprili 17, 2023. Jengo lina sakafu sita.
Pia, alikagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais TAMISEMI linalojengwa na kampuni ya M/S Corporation kwa gharama ya shilingi bilioni 20.29. Ujenzi wake umefikia asilimia 54, ulianza Oktoba 15, 2021 na unatarajiwa kukamilia Oktoba 14, 2023. Jengo lina sakafu sita.
Jengo lingine lililokaguliwa ni Wizara ya Maliasili na Utalii linalojengwa na kampuni ya M/S Li Jun Development Construction Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 16.41. Ujenzi wake umefikia asilimia 69, ulianza Novemba 23, 2021 na unatarajiwa kukamilia Novemba 22, 2023.
Pia, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali linalojengwa na kampuni ya SUMA JKT kwa gharama ya shilingi bilioni 26.81. Ujenzi wake umefikia asilimia 42, ulianza Septemba 9, 2021 na unatarajiwa kukamilia Septemba 15, 2023. Jengo lina sakafu tano.
Mradi mwingine uliokaguliwa ni ujenzi wa jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa gharama ya shilingi bilioni 22.30. Ujenzi wake umefikia asilimia 45.05, ulianza Oktoba 15, 2021 na unatarajiwa kukamilia Oktoba 14, 2023.
Pia, alikagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora linalojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 21.64. Ujenzi wake umefikia asilimia 54, ulianza Septemba 21, 2021 na unatarajiwa kukamilia Machi 20, 2023. Jengo lina sakafu sita.
Awali, Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Mji wa Serikali, Meshack Bandawe alisema awamu ya pili ya ujenzi wa mji huo ilianza Oktoba 2022 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2023. Mradi huo unahusisha majengo 25 ya wizara pamoja na majengo mawili ya taasisi za umma.
Bandawe amesema mradi huo ambao umefikia kata ya asilimia 39 na 45 unajengwa wakandarasi tisa wakiwemo wa Serikali na binafsi umetoa ajira 2,149. Alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 675 hadi kukamilika kwake.