Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuondosha katika nafasi ya Meneja wa RUWASA Wilaya Kondoa Mhandisi Falaura Suleiman Kikusa kwa kushindwa kumudu majukumu yake kikamilifu.

Waziri Aweso akiwa Wilayani Kondoa amebaini kuwa Meneja huyo wa Maji Vijijini Wilaya amefanya usanifu wa mradi wa Maji wa Kisesa kwa gharama isiyo halisia dalili zinazopelekea matumizi mabaya ya fedha za umma na ubadhirifu.

Gharama ya mradi huo ni zaidi shilingi milioni 900 ambao unahusisha ukarabati wa miundombinu ya maji ikiwa gharama hizi sio halisia.
Waziri Aweso amesema mradi huo katika Kijiji hicho Cha Kisesa umeanza kutekelezwa bila ya kutambulishwa kwa Viongozi na jamii husika jambo ambalo limeleta taharuki na zaidi amepokea taarifa juu ya mchezo uliofanyika ili baadhi ya watu kujipatia fedha za umma isivyo halali.

Katika hatua imebainika uwepo wa miradi mingi ambayo haijakamilika Wilayani Kondoa pamoja na uwepo wa fedha huku wananchi wakiendelea kuteseka na changamoto ya Maji kama alivyobainisha Mhe Mbunge wa Jimbo la Kondoa Dkt. Ashatu Kijaji.

Aidha kumekuwepo na hali isioridhisha ya matumizi ya fedha katika utekelezaji wa Miradi ya Maji Kondoa hatua iliopelekea Waziri Aweso kuagiza wakandarasi wote wanaotekeleza Miradi ya Maji Kondoa kufika Wizarani siku ya Jumatatu Tarehe 29 August 2022 sambamba na Viongozi wa Wilaya na mwisho kuagiza kupitiwa upya kwa Usanifu wa mradi huo kabla ya kuendelea na Ujenzi.