Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tabora
JESHI la Polisi linamshikilia mganga wa kienyeji anayetuhumiwa kuwasha moto kisha kusababisha watoto wanne wa familia moja kufariki huku saba wakilazwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo limetokea usiku wa kuamkia jana mkoani Tabora.
Amesema kuwa moto uliowashwa na mganga huyo wa kienyeji ulikuwa kwa lengo la kuondoa mkosi kwenye familia.
Kamanda amesema kuwa watoto hao waliungua moto wakati wakigombania kutoka nje ya kibanda baada ya moto kuzidi.
Moto huo ulikuwa ukiwaka kuzunguka kibanda walichokuwemo pamoja na watu wengine ndani ya familia.
“Kulikuwa kama watu 20 kwenye kibanda kilichowashwa moto na mganga huyo aliyewapa sharti la kutoka mmoja mmoja baada ya moto kuwashwa na katika kujinuasua kila mmoja ilichangia kushindwa kutoka na kusababisha watoto hao kuungua na kufariki,’ amesema.
Amesema tayari mganga anayetuhumiwa kuhusika katika tukio hilo amekamatwa na upelelezi wake unaendelea.”Ni kweli tuna taarifa ya tukio hilo na upelelezi wa tukio zima tunaendelea nao,” amesema Kamanda Ambwao.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kigwa, Bakari Kabata watoto waliofariki wana umri wa miaka kumi na tano ambao walikuwa ni wa familia moja.
Akielezea tukio amesema mwenyeji mwenye mji huo, alimuita mganga kwa mambo ya kimila, akimtaka kumuondolea mkosi kwenye nyumba yake na mganga huyo kusababisha maafa hayo.
Ameeleza kuwa mama wa familia ni miongoni mwa majeruhi saba ambao wamelezwa Hospitali ya Omulinga na ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora,Kitete.