Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea tabia ya udhalilishaji inayodaiwa kufanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana katika halmashauri mbalimbali ikiwemo ya Sikonge.
Akizungumza jana wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Uhai wa chama mkoani Tabora, amesema chama hakiungi mkono udhalilishaji wowote na inafuatilia hatua kwa hatua jambo hilo.
“Nataka niseme na hili la udhalilishaji wanawake kingono, nimelikuta Kaliua na lipo Sikonge, lakini hata kwenye maeneo mengine kwa watumishi wa umma, ujumbe umefika, wenye hiyo tabia waache, waache kuwadhalilisha dada zetu, waache kuwadhalilisha mama zetu, waache kuwadhalilisha ndugu zetu wa kike hapa Sikonge, hiyo tabia imeshamiri kwa sababu tu kuna mtu anadhamana, ana fursa ya kuwasaidia wengine.
“Hamuwasaidii mama zetu, hamsaidii dada zetu mpaka muwadhalilishe kingono,chama kinafuatilia kwa karibu sana, hatutaruhusu udhalilishaji wa aina yoyote kwa wanawake ndani ya nchi hii, wanawake hawa wanauwezo mkubwa sana katika kufungua fursa za maendeleo katika taifa letu.
“Wakithubutu akina mama wanaweza, hatuwezi kuacha uthubutu wao kwa sababu tu sisi akina baba baadhi yetu tunashindwa kuzuia hisia zetu, tena sio kushindwa kuzuia hisia zetu ila hatuna adabu tu, ni utovu wa adabu tuliokuwa nao,” amesema Shaka.