4.+Nape+akihamasisha+kwenye+mkutano+huo,+Kushoto+ni+Mlezi+wa+mkoa+wa+Dar,+Abdulrahman+KinanaMiezi miwili iliyopita niliandika makala katika safu hii yenye kichwa cha habari kisemacho: “CCM inaanguka taratibu kama dola ya Warumi”.
Katika makala hiyo, nilieleza kuwa viongozi wapo kwenye sherehe na safari za ugaibuni. Kwa nadra sana wanafahamu kinachoendelea nyumbani. Dola ya Warumi ilikuwa dola kubwa ulimwenguni.
Ilianguka si kwa sababu nyingine, bali wafalme na wanafamilia katika koo za kifalme waliacha kufanya kazi. Waliigeuza Ikulu yao nyumbani kwa sherehe. Ndani ya familia kila mtu akawa kiongozi. Mama akawa sehemu ya serikali, watoto wakawa watendaji na wajukuu wakawa wabunge. Muda wote ukoo ukawa unajadili jinsi ya kuongoza dola ya Warumi.


Wakaanza kupanga mipango ya kurithishana uongozi kizazi hadi kingine, bila kuwaza fedha za kuendesha Serikali wanayopanga kuiongoza kwa miaka 100 hadi 200 zingepatikanaje.
Katika familia ya kifalme kila mwanafamilia alikuwa na vijakazi wapatao 300. Mwisho wa siku wakawa hawawalipi mishahara, hawawapi matibabu wauguapo, elimu wakaitelekeza, maji wala umeme haikuwa tena ajenda, barabara zikiwa mbovu hawatengenezi na wala hakuna usafiri.
Hali ilipofikia hapo, vijakazi wakaungana. Wakawa na mijadala na vikao visivyo rasmi, wakaona wazalishaji ni wao, wanakusanya mapato yanakwenda kwa wakubwa ambao wapo kwenye vikao kila kukicha na vikao vikiambatana na mvinyo mwaka hadi mwaka, na wakati mwingine hata vijakazi walipopeleka mapato wakubwa walikuwa ‘bwiii’ hata wakathubutu kuwaambia walale na fedha waziwasilishe kesho yake.


Ilipofikia hapo, vijakazi wakaanza kupiga ‘panga’ vijisenti vya wakubwa baada ya makusanyo, kidogo kidogo wakawa wanaweka akiba, mwisho wa siku wakawa na mtaji na wakati mwingine wakajikuta na ukwasi zaidi ya mabosi wao. Hapo ndipo vijakazi walipojitangazia uhuru, wakaamua kuwatangazia mabosi wao kuwa wakati umefika wa wao (vijakazi) kuongoza dola.

Sitanii, nadhani wengi tunakumbuka yaliyowapata wafalme wa Kirumi. Wengi walikimbia makazi wakaanza kuomba sigara kwa vijakazi wakidhani ni watawala wenzao. Sina uhakika sana kama hapa kwetu hali iko tofauti. Najua kwetu hatutatumia mkondo wa mapanga kama walivyofanya Warumi, ila sanduku la kura litasema zaidi.


Tulipo sasa hatuna tofauti na wajenzi wa mnara wa Baberi. CCM nilitaraji kuwa ni chama chenye kandarasi ya kuwasaidia Watanzania. Nilitaraji kuwa kinafahamu fika adhima yake ya kufuta ujinga, maradhi na umaskini. Maadui hao ndio mnara wa Baberi wa taifa hili. Wabunge, wajumbe wa NEC na makada wa CCM walipaswa kushirikiana kuujenga.
Walipaswa kuzungumza lugha moja kupeana mawe, kokoto, mchanga, maji na beleshi kwa nia kuchanganya zege kujenga mnara huo. Nilitaraji awepo kiongozi, ambaye akichoka au akahitimisha muda wake wa uongozi, basi hata wenzake alionao katika safari ya kujenga mnara huo wanajua nani atashika hatamu.
Msumbiji, Botswana, bila kutaja nchi kama Marekani na Uingereza wamekwishafikia hapo. Rais anayeondoka madarakani anakuwa akifahamu nani anayeweza kuendeleza dira ya taifa, bila kujali atatokea chama tawala au upinzani, na ndiyo maana kwa nchi zilizoendelea viongozi wa upinzani wanapewa taarifa za kiusalama za nchi.


Sitanii, nimeshitushwa mno na utitiri wa watangaza nia waliojitokeza kuomba kuteuliwa na CCM kuwa marais wa nchi hii. Wakati naandika makala hii, nasikiwa wamefikia 38.  Naomba niwataje tu, kuwa ni Prof. Mark Mwandosya, Stephen Masatu Wasira, Balozi Amina Salum Ali, Charles Makongoro Nyerere, Amos Robert Siyatemi na Frederick Tluway Sumaye.
Mohamed Gharib Bilal, Ali Karume, Edward Ngoyai Lowassa, John Pombe Magufuli, Prof. Sospeter Muhongo, Samwel John Sitta, Titus Mlengela Kamani, Mwigulu Lameck Nchemba, Mussa Godwin Mwapango, Razaro Samwel Nyalandu, Peter Isaiah Nyalali, Leonce Nicholas Mulenda, Bernard Kamilius Membe na Luhaga Joelson Mpina.
Wengine ni Mwelecele Ntuli Malecela, Hamis Andrea Kigwangalla, Mathias M. Chikawe, January Yusufu Makamba, William Mganga Ngeleja, Boniface Thomas Ndengo, Lidephonce M. Bilohe, Hassy Besen Kitine, Dk. Augustine Philip Mahiga, Mizengo Kayanza Pinda, Dk. Muzzamil Mussa Kalokola, Maliki Salum Marupu, Dk. Asha-Rose Migiro, Jaji Augustine Ramadhan na Dk. Harrison Mwakyembe.


Kinachoniskitisha kati ya wagombea wote hawa ni kauli zao juu ya dhamira ya iwapo wataingia madarakani wataifanyia nini nchi hii. Hili nimeliandika katika makala ya wiki iliyopita, lakini nalisisitiza leo. Nchi yetu inahitaji kiongozi atakayesimamia viongozi wenzake na kuwekeza katika uchumi wa viwanda.
Kauli yoyote isiyolenga katika uwekezaji na hasa wa kusaidia wazawa, itakuwa hailengi kulikomboa taifa hili. Itakuwa inalenga kuendeleza yale yale, kwa staili ileile ambapo tumefika sasa shilingi ya Tanzania inakimbilia Sh 2,400 kwa dola moja.
Ukiuliza wanasema dola imepata nguvu dhidi ya sarafu nyingine duniani, ukiuliza kwa nini wanasema uchumi wa Marekani umeimarika, ukiuliza uchumi wa Tanzania je, wanakwambia watakupigia baadaye!
Sitanii, nirejee katika mada inayonipa hofu juu ya ustawi wa CCM. Kwamba katika kipindi cha miaka 10 wapo wana CCM 38 waliokuwa wanakodolea macho urais wa Rais Kikwete? Hii inanipa hofu. Inaniogopesha iwapo walikuwa wanafanya kazi alizotuma wamsaidie katika uongozi wake au walikuwa chini kwa chini wanatafuta fursa ya kujipatia umaarufu baadae nao washike hatamu.


Kinachonishangaza kingine, ni kasi ya kusemana kwenye majukwaa. Napata shida kuamini kuwa hotuba zinazotolewa wakati wa kuchukua fomu zitatosha kumwezesha mtu yeyote kuteuliwa na chama na hata ikitokea hivyo kuwa ataweza kuendesha nchi. Kwamba mtu hakujiandaa kugombea urais huku akifanya kazi kututhibitishia kuwa anafaa, leo anasema akipewa usukani tutamuona utendaji wake linanipa tabu.
Watanzania wenzangu kwa sasa tuyasikilize na tuyapime maneno ya wagombea wetu. Tujifanye kama tunafanya kazi kwenye kiwanda cha sumu. Sumu haijaribiwi ubora kwa kuonjwa, bali kwa vipimo vya watalaam na uzoefu kuwa aina fulani ya sumu huua panya. Ukienda dukani unasema nipe aina fulani ya sumu ya panya, huhitaji mwonjaji bali moja kwa moja inaua panya. Kuna baadhi ya wagombea ni hatari. Ni wa kuweka mbali na watoto. Uongo ndio msingi wa utendaji wao. Jambo pekee la kweli wanalosema maishani ni pale wanapotaja majina yao!
Sitanii, yapo maneno kuwa baadhi ya wagombea wametumwa kuvuruga mchakato. Mwanzo niliyapuuza lakini sasa naelekea kuyaamini. Dhana ya mtu kuombwa kugombea uongozi inanifanya niamini kuwa mtu huyu hajui nchi hii akipewa uongozi ataipeleka wapi. Enzi za ufalme ilikuwa sahihi, lakini kwa sasa tunataka Rais mwenye ndoto iwapo atachaguliwa atafanya nini kwa nchi hii.


Tunahitaji kujengewa matumaini mapya na kubadilisha fikra zetu. Nchi yetu imeingia katika lindi la kutegemea wafadhili. Wengi wakimwona mgeni wanajua neema imewadia. Wachache wenye fikra za kuanzisha viwanda, kilimo cha kisasa, ufugaji na kujenga nyumba bora. Tunapaswa kuhubiri uzalishaji na kuanzisha mchakamchaka wa maendeleo.
Nimesema wiki iliyopita kuwa nchi yetu ukiacha mazao waliyoacha wakoloni, kahawa, katani, korosho, pamba na mengine, hakuna ubunifu tuliofanya. Leo hatuna sababu ya kuwa na njaa katika taifa hili. Serikali ijayo inapaswa kwenda bungeni Rais akapitisha Azimio la Kilimo. Azimio hili liwe tofauti na la Musoma la Mwaka 1975 la Kilimo cha Kufa na Kupona.
Likipitishwa bungeni wakubali hata kwa fedha za uma kuanzisha kiwanda kimoja tu cha kuzalisha trekta hapa nchini. Kiwanda hicho kifyatue trekta ziuzwe vijijini na wataalam wa ugani wapelekwe kuzisimamia. Tulime mpunga, mahindi, karanga, dengu, mawese, maharage, viazi na miti ya mbao. Majirani zetu wengi waliotuzunguka wana njaa kali.


Mazao yote niliyotaja hapo juu tutawauzia na kupata fedha za kigeni. Hawatanunua tena mchele kutoka Thailand. Kilimo Kwanza ni kweli kimesaidia kuganga njaa kwa Watanzania. Karibu kila familia sasa ina chakula, ila tunataka mapinduzi ya kilimo. Kiwanda cha trekta kisamehewe kodi zote. Kikizalisha trekta za kutosha hapa nchini tutaanza kuuza hata kwa majirani zetu.
Sitanii, tunahitaji uongozi kama wa Nsa Kaisi alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera mwaka 1984. Alitembeza kiboko kwa wanaume waliokuwa wanashinda kwenye pombe kama Rombo, wakakimbilia kwenye matingatinga (amashanga) kulima viazi na mihogo. Mwisho wa siku walizalisha chakula kingi hadi wakasaza. Natamani serikali ijayo wakuu wa mikoa wote, wakuu wa wilaya wote na wizara nyeti ikiwamo ya fedha wawe askari.
CCM ya sasa haiyawezi hayo. Wanawaza kutukanana, kutafutiana kashfa na ndio maana wamewekwa mapandikizi wanaosafisha njia za mabwana. Nilitaraji kauli nzito kwa wagombea hawa mtu atupe ahadi kuwa akichaguliwa atajenga viwanda angalau vitano ndani ya miaka 10, akianza na viwili kipindi cha kwanza na kumalizia na viwanda vitatu vikubwa kipindi cha pili.


Leo wanashindana kutengenezeana zengwe. Kama nilivyosema hapo juu, wamepishana lugha. Mnara wa Baberi wakimtuma mtu saruji anakuja na ndoo ya maji. Wanatukanana bila kujua kuwa baada ya kuivua nguo Serikali ya Rais Kikwete wakati wa kuomba kuteuliwa ndani ya CCM kuna mlima wa kupanda watakapokutana na wapinzani kipenga kitakapopulizwa Agosti.
Yale yale wanayodhani yatawasaidia dhidi ya washindani wao, wapinzani watayawasilisha kwa wananchi na kueleza udhaifu wa CCM na wagombea wake. Tunakumbuka jinsi Wislon Mukama alivyoiua CCM kwa kudhani anapambana na Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge. Alizunguka na John Chiligati wakiwaita wenzake magamba.


Sitanii, nilidhani baada ya Lowassa kuondoka serikalini, Rostam akajiuzulu huo ndio ungekuwa mwisho wa ufisadi ndani ya CCM kama walivyoiaminisha jamii akina Mukama na Chiligati. Hata baada ya hao kuondoka ukatokea wizi mkubwa wa Escrow kuliko waliyokuwa wakitueleza. Ni kwa misingi hiyo napata shida ya kuamini wanachosema walio wengi katika mchakato huu.
Kwa sasa wanapambana na gombea mmoja tu, Lowassa. Kila mgombea amejipanga kupambana na Lowassa kana kwamba Lowassa sasa ni sera ya CCM. Nimemfurahia Mwakyembe. Ameeleza akiteuliwa atafanya nini na asiposhinda kuwa atamuunga mkono yeyote atakayeteuliwa na CCM. Pinda halikadhalika, anawambia wasichafuane. Jaji Ramadhan hajapambana na watu anajenga hoja atafanya nini.


Naomba kuhitimisha makala hii kwa kuihusia CCM kuwa inaweza kuamua kupitisha mgombea inayedhani itatumia Jeshi la Polisi kumpa ushindi au mashine za BVR kuiba kura kama walivyofanya Kenya, lakini hatari iliyopo kura zinaweza kuwa nyingi za wapinzani wake mkaiba (kama kuna mpango huo) hadi viroba mlivyoandaa vikajaa zikasalia na za mgombea wenu zisitoshe. Nyomi ya vijana waliojindikisha inatisha.
Sitanii, Watanzania tuanze kujiandaa kisaikolojia. Watendaji serikalini anzeni kujiandaa kisaikolojia kuwa UKAWA wasipogawanyika na CCM ikafanya uamuzi wa mkomoeni bila kuruhusu demokrasia kufanya kazi ndani ya chama, mwisho wa CCM si zaidi ya Oktoba. Mungu ibariki Tanzania.