Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unakuwa imara, endelevu na stahimilivu kwa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa mfuko huo ni moja kati ya mfumo unaotumika katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa nchini.
Hayo ameyasema na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari leo Septemba Mosi, 2022 kwenye ofisi za NHIF jijini Dodoma.
“Niwatoe wasiwasi wadau wote wakiwemo wanachama, watoa huduma pamoja na Watanzania wote kuwa mfuko wa NHIF utaendelea kuwepo na kutoa huduma kama kawaida kwa wananchi kwa kuwa mfuko huu ndio umekuwa tegemeo la Watanzania wengi hususani wa kipato cha chini, Mfuko huu pia ndio umekuwa tegemeo la vituo vya kutoa huduma za afya nchini,” amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema pamoja na kuwa na wanachama asilimia nane (8) tu ya Watanzania wote, vituo vingi vya kutolea huduma vinategemea mapato kutoka katika Mfuko kwa zaidi ya asilimia 70.
“Ili kuhakikisha mfuko wetu unakuwa endelevu na imara zaidi katika kuwahudumia wananchi tumeona uendelevu wa mfuko huu kuwa unategemea sana ongezeko la wanachama watakaoandikishwa katika Mfuko huu,”amesema Waziri Ummy.
Waziri ummy ameendelea kubainisha kuwa, mfuko huo unahudumia takribani wanufaika milioni 4.8 ikilinganishwa na wanufaika 691,173 waliokuwa wakihudumiwa mwaka 2001/02 hivyo uwepo wa takribani asilimia 99 ya wanachama waliojiunga kwa hiari ambao ni wagonjwa imekuwa ikiongeza gharama za matibabu zinazolipwa na mfuko.
Aidha, imebainika kuwa ili mfuko huo uweze kuendelea lazima hatua stahiki zichukuliwe ikiwemo hatua ya kuimarisha afua za kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuongeza idadi ya wanachama, kudhibiti vitendo vya udanganyifu, kudhibiti matumizi ya huduma yasiyo na tija, kupunguza gharama za matibabu nchini na kuwa na Mfumo endelevu wa kuhakikisha Mfuko unakuwa na fedha wakati wote.
Changamoto kubwa ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni wagonjwa na hatua hii imetokana na kutokuwepo kwa Sheria ya ulazima kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itaweka mazingira kwa kila mtanzania kuwa na bima ya afya ili kuwezesha dhana ya kuchangiana gharama za matibabu na hivyo kuwaepusha wananchi katika hatari ya janga la umaskini pindi wakiwa wagonjwa.
Mwisho Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka Watanzanzia kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ili kuweza kupata huduma hata pindi mwananchi anapokuwa hana fedha za kumudu gharama kwa wakati huo.