Serikali Kuu na Manispaa ya Kinondoni wameruhusu ujenzi wa Shule ya Saint Florence Academy iliyopo Mikocheni “B”, Dar es Salaam juu ya barabara.
Hatua hiyo, licha ya kuwa imevunja sheria za Mipango Miji, imekuwa kero na hatari kwa usalama wa wanafunzi na majirani wa kiwanja hicho namba 622.
Pia imebainika kuwa mmiliki wa shule hiyo pamoja na familia yake, wanaishi na wanafunzi ndani ya eneo la shule hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa mmiliki amepata vibali cha kuanzisha shule kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, licha ya eneo hilo kukosa sifa za kujengwa shule.
Sifa mama ilizokosa ni kwamba eneo ilipojengwa ni dogo mno; na pili, ujenzi wa baadhi ya madarasa umefanywa juu ya barabara na hivyo kuuziba kabisa mtaa.
Taarifa za kufungwa kwa barabara hiyo zimeshafikishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, lakini hakuna hatua zilizokwishachukuliwa. Mmiliki wa shule hiyo anatajwa kuwa ndiye pia mwenye maslahi na baa maarufu ya Rose Garden iliyopo jirani.
Baa hiyo iliwahi kuwagonganisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba; na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli. Makamba alitaka kumuondoa eneo hilo kwa maelezo kwamba ni la hifadhi ya barabara, lakini Dk. Magufuli alimtetea kwa kile kilichokuja kubainika baadaye kuwa ni maelekezo aliyokuwa akiyapata kutoka juu.
Ramani ya eneo la shule ya Saint Florence Academy inaonyesha kuwa mahali yalipojengwa madarasa kadhaa na ofisi za shule hiyo ni la barabara. Eneo la nyuma nalo limemegwa bila kuwa na vibali na sasa kumeongezwa madarasa na mabweni.
Kwa mujibu wa ramani, eneo ambalo shule imejengwa, pamoja na familia inamoishi lina ukubwa wa mita 30 kwa 30. Kwa mujibu wa Waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa mwaka 2011, shule iliyo mjini itapata usajili endapo itakuwa na eneo la ukubwa hekta 1.5.
“Shule ina wanafunzi wengi, zaidi ya 500. Barabara ni moja, magari yanayopeleka na kutoa wanafunzi hapa ni mengi. Kama itatokea suala la moto hapa watakufa wanafunzi na watu wengine wengi. Kuna kelele nyingi hapa, uharibifu wa mazingira kwa majirani ni mkubwa. Kuna mapipa ya taka yananuka, kuna moshi unaotoka shuleni unaudhi majirani.
“Suala hili tumelipeleka Manispaa lakini hakuna suluhisho. Sheria zimevunjwa, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa,” wamelalamika majirani kwenye barua yao kwenda Manispaa ya Kinondoni.
Mwaka 1999, iliyokuwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam, katika barua yake ya Mei 11 ilitamka wazi kuwa mahali kulikojengwa shule hiyo ni makazi ya watu.
Uongozi wa shule hiyo, kwa nyakati tofauti uliomba na kufanikiwa kupewa kibali cha kuendeleza eneo la nyuma ya shule kwa ajili ya kupanda miti na kujenga uwanja wa michezo.
Uamuzi wa uongozi wa shule ulilenga kupunguza hewa chafu inayotoka kwenye mabwawa ya maji machafu, na hivyo kuwa na athari kwa afya za wanafunzi na watu wanaoishi eneo hilo.
Hata hivyo, imebainika kuwa polepole eneo hilo limeanza kuangukia mikononi mwa mmiliki wa shule hiyo kwa kuongeza wigo wa shule.
Julai 22, 2009 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilimwandikia barua mmiliki wa Saint Florence Academy na kusema: “Eneo unaloomba ni eneo lililoachwa wazi kwa ajili ya kuzuia hewa chafu kutoka kwenye mabwawa ya majitaka yaliyopo eneo hilo…Kuna mtindo wa baadhi ya wana mazingira wasio waaminifu ambao mara wapewapo idhini ya kuotesha miti katika eneo fulani wanatumia eneo hili kwa matumizi mengine kinyume cha taratibu. Kwa barua hii unapewa idhini ya kuotesha miti na kuitunza ili eneo hili lipendeze na liwe endelevu na si vinginevyo.” Barua hiyo ilisainiwa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo aliyetambulika kwa jina la Mkomba.
Pamoja na kutambua kuwa eneo ambalo shule hiyo imejengwa halikidhi sifa za kisheria za kuanzisha shule; Wizara ya Elimu imetoa kibali cha ujenzi wa shule. Aidha, licha ya Manispaa ya Kinondoni na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutambua kuwa sehemu hiyo inapaswa ipite barabara, mmiliki wa shule hiyo amejenga juu ya barabara hiyo na kuiziba kabisa.
WARAKA WA ELIMU NA. 10 WA MWAKA 2011
MASHARTI MAPYA YA USAJILI WA SHULE
Waraka huu unakazia Mwongozo wa Usajili wa Shule uliotolewa mwaka 1982. Sehemu ya Waraka Na. 10; ambao kimsingi ni mwendelezo wa Mwongozo wa mwaka 1982 ambao “unatengua” usajili wa Saint Florence Academy. Unasema:
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ndiyo msimamizi wa Elimu nchini kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 na sheria ya Elimu Na.25 ya Mwaka 1978 na rekebisho lake Na. 10 la Mwaka 1995.
Mashirika, taasisi mbalimbali na watu binafsi wenye uwezo wa kuanzisha shule zisizo za serikali hapa nchini, wanashauriwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara.
Mwenye nia na uwezo wa kuanzisha Shule/Chuo cha ualimu ni lazima atomize masharti yafuatayo:-
• Awe na eneo lisilopungua Hekta 3 kwa maeneo ya vijijini na 1.5 kwa eneo la mjini lililotolewa kwa madhumuni ya Elimu na Mamlaka husika (Wizara ya Ardhi na Serikali za vijiji).
• Aombe kibali cha kujenga majengo ya shule/chuo kwa kufuata ramani zilizopendekezwa na Wizara ama zitakazokubaliwa na Wizara na ambazo
zimepitishwa na mamlaka za Halmashauri husika (Mhandisi wa Wilaya na Mipango Miji wa Wilaya).
• Akamilishe majengo muhimu ya mwanzo yakiwemo madarasa ya kutosheleza wanafunzi wa mwaka wa I na II, jengo la utawala/ofisi za walimu, bwalo/ukumbi, maabara moja kwa kuanzia, maktaba, vyoo vya wasichana, wavulana na wafanyakazi na samani.
• Aombe kuthibitishwa kuwa Mwenye Shule/chuo na Meneja wa Shule kwa kujaza fomu Na. RS 6 na RS 7 na kuziwasilisha kwa Afisa Elimu wa Wilaya/Mji/Manispaa ilipojengwa shule kwa maoni na mapendekezo. Pia Mwenye Shule/chuo mtarajiwa atatakiwa kuwaomba Maafisa wa Afya,
Mhandisi wa Majengo na Mkaguzi Mkuu wa Shule (wote wa Wilaya) Mji/Manispaa wafanye ukaguzi na taarifa zao zitatumiwa kuona hali halisi na utayari wa majengo na mazingira ya shule/chuo.
Baada ya Mwenye Shule/Chuo na Meneja kuthibitishwa atajaza fomu na. RS. 8 ya kuomba kusajili Shule/Chuo. Fomu hii itawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Shule wa Kanda shule ilipojengwa. Endapo shule ina sifa stahili itasajiliwa na kupewa namba ya usajili na ndipo itaruhusiwa kuandikisha wanafunzi.
Tendo la kusajili litakuwa endelevu, na litajirudia kila baada ya miaka minne (4) ili kuhakikisha kwamba viwango vilivyowekwa vinazingatiwa.
Shule/Chuo kitasajiliwa iwapo kitakuwa kimetimiza masharti yote ya usajili na kupewa namba ya mtihani.
Waraka huu unafuta nyaraka zote za nyuma na unaanza kutumika kuanzia Januari, 2012.
M. M. Wassena
KAIMU KAMISHNA WA ELIMU
Manispaa ya Kinondoni
Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhohela, ameliambia JAMHURI kuwa si kila anayelalamika yuko sahihi na wengine wameamua kufanya hivyo tu.
“Kazi zetu siyo kukaa ofisini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameweka dawati la malalamiko kwa kila Halmashauri; sasa inatakiwa elimu gani? Au tuwapigie ngoma?” Amehoji Mhohela kwa ukali.
Anasema watu wamekuwa wakikimbilia kwa Mkurugenzi wa Manispaa kupeleka malalamiko yao na kujikuta wakitakiwa kufuata utaratibu kwa kuwaona wakuu wa idara.
Hata hivyo, amekwepa kujibu swali lililohoji sababu za kuruhusu ujenzi wa Shule ya Saint Florence Academy ndani ya barabara na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine na majirani.
Hata hivyo kwa vigezo vya sera ya elimu eneo hilo lilipojengwa shule ya saint Florence Academy halina ukubwa unaohitajika na liko kwenye makazi ya watu.
Mmiliki wa shule
Mkurugenzi wa Shule hiyo, Flora Assey amelieleza JAMHURI kwamba suala la kujenga shule eneo hilo la barabara ni la kawaida kwani hata katikati ya jiji kuna shule nyingi zimejengwa.
“Hakuna njia kule, kuna mabwawa na matuta yameinuliwa juu, pia kuna uzio kwa hiyo njia wanayosema nimeiziba kwa kujenga shule, haipitiki,” anasema Assey.
Kero nyingine wanayoipata watu wanaoishi jirani ni takataka zinazozalishwa shuleni hapo ambazo hutupwa hovyo na kusababisha harufu kali kwenye makazi ya majirani.
Wizara ya Elimu
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, aliyefahamika kwa jina la Bunyazu, ameeleza kuwa ziko taratibu zinazomtaka mtu anayehitaji kuanzisha shule kuzifuata.
Alipoulizwa kuhusu shule hiyo iliyojengwa kwenye barabara, amesema suala hilo litashughulikiwa mara baada kupata taarifa za kutosha.
Hata hivyo, alisema Manispaa ya Kinondoni ndiyo watoaji wa vibali, kwa hiyo kama kuna makosa, yalianzia huko.
Januari, mwaka huu akiwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene alisimamia ubomoaji wa jengo la mghahawa lililojengwa kinyume cha sheria ndani ya eneo la wazi la bustani katika Mtaa Samora. Jengo hilo lilikuwa mali ya kampuni ya Easy Payment Limited.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya JAMHURI kuandika kuhusu viongozi wa Jiji la Dar es Salaam ‘kuuza’ eneo hilo.
Manispaa ya Kinondoni imetajwa kuwa ndiyo inayongoza nchini kwa kuwa na uvunjifu mkubwa wa sheria za mipango miji. Tatizo kubwa linalolalamikiwa ni la watendaji wasio waaminifu.