Mwandishi wa Gazeti la JAMHURI, Manyerere Jackton, katika makala yake iliyokuwa na kichwa cha habari, ‘Kutokufanya kitu nako ni kufanya kitu’, toleo Na. 190 aliandika hivi, ‘Ukiyatafakari mengi yanayolikabili Taifa letu, hata kama ulikuwa na nia ya kugombea urais, unaweza kughairi.’
Kwanza niseme kabisa kwamba maneno haya ya Manyerere si ya kuwakatisha tamaa wanaowania nafasi ya urais. Ni angalizo kwa rais ajaye. Ni tafakuri kwa rais ajaye. Ikumbukwe kwamba Manyerere ni mwandishi, pia ni mtafiti wa masuala mbalimbali, kwa ujuzi wake na uchambuzi wake ametambua Taifa linavyotafunwa na wachache wanaojiita wakuu wa nchi na ndiyo maana akayaandika haya maneno kwa huzuni.
Rais ajaye lazima atafakari atakapoanzia na kumalizia, maana nchi imetafunwa yamebaki makapi tu. Migodini ni mashimo tu. Kwenye mbuga zetu za wanyama – fisi, sungura, swala, nyani ndiyo wengi, wale wanyama wa kuliingiza Taifa pato kubwa ni wa kuhesabu. Wametoroshwa na viongozi wetu, wengi wao wakiwa wazima.
Taifa kama Taifa tumepoteza dira ya kujitegemea kiuamuzi na kimkakati. Tumefika mahala pa kuamini kwamba maendeleo yanaletwa kwa kaulimbiu zinazobadilikabadilika kila siku. Kwa uhalisia ulioasisiwa na chama tawala ni kwamba ukweli unapotoshwa kwa sababu binafsi na kwa manufaa binafsi.
Hali hii inajidhihirisha kupitia matumizi mabaya ya madaraka, mikataba mibovu, kupindishwa kwa sheria na kufumbia macho uhalifu unaofanywa kichinichini kwa manufaa ya viongozi wa chama tawala.
Nimepembua, nimetafakari, nimejihoji na kuhojiwa, nimetafiti hatimaye nimebaini kwamba kunahitajika uamuzi mgumu na wa pekee ili Taifa letu liweze kusonga mbele kiuchumi, kielimu, kifikra na kiuzalendo. Uamuzi huu ni kukiondoa chama tawala madarakani, hiyo ndiyo njia pekee iliyosalia na iliyo ya muhimu zaidi.
Hakuna ubishi kwamba Taifa sasa ni la watu wachache. Ni Taifa la viongozi wa Serikali ya CCM na wawekezaji. Hii ni hatari. Hizi ni dalili mbaya kwa Taifa. Kwa sasa hakuna kukubali Taifa kuwa la mabilionea wachache wa chama tawala. Serikali ya CCM sasa hivi inaongozwa na fedha, haiongozwi na fikra wala utu wa kibinadamu.
Chama tawala katika uongozi wake kimeliweka Taifa hili njiapanda, kila mtu anajua hilo, iwe ni Mtanzania, Mhindi, Mzungu wanafahamu kwamba Tanzania haina mwelekeo wala viashiria vya kuwa na maendeleo. Tanzania inahitaji msaada, na msaada wa manufaa ni kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani.
Oktoba ni kuindoa CCM kwani katika uongozi wake imewatesa Watanzania. Imehujumu rasilimali za Watanzania, imewagawa Watanzania katika makundi ya aliyenacho na asiyenacho. Imepoteza mwelekeo wa Watanzania katika elimu, uchumi na uzalendo. Ndani ya chama tawala hakuna kiongozi mwenye uchungu na rasilimali za Taifa hili. Wote kauli yao ni ya chuma ulete, chuma ushibe na familia yako.
Tanzania ya leo kila mtu anayepewa dhamana ya kusimamia rasilimali za Taifa anatumia mwanya huo kujitajirisha yeye na familia yake. Na anafanya hivyo akitambua kwamba ni makosa, lakini inambidi kwa sababu mfumo wote wa uongozi ni wa kifisadi.
Wakati umewadia sasa Watanzania kuwa na sauti moja, kauli moja, mwelekeo mmoja ili kulinusuru Taifa kutoka kwa makaburu hawa wa Kitanzania. Taifa linahitaji mabadiliko katika nyanja zote zinazomhusu binadamu. Kuna matatizo ya msingi ndani ya Taifa. Uchumi unaendeshwa vibaya sana hadi kufikia kuwa Taifa ombaomba.
Hakuna chakula cha kutosha kwa bei inayowafaa wananchi wake. Huduma za afya ziko katika hali mbaya, kwa kuwa hospitali hazina dawa za kutosha. Mfumo wa elimu hauna weledi wa viwango wa kumkomboa Mtanzania. Viongozi wanajifurahisha kwa kufanya ufujaji wa rasilimali za umma. Haya ni matatizo ambayo si ya kufumbia macho wala kuyanyamazia.
Si vyema kupuuza kutatua matatizo haya ifikapo Oktoba, mwaka huu. Umaskini wa kipato na kifikra bado umetufunga hata hatuwezi kufurukuta. Wananchi wengi hawana makazi bora ya kuishi na familia zao. Chama tawala na viongozi wake wamepoteza mwelekeo wa kuliongoza Taifa hili. Wanatapatapa tu.
Nchi imeoza kwa sababu ya uongozi dhaifu wa chama tawala. Nchi imegawanyika vipande vipande kwa sababu ya uongozi dhaifu wa chama tawala. Watanzania wamegawanywa na kweli wamegawanyika. Nchi iko gizani kwa upande wa maendeleo. Kumbe uongo ndani ya chama tawala ni sifa mojawapo ya kuwa kiongozi.
Ufisadi ndani ya chama tawala ni kigezo cha kugombea urais. Mikataba feki ni mojawapo ya ilani ya chama tawala. Ikulu kwa upande wa chama tawala ni sehemu ya kuhamishia familia. Sera za chama tawala zimeshindwa kulikwamua Taifa hili kutoka kwenye sifa ya kuombaomba. Mwenyezi Mungu amelijaalia Taifa la Tanzania rasilimali lukuki.
Hebu tuangalie. Kanda ya Ziwa imejaa dhahabu, almasi, nikeli. Kanda ya Magharibi imejaa shaba, mafuta na madini ya fedha. Kanda ya Kati ina madini ya urani yanayotumika kutengeneza mabomu ya nyuklia. Kanda ya Pwani imejaa gesi na mafuta. Kanda ya Kusini imejaa makaa ya mawe.
Pamoja na utajiri wote huu bado Watanzania ni maskini wa kupindukia. Hakika hii ni aibu. Kila kanda kuna utajiri mkubwa na wa aina yake. Lakini pia kila kanda wamejaa Watanzania ambao ni maskini waliojikatia tamaa ya kuishi katika nchi yao.
Eti wanakuja watu ambao hawana hata nguo za kubadili, wanapata leseni ya kuchimba dhahabu katika migodi, wanakuwa matajiri kwa kutumia miliki ya rasilimali za Watanzania, lakini wenyewe wanabaki mafukara. Swali la kujiuliza ni; nani anafikiri badala ya Serikali ya CCM?
Serikali ya CCM imetengeneza mataifa mawili ndani ya Taifa moja. Tofauti kubwa sana za kiuchumi zinazidi kupanua utengano wa kimatabaka kati ya wenye nguvu za kiuchumi na wasio na kitu. Wenye nguvu za kiuchumi wanamiliki uchumi, siasa, mashamba, majumba ya kifahari n.k. Kuna taifa la watu matajiri na kuna taifa la watu maskini; mataifa yote haya yako ndani ya Taifa moja la Tanzania.
Kuna taifa la wanaosikilizwa na kuna taifa la wasiosikilizwa. Kuna taifa la wenye haki na wasio na haki. Mtoto wa maskini hakutani na mtoto wa mwenye uwezo. Mtoto wa maskini shule anayosoma haina maktaba ya vitabu, haina madirisha, vyoo ni vya kuchangia na walimu wao, pengine wengine wanajisaidia vichakani. Loh! hii ni aibu.
Serikali ya CCM imekaribisha ufukara katika Taifa hili. Serikali ya CCM imesababisha Taifa hili kuwa na ombaomba wengi. Vijana kwa wazee wanazurura mitaani wakitafuta ajira, huo ni ujumbe tuujibu Oktoba.
Kambi za wazee wasiojiweza maisha wanayoishi hayatamaniki, ukitembelea utashuhudia hali za wazee kukosa sabuni za kuogea, mahala wanapolala ni pachafu, chakula kwao ni cha shida wakati mwingine wanalala bila hata kunywa uji. Je, hayo ndiyo ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ kama tulivyoahidiwa na Serikali ya CCM?
Tutafakari. Tuamue kupiga hatua. Tupinge ukatili wa Serikali ya CCM, ama kwenye ‘Delete CCM October’-CCM ifutwe Oktoba.
Kweli Serikali ya CCM ni ya kuogopa kama ugonjwa wa ebola. Hakuna ubishi tukisema kwamba mchawi wa Tanzania ni Serikali ya CCM. Dalali wa mali za Watanzania ni sehemu ya watumishi wa Serikali ya CCM. Mwizi wa mali za Watanzania ni sehemu ya makada wa CCM. Kama unabisha soma ripoti ya kila mwaka ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Maisha ni mapokezano, kuna wanaofariki dunia, na kuna wanaozaliwa. CCM ipumzike, kuleni pensheni zenu, mlivyochuma vimewatosha sasa. Baba wa kiroho, Sai Baba, alipata kunena maneno haya yenye busara, tuyatafakari.
Maisha ni wimbo, uimbe,
Maisha ni mchezo, ucheze,
Maisha ni changamoto, ikabili,
Maisha ni ndoto, ielewe,
Maisha ni sadaka, itoe,
Maisha ni upendo, ufaidi,
Maisha ni lengo, lifikie,
Maisha ni kengele, igonge,
Maisha ni barabara, ipite,
Maisha ni mti, upande.
Sasa tushawishike kusema, ‘CCM ni chama tukiondoe Oktoba’.
Mwanafizikia wa Kijerumani, Albert Einstein [1879-1955] alipata kusema, ‘Hatuwezi kutatua matatizo kwa kutumia namna ileile ya kufikiri tuliyotumia katika kuyaanzisha matatizo.’
Serikali ya CCM ndiyo waanzilishi wa rushwa katika Taifa hili. Serikali ya CCM ndiyo waanzilishi wa uongozi dhaifu katika Taifa hili. Serikali ya CCM ndiyo walioanzisha matatizo na balaa katika Taifa hili. Serikali ya CCM kwa wao ni vigumu kubuni sera madhubuti ya kuwabana viongozi wanaokiuka miiko ya kiuongozi.
Ni vigumu mtu kutunga sheria anayofahamu kwamba inambana katika vipengele fulani fulani. Ushahidi wa hoja hii umeonekana waziwazi wakati wa kujadili Rasimu ya Katiba mpya. Mawazo yalikinzana kwa sababu wenye maslahi binafsi walikuwa wengi, walitumia kila mbinu kulinda ubinafsi.
Ndani ya Serikali ya CCM kuna viongozi waliobobea katika rushwa. Ndani ya Serikali ya CCM kuna viongozi ambao ni wafanyabiashara haramu. Wewe unafikiri ni nani anatorosha wanyamapori wetu? Ni nani anatorosha madini yetu? Kama siyo baadhi ya viongozi wa chama tawala?
Ndani ya Serikali ya CCM kuna madalali na mafundi wa kusaini mikataba hewa, hivyo kwa wao kutunga sheria ambayo inawabana hilo Watanzania wenzangu tulisahau.
Watanzania lazima tufahamu kwamba adui wa Tanzania yupo Tanzania. Nyoka yumo tayari chumbani tusiulizane ana urefu gani au nani aliacha mlango wazi nyoka huyo akaingia ndani. La msingi tuchukue mashoka na marungu ili tumbamize kichwa huyu nyoka.
Jeffrey Gitomer alipata kuandika hivi, ‘Vipingamizi haviwezi kukusimamisha. Matatizo hayawezi kukusimamisha. Watu walio wengi hawawezi kukusimamisha. Wewe peke yako unaweza kujisimamisha’.
Mwaka huu tusikubali kusimamishwa na Serikali ya CCM. Mwaka huu tusikubali kusimamishwa na makada wa CCM. Mwaka huu tusikubali kusimamishwa kwa Sh. 5,000. Tusikubali kusimamishwa kwa kilo moja ya sukari. Tusikubali kusimamishwa kwa fulana iliyoandikwa kwa maneno hewa.
Watanzania tujifariji kwa maneno haya ili mioyo yetu itulie wakati tunajiandaa kufanya uamuzi sahihi ifikapo Oktoba mwaka huu. Ukiwa maskini bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa kijana bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa mzee bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa tajiri bado wewe ni mtoto wa Mungu.
Ndiyo, ukiwa machinga bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa mfupi bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa mrefu bado wewe ni wa Mungu. Ukiwa yatima bado wewe ni Mungu. Ukiwa mgonjwa bado wewe ni mtoto wa Mungu. Mtoto wa Mungu ana uamuzi.
Tuamue vyema Oktoba. Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena. Tunataka iwe hivyo na ieleweke hivyo mbinguni na duniani, Ulaya na Amerika, Asia na Afrika yote. Tusiote kufanya makosa, hivyo Oktoba usifanye makosa kuichagua tena Serikali ya CCM kurudi madarakani.
Kijana mmoja alikuwa akisafiri kwa usafiri wa basi. Wakati wa safari yake kijana huyu alikuwa anafoka na kuwatukana watu hovyo. Mwisho wa safari yake wakati anashuka, abiria mmoja akamwambia; “Kijana umeacha kiatu”. Kijana akauliza kwa ukali, “Nimeacha nini?” Abiria akamwambia, “Umeacha jina chafu’’.
Hapana shaka kwamba hata katika maisha yetu ya kawaida tunayoishi kuna watu walio na sifa kama za huyu kijana. Lakini Serikali ya CCM ni zaidi. Serikali ya CCM itaondoka madarakani ikiwa imetuachia makovu ndani ya mioyo yetu na nje ya mioyo yetu.
Ipo methali ya Kichina inayosema hivi, ‘Maua ya kesho yako kwenye mbegu za leo’. Kesho ya Tanzania haiwezi kuongelewa bila leo. Tunachopanda leo ndicho tutakachovuna kesho.
Leo ni msingi wa kesho. Leo tukipanda ufisadi tusitarajie kesho kuvuna uadilifu, tutavuna tu ufisadi huo ndiyo ukweli. Watanzania tuwe tayari, jana ya Taifa hili imeharibiwa na Serikali ya CCM, jana ya Taifa hili imejaa rushwa. Ni jukumu letu kuitengeneza leo yetu vizuri kwa kuwachagua viongozi wenye uzalendo na Taifa hili.
Miaka mingi iliyopita aliishi mtawala na mbunifu maarufu wa mbinu za kivita aliyeitwa Hannibal (183-247) aliyepata kusema hivi, “Lazima tuone njia kama haipo tuitengeneze.” Watanzania, Tanzania kuna njia au kichaka? Tafakari mwenyewe. Njia ya Serikali ya CCM ni ufisadi. Njia ya Serikali ya CCM ni matumizi mabaya ya dola. Njia ya Serikali ya CCM ni rushwa.
Aliyepata kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Paulo wa VI [1963-1978], alipata kuandika maneno yafuatayo: “Ukitaka amani, ifanyie kazi haki”.
Tanzania ya leo haki ya wastaafu iko wapi? Tanzania ya leo haki ya walimu iko wapi? Tanzania ya leo haki kwa vyama vya upinzani iko wapi? Tanzania ya leo haki ya maskini iko wapi? Tanzania ya leo haki ya walemavu wa ngozi iko wapi? Tanzania ya leo haki ya wazee iko wapi? Tanzania ya leo haki ya vyombo vya habari iko wapi?
0783 994403/0757 852377