Kamishina Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Bw. Filippo Grandi yupo nchini tokea tarehe 24 Agosti 2022 kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Serikali na kutembelea Kambi za Wakimbizi mkoani Kigoma.
Bw. Grandi ambaye jana ametembelea Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu ya mkoani Kigoma na baadaye kuwasili mkoani Dodoma na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na huduma bora zinazotolewa kwa Wakimbizi ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita alipofanya ziara kama hiyo mwaka 2019.
Kwenye Kambi ya Nyarugusu, ambayo inahifadhi Wakimbizi zaidi ya 130,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi,Bw. Grandi alijionea hali halisi ya maisha ya wakimbizi hao na kusikiliza maelezo ya wawakilishi wao pamoja na taasisi mbalimbali zinazohudumia wakimbizi.
Baada ya kusikiliza maelezo, Bw Grandi aliahidi kuwa UNHCR itaendelea kushirikiana na wadau ikiwemo Serikali Ili kuboresha maisha ya wakimbizi pamoja na kukabiliana na athari zitokanazo na shughuli za wakimbizi kama vile uharibifu wa mazingira.
Ziara ya Bw. Grandi nchini imekuja kufuatia mazungumzo yake aliyofanya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan jijini New York wakati wa Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2021.