Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Wizara ya Fedha na Wizara ya Maji zimekubaliana kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanashirikiana katika kuweka mazingira wezeshi ya kuwahudumia Wazee nchini.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Viongozi hao Agosti 27, 2022 katika Makazi ya Wazee Misufini yaliyopo mkoani Tanga.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema lengo la Wizara ni kushirikiana Wizara za kisekta ili kuweka mazingira mazuri ya kuwahudumia wazee nchini na kufanya Makazi ya Wazee yaliyochini ya Wizara kuwa na tija ya uzalishaji na kuhudumia Wazee.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju, akizungumza wakati wa ziara ya Manaibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Maji kwenye Makazi ya Wazee Misufini yaliyopo mkoani Tanga.

Ameongeza kutokana na ziara ya Viongozi wa Wizara hizo katika Makazi ya Wazee yanayohudumiwa na Serikali inaonesha umuhimu wa kuwepo na Wizara za kisekta ili kupata hali halisi ya kuona namba bora ya kutatua changamoto zilizopo.

“Sisi kama Wizara tupo tayari kutembea pamoja na Wizara zingine na kuhakikisha Wazee wanapata huduma bora katika Makazi na jamii nzima” alisema Mpanju

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashir Abdalah amesema Wizara hiyo itapeleka Maafisa wake kwenye eneo hilo la Makazi ya Wazee Misufini ili kutathimimi hali ya sasa ya Uwekezaji katika eneo husika kwa manufaa ya Wazee na Ustawi wa Jamii kwa ujumla.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju, akisalimiana na Wazee wanaohudumiwa katika Makazi ya Wazee Misufini yaliyopo mkoani Tanga wakati wa ziara ya Manaibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI,  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na Wizara ya Maji katika Makazi hayo 

“Tutahakikisha jambo lolote linalohusu Uwekezaji Viwanda na Biashara ndani ya maeneo ya Makazi ya Wazee nchini linatekelezwa kwa kasi na kwa matokeo chanya” alisema Dkt. Hashir

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Kaspar Mmuya amefafanua kuwa, suala la huduma kwa Wazee ni mtambuka na linashirikisha Sekta zote hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kusimamia Uratibu wa Sera ambazo zinasimamia Wazee nchini ili kuboresha utoaji huduma kwa wazee.

Awali akitoa taarifa ya Makazi ya Wazee Misufini Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Mwamvita Kilima amesema Makazi hayo yanachangamoto ya mgogoro wa ardhi kwa wananchi kuvamia maeneo ya Makazi hayo, uchakavu wa miundombinu iliyopo hivyo amewaomba viongozi hao kusaidia kutatua changamoto hizo.

Ambapo katika hatua za awali za kutatua changamoto za kuwahudumia Wazee nchini ameiomba Wizara kuongeza watumishi wengine kwenye Makazi ya Wazee hasa ya Misufini ili kuongeza nguvu katika kutoa huduma bora kwa wazee.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Tullo Masanja akitoa taarifa ya Mpango wa Wizara kwenye kuboresha huduma ya Makazi ya Wazee Misufini, amesema Wizara imeaanda andiko la mradi wa ujenzi wa Majengo ikiwemo nyumba tatu za kuhudumia Wazee 60 kwa pamoja na kuboresha miundombinu mengine.

Amefafanua kuwa lengo la Wizara ni kuweka mazingira mazuri ya kuwahudumia Wazee kwa kuhakikisha Makazi ya Wazee yanakuwa na miundombinu mbinu bora na nyenzo zingine kwajili kuwahudumia Wazee.

Nao baadhi ya Wazee wanaohudumiwa ndani ya Makazi ya Wazee Misufini wameishukuru Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha kutoka huduma kwa wazee wasio na ndugu na jamaa wa kuwatunza.

Ziara hiyo imejumuisha pia wadau kutoka WHO, SIDO TASAF na wadau wengine wa maendeleo nchini ikiwa ni muendelezo wa Wizara kutembelea na kufanya tathmini ya kina na kuja na mbinu mbadala ya kuhudumia makazi ya Wazee.