Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ametangaza kuondoa katazo lililokuwa likizuia mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi kutoruhusiwa kupakia abiria au kushusha katika vituo binafsi na badala yake ameruhusu utaratibu huo kuendelea kwa sharti la kila basi kuingia ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli.
RC Makalla ametoa maamuzi hayo wakati wa kikao cha pamoja baina ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),wamiliki wa stendi binafsi na Halmashauri ya Ubungo na kubaini pasipokuwa na shaka kuwa waliotengeneza vituo binafsi walifuata taratibu na kupatiwa vibali na LATRA baada ya kukidhi vigezo.
Miongoni mwa vigezo vilivyotolewa na LATRA ili kuruhusiwa kuanzisha stendi binafsi ni pamoja na uwepo wa vyoo, sehemu ya mapumzimo kwa abiria, virutubisho na sehemu ya maegesho.
Kutokana na hilo, RC Makalla ameridhia vituo binafsi vitano vilivyohakikiwa kuendelea kutoa huduma na kufungua milango kwa wamiliki wengine wanaohitaji kuwa na vituo binafsi kushirikiana na LATRA ili wapatiwe vigezo vinavyohitajika ambapo wamepewa mamlaka ya kufuta au kutoa leseni.
Aidha, RC Makalla ameagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kukaa kikao mara moja na wamiliki wa stendi binafsi ili kuona njia bora ya ukusanyaji wa mapato.