LowassaaMbunge wa Monduli na Waziri Mkuu (mstaafu) Edward Lowassa, ameanza rasmi ‘Safari ya Matumaini’ baada ya kutangaza nia ya kugombea urais mwishoni mwa wiki na kuainisha nguzo za mafanikio.
Katika mkutano wa kutangaza nia uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa, Lowassa amejikita kwenye hoja na ajenda za msingi zinazolenga kuiondoa Tanzania katika lindi la umaskini.
Anaamini elimu ni nguzo ya msingi kwa yeyote anayetaka kupambana na umaskini na akasisitiza kuwa anauchukia umaskini na haoni sababu ya Watanzania kuendelea kuwa maskini.


“Nimeamua kugombea urais ili kupambana na umaskini.  Ninapata hasira ninapoona umaskini ambao ungeweza kuepukwa kutokana na raslimali nyingi tulizonazo. Kinachohitajika hapa ni uongozi imara wa kutokomeza umaskini,” amesema Lowassa.
Ukiacha umasikini, Lowassa alizungumza kwa msisitizo na uchungu mkubwa juu ya elimu: “Napenda kusisitiza kuwa, elimu ndiyo muhimili wa maendeleo, ndiyo mkombozi wa kweli wa binadamu.
“Mimi ni mfano hai wa ukombozi wa elimu. Elimu ndiyo imenivusha kutoka kijijini kwetu Ngarash na kunipa upeo wa kitaifa.


 “Mama akiwa na elimu atatambua umuhimu wa kumpeleka mwanae shule, anapata lishe bora na chanjo stahili na kuwa anaishi katika mazingira safi. Mkulima akipata elimu stahiki, atakuwa mkulima bora na kilimo chake kitampa tija na kumletea maendeleo. Elimu ndio silaha dhidi ya umaskini, maradhi na ujinga.”
Huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliofika uwanjani hapo, Lowassa aliainisha ramani ya maendeleo ya kweli inayoiwezesha Tanzania kuondokana na umaskini na kuanza kutoa misaada kwa nchi nyingine, huku akisema ni aibu Tanzania kuendelea kutegemea misaada.
Ametaja mambo yaliyomsukuma kugomeba urais kuwa ni pamoja na vuguvugu la kisiasa lililopo hapa nchini, ambapo wananchi wameanza kuelekeza siasa katika mapambano binafsi badala ya kushindanisha sera jambo ambalo halina afya kwa taifa hili.
Suala jingine anasema ni nia yake kuendeleza Muungano na mshikamano miongoni mwa Watanzania mambo yatakayoendeleza utulivu na amani ambao ni mtaji msingi kwa maendeleo ya nchi yoyote.


Amezitaja hofu walizonazo wananchi kuwa ni pamoja na vijana kuendelea kukosa ajira, Watanzania kupata wasiwasi iwapo watanufaika na rasilimali ya gesi iliyopatikana na maisha kuzidi kuwa magumu, kisha akasema: “Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto hizi na kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake anaishi akiwa na uhakika wa usalama wa maisha yake, mali zake na mahitaji yake muhimu.
“Papo hapo akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake, na kesho yake itakuwa bora zaidi kuliko leo yake. Kwa maneno mengine, Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi imara, unaoweza kuwaongoza kujenga taifa imara. Hii ndio Safari ya Matumaini.”
 
Uamuzi mgumu
Lowassa ametaja sifa anazopaswa kuwa nazo Rais wa kuiongoza Tanzania kuanzia Oktoba, mwaka huu, kwa kusema: “Kwa maoni yangu, ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo: Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya maamuzi magumu; Uongozi thabiti, makini na usioyumba; Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa; Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa; na Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
“Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo: Aweze kuwaunganisha Watanzania; Aweze kubuni sera na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza pato la Mtanzania; ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato kati ya aliyekuwanacho na wasiokuwanacho; Aweze kubuni sera na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;


“Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika; Aweze kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali; Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara; Aweze kusimamia matumizi ya raslimali zetu ili kuutokomeza umaskini wa Waatanzania na; Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo.”
 
Lowassa na uamuzi mgumu
Lowassa anafahamika kwa kuwa kiongozi mwenye kufanya uamuzi mgumu. Akiwa Waziri wa Maji na Mifugo, alivunja mkataba na kampuni ya City Water ya Uingereza iliyokuwa imekuja nchini kutoa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na ikashindwa kutimiza makubaliano. Kampuni hiyo ilikwenda mahakamani ikashindwa.
Si hilo tu, uwezo wa Lowassa kufanya uamuzi ulithibitika mwaka 1994 wakati akiwa Waziri wa Ardhi, alipoagiza wananchi kuvunja uzio katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam uliokuwa umejengwa na mfanyabiashara maafuru kwa jina la Baghdad.
Mwaka 2004 akiwa nchini Misri alifanya uamuzi mgumu kwa kuwambia Wamisri, tena akiwa katika ardhi yao jijini Cairo, kuwa kama wanataka kupigana vita na Tanzania kwa kuwa Tanzania ilikuwa inachukua maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga na Kahama, basi Tanzania iko tayari kwa vita. Aliwaeleza pia kuwa Tanzania haijawahi kuwa koloni la Uingereza kama unavyotamka mkataba huo kwani Uingereza walikuwa waangalizi wa Tanzania chini ya Umoja wa Mataifa (UN). Wamisri walinywea baada ya kauli hiyo, wakaishia kuahidi misaada.


Akiwa Waziri Mkuu, ndani ya miaka miwili ya mwanzo alifanya uamuzi mgumu kwa kusimamia Ujenzi wa shule za Sekondari za Kata. Shule hizi zimesaidia vijana wengi wa Tanzania hadi sasa karibu kila familia ina tatizo kubwa la kupata mfanyakazi wa ndani kwani karibu wanafunzi wote wanajiunga na shule za Kata baada ya kuhitimu shule ya msingi.
Ameahidi kumaliza foleni katika Jiji la Dar es Salaam baada ya miezi 12 akichaguliwa kuwa Rais. Hili alipata kulifanya akiwa Waziri Mkuu, kwani mwaka 2007 aliagiza matumizi ya njia tatu jijini humo kupunguza foleni. Kwa sasa barabara za Kilwa, Barack Obama na Banana-Kitunda, zimeanza kutumia njia tatu walizokuwa wanabeza watu na utaratibu huu unapunguza foleni kwa kasi kubwa.


Wapo watu wenye kupendekeza kuwa hata barabara za Morogoro, Nyerere, Kawawa na Ali Hassan Mwinyi zikitumia utaratibu huu wa njia tatu alizopendekeza Lowassa foleni zitapungua kwa kiasi kikubwa jijini Dar es Salaam.
Lipo jingine, ambalo wapinzani wa Lowassa kisiasa hawataki kulitaja, nalo ni hatua yake ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu Februari 7, mwaka 2008. Huo ulikuwa moja ya uamuzi mgumu. Kashfa ya Richmond, ambayo ameitaja mwezi uliopita kuwa ilisukwa kisiasa na wanasiasa, alivyoikabili nalo ni uamuzi mgumu. Kwa wanasiasa wenye uchu wa madaraka angeweza kulumbana na Rais Jakaya Kikwete na kuyumbisha nchi, ila kwa unyenyekevu mkubwa akaamua kuubeba msalaba huo binafsi.


Wapo wanaohoji kwa nini imemchukua miaka saba kueleza umma kuwa hakuhusika katika kashfa ya Richmond, lakini wanasahau kuwa mwaka 2012 Lowassa alimhoji Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete katika kikao cha NEC kuwa katika suala la Richmond ni lipi alilofanya bila baraka au maelekezo yake, na hadi leo Kikwete hajawahi kujibu swali hilo.
Katika kinachoitwa kashfa ya Richmond, taarifa zinazoweza kushangaza wengi na kuwapa tabu kuziamini ni kwamba kwa uhalisia Richmond haikupata kulipwa hata senti tano kutoka serikalini, ingawa ripoti ya Dk. Harrison Mwakyembe iliulaghai umma wa Watanzania kuwa kila siku kampuni hii ilikuwa inalipwa Sh milioni 150.


Kwa upande mwingine, Dk. Mwakyembe aliyesema bungeni wakati anawasilisha ripoti mwaka 2008 kuwa kama angesema yote Serikali ingeanguka, hivi karibuni amenukuliwa kwenye mitandao ya kijamii akisema ikibidi atasema hata ambayo aliyaacha kwenye ripoti baada ya Lowassa kusema hahusiki.
Kisheria, kwa kauli hii ya Mwakyembe ilibidi afunguliwe uchunguzi unaojitegemea ikiwa aliacha baadhi ya masuala ya msingi katika riporti aliyoitoa ambayo sasa anataka kuyasema. Ikiwa hivyo ndivyo, ni wazi alilidanganya Bunge kwa kulipa taarifa isiyo sahihi, suala ambalo ni jinai.
Lowassa juzi wakati anatangaza nia, alieleza jinsi alivyofanya uamuzi mgumu kwa kushiriki vita ya Kagera, tena mstari wa mbele. “Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni mwa askari wa mstari wa mbele wa mapambano… sijui wengine kama walifika Kagera,” anasisitiza.
Huku akishangiliwa na kusisitiza kuwa kazi ya kuongozi nchi si lelema, inahitaji mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi, amesema hata kabla ya kushawishiwa mtu anapaswa kuwa na wazo la kuutaka urais, kisha akawaeleza wananchi akiungwa mkono ataendeshaje nchi, hali inayoweza kuleta mabadiliko ya kweli badala ya kusubiri kushawishiwa.
 
Mchakamchaka wa uchumi
 Lowassa akasisitiza mambo ya msingi kwa maendeleo ya Tanzania ikiwamo ujenzi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, aliposema anataka kupambana na rushwa kwa vitendo na si maneno, uchumi kuwafikia watu walioko vijijini, kuondokana na kuwa taifa ombaomba na kuweleza katika elimu.
Kwa hamasa ya kipekee, Lowassa amesema anaanzisha mchakamchaka wa kuondoa umasikini Tanzania. Katikati ya hotuba yake, aliingiza maneno: “Mchakamchaka… mchakamchaka… mchakamchaka…” huku umati wa watu waliohudhuria ukiitikia chinja… Lowassa aliongeza kuwa anaanzisha fikra mpya.
“[Nitaanza] Kujenga fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua azma ya kujitegemea kama Taifa. Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza kujitegemea na kuijenga Tanzania sisi wenyewe. Kujiamini na kujitegemea ndio uhuru wa kweli.”


Lowaasa alitaja mambo 12 anayotaraji kufanya ikiwa atateuliwa na CCM, kisha kuchaguliwa kuwa Rais, na msisitizo wake ukawa kwenye umoja, mshikamano, elimu, ajira, kuondoa umasikini, kupambana na rushwa, kuondoa tofauti ya kipato na akasema akichaguliwa kuwa Rais ndani ya miezi 12 ya kwanza foleni na msongamano wa magari vitakuwa historia katika Jiji la Dar es Salaam na majiji ya Arusha, Mwanza na Mbeya.
Ameahidi kushirikiana na sekta binafsi, kuboresha masilahi ya walimu na watumishi wengine wa umma, bila kusahau mazingira bora kwa mama ntilie, bodaboda na wamachinga aliosema ni marafiki zake wa dhati.
Kwa upande wa michezo, amesema: “Tumechoka kuwa kichwa cha mwendawazimu. Tumeendelea kuwa washiriki washindwa, na hili halikubaliki,” amesema Lowassa na kuahidi kulipatia ufumbuzi ikiwa atapata fursa ya kuliongoza taifa la Tanzania.


Kauli yake ya mwisho, ambayo ukimwangalia hata usoni unaona anamaanisha asemacho, Lowassa alisema: “Nauchukia umasikini, tuanze pamoja mchakato wa maendeleo.” Huku hotuba yake ikikatizwa mara kwa mara na kelele la “Rais, Rais, Rais… rudia, rudia, rudia,” Lowassa aliyedhihirisha kuwa mwenye siha njema, alikuwa akikunja uso anapozungumzia matatizo ya Watanzania, na kuonyesha kuwa ana nia ya dhati ya kuiingiza nchi katika mchakamchaka wa kufuta umaskini kama alivyoahidi uwanjani hapo. Lowassa hakuwasema wapinzani wake zaidi ya kuwaomba wamuunge mkono. Kwa undani zaidi soma hotuba yake kuanzia Uk. 13.
 
Kingunge anena
 Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, alisema mkutano wa Lowassa Jumamosi iliyopita, umemkumbusha mikutano ya TANU enzi za wapigania uhuru na walipompokea Mwalimu Julius Nyerere akirejea kutoka Umoja wa Mataifa.
Kingunge alisema Lowassa mchakato aliouanzisha Arusha, unamaanisha hatima ya CCM na Tanzania inaanzia hapo. Alisema wapo wana-CCM wanaotangaza nia, lakini kwa kuwa suala la urais ni la wananchi, basi ni bora wananchi wakaachwa waseme.
 
Ampongeza Kikwete
 Alipongeza kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mjini Dodoma juzi kuwa chama kinapaswa kuchagua mtu anayekubalika ndani na nje ya chama kwa kusema kuwa huo ni msimamo sahihi wa chama uliodumu tangu enzi za Nyerere.
Kingunge amesema urais ni mzigo mzito unaopaswa kubebwa na Mnyamwezi na akiangalia ndani ya CCM, “Mnyamwezi ni Lowassa.” Alisema chama kimekuwa na utamaduni wa kulea makada wake, ambapo kiliwalea Kikwete, Lowassa na Abdulrahman Kinana, waliopitia hadi jeshini kuijua nchi na akiangalia ndani ya CCM kwa sasa hakuna kama Lowassa.


Kwa upande wake, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alisema Oktoba, mwaka huu si mwaka wa kufanya majaribio katika suala la uchaguzi mkuu. Alisema Lowassa anatosha na hivyo hakuna mwingine anayepaswa kupewa fursa hiyo isipokuwa Lowassa.
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alipagawisha baada ya kutoa hotuba yenye mvuto uwanjani hapo na kuwambia maelfu ya watu waliokuwapo kuwa Lowassa ndiye chaguo sahihi na kasema “asiyemtaka Lowassa na ale malimao.”
Pamoja na wabunge zaidi ya 50, pia walihudhuria wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) wapatao 185.
Wingi wa watu na hamasa iliyokuwapo uwanjani hasa baada ya Lowassa kueleza mpango wa kujenga viwanda, kuwezesha wazawa na kuanzisha mchakamchaka wa maendeleo kufuta umaskini, vinaacha mwangwi mkubwa kuwa huenda Lowassa anajua nchi inakopaswa kuelekea kuliko mtu yeyote kwa sasa katika Tanzania.