Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kuwasajili na kuwawezesha wakandarasi na wahandisi wazawa ili waweze kunufaika na fursa za miradi ya ujenzi inayoendelea nchini.
Amesema hayo jijini Dodoma, katika taarifa yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na kusisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wahandisi na wakandarasi wazawa wanaungana katika vikundi ili wanufaike na fursa za kujengewa uwezo wa utaalamu, mitaji, mitambo na uzoefu ili waweze kupata kazi nyingi na kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
“Tumejipanga kuhakikisha wahandisi na wakandarasi wetu wanabobea katika usimamizi wa miradi na mikataba ili kuwawezesha kupata miradi mingi na kujenga hazina ya wataalam wa Sekta ya Ujenzi hapa nchini”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amesema Serikali inajipanga kujenga barabara ya Kibaha – Chalinze – Morogoro ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka jijini Dar es Salaam na kuhakikisha barabara zote kuu na za mikoa zinakuwa katika kiwango bora na kupitika kipindi chote cha mwaka.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso, amehimiza Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), kusimamia vizuri wahandisi wanaosimamia miradi ya Serikali kujengwa katika viwango bora na hivyo kulinda fedha za Serikali kwa kuiwezesha kudumu kwa muda mrefu.
Aidha, amezungumzia umuhimu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kuwezeshwa kupata fedha za kutosha ili barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi ziweze kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na hivyo kuondoa usumbufu kwa wananchi na kuvutia wadau wengi kutumia barabara za hapa nchini.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Balozi Mha. Aisha Amour, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara imejipanga kupambana na rushwa na uzembe katika mizani zote nchini na itaendelea kutoa elimu kwa maofisa wanaosimamia mizani, wasafirishaji na watumiaji wa barabara wakati wote.
Amesema katika kutengeneza uwiano wa wahandisi na wakandarasi, Wizara inaendelea na juhudi ya kuhakikisha wahandisi na wakandarasi wanawake wanasajiliwa kupata fursa za elimu na kushiriki katika miradi ya ujenzi kwa nyanja zote.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepokea, kujadili na kushauri taarifa ya waziri wa ujenzi na uchukuzi kuhusu masuala mbalimbali ya Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuz