Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Kibaha
Halmashauri ya Mji Kibaha ambayo imepewa dozi 40,000 ya chanjo ya matone ya kutokomeza polio inatarajia kutoa chanjo hiyo kwa watoto wasiopungua 38,748 kwa awamu hii kwenye Kata 14 na Mitaa 73 inayounda Halmashauri hiyo ambapo tayari watoto 11,347 sawa na asilimia 30.3 wamepata chanjo kwa siku ya kwanza .
Awali akiwasilisha taarifa ya mikakati ya kufanikisha zoezi hilo, kwenye kamati ya PHC,Mratibu wa chanjo Halmashauri ya Mji Kibaha Hope Rutatina ,amesema jumla ya timu 69 zenye wataalam watatu kila moja zimeundwa kwa ajili ya kufanikisha na kwamba zitatembea nyumba kwa nyumba ili kuwafikia walengwa.
Mganga Mkuu wa Halmashauri Dkt.Tulitwen Mwinuka almetoa rai kwa wazazi na walezi wote kuhamasika na kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa bure ili kuepuka gharama kubwa za kumtibia mgonjwa wa polio kwani madhara yake ni Makubwa.
“Ndugu wajumbe wa PHC niwaombe tushirikiane kuwahamasisha wananchi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma ya chanjo,chanjo hii ni salama na imegharamiwa na Serikali.Tuwape Elimu kuwa madhara ya ugonjwa wa Polio ni Makubwa ikiwa ni pamoja na ulemavu wa viungo ambavyo matibabu yake yanahitaji fedha nyingi.Chanjo zipo nyingi na mara zote zimekuwa na mafanikio ya kuzuia maradhi” alisema Dkt.Mwinuka
Dkt.Mwinuka aliongeza ,chanjo hiyo inatolewa kwa kila Mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano hata kama alishawahi kupata awali kwani ugonjwa wa Polio ni hatari hivyo amewasihi Wazazi na walezi kuondoa shaka kwani iwapo Mtoto atapata madhara Serikali itagharamia matibabu yake.
Taarifa za kitabibu zinaonesha kuwa chanzo cha ugonjwa wa Polio husababishwa na kirusi ambacho huambukizwa kutoka kwa mtu aliyeathirika kwenda kwa mtu mwingine kwa kula au kunywa kitu kilichochafuliwa na kinyesi chenye virusi vya Polio.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeanza zoezi la Kitaifa la kutoa chanjo ya matone ya kutokomeza Polio kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano kuanzia Septemba 1,2022 kukiwa na lengo la kuwafikia watoto 12,386,854 Kitaifa katika awamu hii ya tatu.