Waziri wa Nishati,January Makamba, amekabidhiwa Uwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Mradi wa Umeme wa Rusumo wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji unaoshirikisha nchi tatu za Burundi, Rwanda na Tanzania.
Waziri Makamba amekabidhiwa jukumu hilo wakati wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Mradi wa Umeme wa Rusumo na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda Dkt.Ernest Nsabimana katika eneo la Mradi Rusumo, Wilayani Ngara, Mkoani Kagera.
Mradi huo utazalisha Megawati themanini (80MW) ambapo kila nchi itapata 27MW.
Akizungumzia kuhusu jukumu jipya la Uwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Burundi, Rwanda na Tanzania katika Mradi wa Umeme wa Rusumo, Waziri Makamba amesema, Mradi wa Rusumo una miundo yake ya Uendeshaji ambapo kuna Baraza la Mawaziri, Bodi ya Kampuni na kamati ya Uendeshaji (Sterling Committee) ambapo kila chombo kina kazi yake katika Mradi huo.
Amesema,kazi ya Baraza la Mawaziri, ni kutoa miongozo ya ki-sera kufuatilia, kusimamia, kusukuma, na kuwezesha utekelezaji wa Mradi.
Waziri Makamba ameeleza kuwa,baraza hilo hukaa mara moja kwa mwaka na huomba taarifa ya Maendeleo ya Mradi na kuelekeza kuharakisha utekelezaji wa Mradi pamoja na kutoa maelekezo mahususi kwa ajili ya ufanisi wa Mradi na vyombo vyote vinaripoti kwenye Baraza la Mawaziri.
Amesema, Baraza hilo ni chombo muhimu sana katika uendeshaji wa Mradi huo na kasi ambayo imepatikana hivi sasa katika utekelezaji wa Mradi, kwa sehemu kubwa imetokana na Uongozi wa Baraza hilo la Mawaziri ambalo linatoa mchango mkubwa sana katika utekelezaji wa Mradi.
Waziri Makamba amesema, nchi hizo hupokezana Uwenyekiti ambapo kabla ya Rwanda nchi Mwenyekiti wa Baraza hilo ilikuwa ni Burundi, na sasa ni Tanzania.
Ameeleza kuwa, jukumu lake la Uwenyekiti katika Baraza hilo la Mawaziri, litakuwa ni kuongoza vikao na kuitisha vikao na kuwa na Mawasiliano ya moja kwa moja na Bodi kuhusu mambo ya kiutendaji ya kila siku yanayohitaji miongozo ya Mawaziri kabla , wakati na baada ya vikao pale inapohitajika.
Akizungumzia kuhusu Mradi wa Umeme wa Rusumo, Waziri Makamba amesema Mradi huo una umuhimu mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi zote tatu za Burundi Rwanda na Tanzania.
Ameuelezea Mradi huo kuwa, ni ndoto ya viongozi waasisi wa nchi zote tatu kwa muda mrefu tangu miaka ya sitini ambapo, hatimaye ndoto hiyo inakaribia kukamilika.
Waziri Makamba amesema, Mradi huo utaongeza umeme unaohitajika sana na wa bei nafuu katika nchi tatu hodhi za Mradi huo wa umeme wa Rusumo kutokana na mahitaji makubwa ya umeme na utakuwa ni chachu ya maendeleo kwa nchi hizo zinazoendelea.
Waziri huyo wa Nishati, ameongeza kuwa, Mradi huo unaashiria ushirikiano wa nchi hizo tatu zinazopakana na kuwa huo ni msingi wa maendeleo na unaashiria utashi wa nchi hizo tatu kutumia rasilimali asili zilizopo ikiwemo mito kuleta maendeleo ya watu wake.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa Mradi wa Umeme wa Rusumo na utabadilisha sana taswira ya uchumi hasa wa eneo hilo.
Waziri Makamba amesema, kwa upande wa Tanzania, maeneo makubwa yanayozalisha umeme ni upande wa kusini mashariki mwa Tanzania katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Dar-es-salaam ambapo kuna mitambo mingi ya kuzalisha umeme.
Ameeleza kuwa, umbali wa kusafirisha umeme kutoka maeneo ya uzalishaji hadi upande wa Magharibi mwa nchi kuna umbali mkubwa sana, hivyo uwepo wa uzalishaji umeme katika eneo la Rusumo utaongeza upatikanaji wa umeme katika Gridi ya Taifa na maeneo yaliyopo karibu na eneo la Mradi yatapata umeme wa uhakika bila kuusafirisha kutoka umbali mrefu.
Waziri Makamba amewaambia Watanzania kuwa, wategemee kunufaika na Mradi wa Umeme wa Rusumo ndani ya Kipindi cha miezi 6 kuanzia sasa na mradi huo unategemewa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu ambapo Mtambo wa kwanza utaanza kujaribiwa kuwashwa na umeme unatarajiwa kuanza kupatikana katika robo ya kwanza ya mwaka 2023 umeme utakapoanza kusambazwa na kuingia