Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), limeshatoa mapendekezo ya awali ya kumsaidia Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ili kumpata mgombea urais atakayekiwakilisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Baraza hilo linaundwa na wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu. Wajumbe wake ni marais wastaafu – Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour, Amani Abeid Karume, John Malecela na Pius Msekwa (Katibu).
Duru za uchunguzi zinathibitisha kuwa tayari wazee hao wameshamdokeza Rais Kikwete na Katibu wa CCM, Abdulrahman Kinana; namna ya kumaliza vema harakati za kumpata mgombea ili chama hicho kiendelee kuwa na mshikamano miongoni mwa wanachama wake.
Busara za wazee zinawataka viongozi wakuu wa CCM watambue kuwa karibu wagombea wote waliokwishajitokeza wana dosari, hivyo si rahisi kuwaengua baadhi na kuwaacha wengine.
Mmoja wa watu mashuhuri waliozungumza na JAMHURI wamethibitisha kuwa wazee wanashauri wagombea waachwe wapambane kwenye upigaji kura ili wale watakaokuwa wameongoza kwenye vikao vya awali, hasa Halmashauri Kuu, majina yao yapelekwe kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa kwa ajili ya uamuzi wa mwisho wa wanachama.
Hoja ya wazee hao ni kwamba Sekretarieti na Kamati ya Maadili, ama zilichelewa, au zilishindwa kuwadhibiti baadhi ya wawania urais ambao walionekana tishio tangu awali.
“Kila mmoja aachwe aogelee, atakayezama, basi amezama. Kama kuwadhibiti, mmeshindwa,” amesema mtoa taarifa wetu ambaye yupo karibu na Baraza hilo la Ushauri la Wazee.
Wazee wanaamini kuwa hata adhabu waliyopewa makada sita na kudumu kwa zaidi ya mwaka mmoja ilichelewa; na kwamba chama kilipaswa walau kuwadhibiti kuanzia mwaka 2010.
Makada sita walioadhibiwa Februari 18, mwaka jana na kuondolewa adhabu mwezi uliopita ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye (mawaziri wakuu wastaafu), na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba; na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja. Wote hao wameshatangaza kuwania urais kupitia CCM.
“Nakwambia Mwenyekiti Kikwete na Kinana vichwa vinawauma. Walichelewa kuwadhibiti, wenzao walianza kujiwekeza tangu huko nyuma. Kwa sasa unamdhibiti nani?” Kimehoji chanzo chetu kilicho karibu na Baraza la Ushauri la Wazee.
Ushauri wa wazee umezingatia historia ya CCM, hasa mwaka 2005 ambako mmoja wa wagombea, Jakaya Kikwete, aliundiwa “zengwe” na Kamati ya Maadili, lakini busara ya Mwenyekiti Mkapa ilisaidia kuumaliza mchuano wa wagombea kwa namna ambayo haikuibua malalamiko ya upendeleo.
Pia, wazee wanazingatia dhoruba iliyoipata CCM mwaka 2010 baada ya kupoteza viti muhimu vya ubunge kutokana na kuwaengua wanachama walioonekana kuungwa mkono na wana-CCM na wananchi wengi. Wanatoa mifano ya majimbo ya Iringa Mjini ambako Chadema kupitia kwa Peter Msigwa walishinda baada ya CCM kumuengua Fredrick Mwakalebela, aliyeshinda kura za maoni na kumweka Monica Mbega.
Maeneo mengi ambako CCM ilipoteza kwa kupuuza maoni ya wana-CCM wengi ni Arusha Mjini, Bukombe na Mbeya Mjini.
Msimamo wa wazee wa CCM unatajwa kuwa chachu ya kauli za hivi karibuni zilizotolewa na Rais Kikwete na Kinana, kwa nyakati tofauti wakisema kwamba hawana wagombea kati ya wote wanaochukua fomu za kuwania urais.
“Mmemsikia Rais Kikwete akisema hana mgombea anayembeba. Unadhani amesema hivyo kwa sababu gani? Amesema kwa sababu wazee wamemwambia hali ya mambo ilivyo ni ngumu. Awaache wenyewe wachuane ili mgombea apatikane kwa wingi wa kura,” kimeongeza chanzo chetu.
Kauli za viongozi hao zinashabihiana na kauli ya aina hiyo inayorejewa mara kwa mara na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Sadifa Hamis Juma, ya kwamba mwaka huu hakuna mgombea atakayekatwa jina kwenye Kamati Kuu (CC). Sadifa, kwa wadhifa wake ni Mjumbe wa CC.
Aidha, wazee wana imani kuwa Mwenyekiti Kikwete atakubaliana na ushauri wao, hasa kutokana na tabia yake inayojulikana ya kutotaka kulaumiwa.
“Mwenyekiti si mtu anayetaka lawama. Utaona hata kubadili Baraza la Mawaziri mara zote amelibadili kutokana na shinikizo, ama la wabunge, au la wananchi. Shinikizo likifika juu kabisa utasikia anasema ‘unaona wabunge au wananchi hawakutaki, kwa hiyo naomba tu tuheshimu misimamo yao’. Hataki kuonekana amemkwaza mtu, na kwa sababu hiyo haitashangaza kuona majina yote yakipelekwa Halmashauri Kuu na hapo majina matatu au matano ya juu yakapelekwa Mkutano Mkuu kwa kura za mwisho,” kimesema chanzo chetu.
Rais Kikwete aliyekuwa ziarani Ulaya hivi karibuni, alizungumza na jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi na kuwahakikishia kuwa hana mgombea wake “mfukoni” anayetaka kumwachia madaraka.
Akasema wingi wa wana-CCM wanaojitokeza kuwania urais ni matokeo ya kukua kwa demokrasia ndani ya chama hicho.
“Lakini niwahakikishie acheni waumane, lakini mimi binafsi sina chaguo langu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa chama ndicho kitakachoamua; na kwamba kuna hakika ya kumpata mgombea sahihi kwa saizi na hadhi ya chama hicho.
Hata hivyo, alikiri kuwa wapo wagombea wanaojipitisha kwake wakiomba kuungwa mkono, lakini pamoja na hayo, tayari amewajibu kuwa hana mgombea aliyemweka kwapani.
Naye Kinana anasema hana mgombea, lakini anasisitiza kuwa chama kipo makini kumpata mgombea makini atakayeshinda.
Amewatoa hofu wana-CCM na wananchi kwa jumla juu ya harakati za kuwania urais ndani ya CCM, akisema wamejipanga kuendesha uchaguzi kisayansi, kwa umakini mkubwa, na kutovunja imani ya wanachama.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, wagombea nafasi ya urais kupitia CCM walikuwa 33 baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda naye kutangaza na kuchukua fomu.
Wengine ni Makamba, Ngeleja, Sumaye, Lowassa, Membe, Wasira; mkazi wa Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo; na mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Eldefonce Bilohe.
Pia wamo makachero, Dk. Hassy Kitine na Balozi Agustino Mahiga; Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Dk. Mwele Malecela; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, Balozi Amina Salum Ali; na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wengine ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Dk. Mzamini Kalokola (kutoka Tanga); Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe; Balozi Ali Karume; Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya; mtumishi wa CCM Idara ya Siasa na Uhusiano, Amos Siyantemi; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Wakili mwandamizi Mahakama Kuu Tanzania, Godwin Mwapango; Peter Nyalile, na Leonce Mulenda.
Wengine ni Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani; Makongoro Nyerere, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Amos Robert; na Monica Mbega.
Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka wiki hii. Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Julai 2, mwaka huu saa 10 jioni.
Julai 8 kitafanyika kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili. Julai 9 ni siku ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa; Julai 10 kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa. Mkutano Mkuu wa Taifa ni Julai 11 hadi 12.
Mkutano Mkuu ndiyo utakaochagua jina la mwanachama mmoja atakayekiwakilisha chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu utakaoshirikisha vyama vingine vya siasa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepanga Oktoba 26, mwaka huu, kuwa Siku ya Uchaguzi Mkuu.