Mkutano wa 8 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8 Summit) umeanza kufanyika leo tarehe 27 Agosti 2022 mjini Tunis, Tunisia. Hii ni mara ya pili kwa mkutano huu kufanyika katika ardhi ya Bara la Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya ule wa Kenya (TICAD 6) uliofanyika mwaka 2016.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu wa Tunisia Mhe. Najla Bouden alipowasili mjini Tunis, Tunisia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anawakilishwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) katika Mkutano huu.

Mkutano wa TICAD 8 utafanyika kwa siku mbili tarehe 27 na 28 Agosti 2022; na umetanguliwa na Kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika nchini Japan, kilichofanyika tarehe 25 Agosti 2022. Pamoja na masuala mengine, Mkutano huu unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.

Agenda 2063 ilikubaliwa na viongozi wa Afrika wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika kwa lengo la kuliunganisha Bara la Afrika katika masuala ya kukuza uchumi; kuhamasisha utawala bora na utawala wa sheria; kuhakikisha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja; kuhakikisha amani na usalama unaimarika na kuiweka Afrika katika nafasi ya mchangiaji mkuu wa uchumi duniani.

Kassim Majaliwa katika mkutano huu anatarajiwa kuwa na mazungumzo ya pembezoni na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Fumio Kishida na watendaji wakuu wa kampuni na taasisi za Japan ikiwemo Shirika la Maendeleo la Japan (JICA); Kampuni ya Mitsubishi; Bodi ya Japan Tobacco Inc (JT Group); na Taasisi ya Japan inayojishughulisha na masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Afrika (Association of African Economy and Development – AFRECO).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea mjini Tunis, nchini Tunisia.

Tangu kuanza kufanyika kwa mikutano ya TICAD, Japan imekuwa ikiongeza kiasi cha fedha za mkopo wa masharti nafuu na msaada katika kuchangia maendeleo ya Afrika kutoka Dola za Marekani bilioni 0.6 kwa mwaka 1993 (TICAD 1) hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 20 kwa mwaka 2019 (TICAD 7). Kwa upande wa Tanzania misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka Japan imesaidia katika utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, afya, nishati ya umeme, kilimo na elimu.

Ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Japan unazingatia mwongozo wa Agenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu inayojikita kwenye kupunguza umasikini na kukuza maendeleo. Japan ni miongoni mwa washirika wakubwa wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania kupitia JICAkuanzia mwaka 1962.

Tanzania ni nchi pekee inayoshirikiana na Japan katika maeneo matatu ya ushirikiano yaliyopewa kipaumbele na nchi hiyo ikiwemo, ushirikiano katika misaada na mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo; ujuzi na uzoefu kupitia program ya wajapani ya kujitolea chini ya Japan Overseas Cooperation Agreement; na fursa za mafunzo na masomo