Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
BADO kuna changamoto za utoaji taarifa kuhusiana na vitendo mbalimbali wanavyofanyiwa watoto nchini na kuchangia matukio ya ukatili kuendelea kutokea.
Hayo yamebainishwa katika mafunzo kwa wakuu wa vitengo vinavyosimamia wanafunzi wa uandishi wa habari katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza katika mafunzo hayo mkoani Morogoro Darius Mukiza, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Undishi wa Habari amesema kuwa taarifa nyingi zinazowahusu watoto kwenye vyombo vya habari hazipewi kipaumbele na pia kutokuwepo kwa mwendelezo wa changamoto wanazokumbana nazo.
“Utoaji wa taarifa kwenye vyombo vya habari zinazowahusu watoto bado upo chini pia mwendelezo wa matukio kutokuwepo hizi ni changamoto zinazochangia matukio ya ukatili kwa watoto kuendelea kutokea.
“Pamoja na kwamba zipo habari zinazoripotiwa, mchakato wa habari hizo huacha mambo mengi na wakati mwingine habari hizo zinakosa muendelezo,” amesema Mukiza.
Naye Paulo Mabuga ambaye ni mdau wa masuala ya habari kutoka Mwanza amesema, mwongozo kwa walimu wa waandishi unastahili kuandaliwa kwa ustadi kwa kuwa, ndio huwaandaa waandishi wa kesho.
“Hivi karibuni nilisoma taarifa kutoka kwenye chombo kimoja cha habari, namna walivyoripoti habari ya tukio la mtoto, ilinisikitisha. Mwandishi alishindwa kupanga picha, kutoa maelezo na hata mwisho wa taarifa ile haikuwa na ujumbe wenye athari,’’ amesema Mabuga.
Nassoro Ali, Mkuu wa Kitengo cha Uandishi wa Habari Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro (MUM), amesema kuna haja ya kuwaandaa wanafunzi kuyakabili mazingira ya uandishi wa habari za watoto za uchunguzi.
Diana Msovu kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Idara ya Undishi wa Habari amesema, kuna kila sababu ya kuimarisha uandishi wa habari za wanawake.
“Nchini kwetu bado uandishi wa habari za namna hii upo chini, unapoangalia uwasilishwaji wa taarifa hizi katika nchi nyingine ndio utabaini utofauti.
“Hili linapaswa kuwanza vyuoni kwa wanafunzi, kila habari ina umuhimu wake hivyo zote zinapaswa kuandikwa kwa uzito unaofanana,’’ amesema.
Naye msimamizi wa mafunzo hayo Neville Meena amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa kwa walimu hao kwani wao ndio waandaaji wa waandishi hivyo ni vizuri wakajengewa uwezo wa namna ya kuandika habari zinazoweza kubadilisha taswira kwa watoto na kufundisha.
“Tunafanya hivyo kama mlivyoeleza wenyewe kwamba,taarifa za wanahabari kuhusu habari za watoto zina kasoro nyingi kuanzia uandaaji wa picha, mpangilio na maelezo yanayotolewa,’’ amesema Meena.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF), limeendesha mafunzo hayo ya siku tatu kwa lengo la kuwajengeo uwezo walimu ambao ndio wanasimaia wanafunzi wa waandishi wa habari katika vyuo vyao.