Rais Jakaya KikweteChama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) kimeunda timu maalum itakayokwenda bungeni Dodoma, kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa Sheria wa Vyombo vya Habari baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali, ulitakiwa kuwasilishwa katika kikao kilichopita kwa hati ya dharura, jambo ambalo halikuwezekana, baada ya kupingwa na wadau na baadhi ya wabunge.


Hata hivyo, muswada huo uliorejeshwa kwa wadau kujadiliwa, unatarajiwa kupelekwa kwa mara nyingine katika Kikao cha Bajeti kinachoendelea ingawa si kawaida kwa Bunge la Bajeti kujadili miswada ya sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam wiki iliyopita,  Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi, anasema baada ya kuusoma, wamegundua kuna kasoro nyingi na miongoni mwa kasoro hizo ni kukosa tarehe rasmi ya kuanza kwa sheria hiyo ikisainiwa. Ni mtego huo.
Pia kama Rais Jakaya Kikwete atasaini muswada huo na kuwa na sheria, adhabu kwa wanataaluma wa Watanzania wenye mapenzi na nchi yao, ambayo wazazi wengine wanategemea riziki kupitia ajira hii ya kuandika habari kama wanataaluma, adhabu kwa wakosaji katika uandishi zitawafanya wabadili mawazo na kutafuta kazi nyingine.


Anasema wadau wa habari na wataalamu wa sekta hiyo wataendelea kuwaelewesha wabunge juu ya masuala mbalimbali yaliyomo katika muswada huo, ili hata wanapoupitia wawe na uelewa wa kutosha wa kitu wanachotaka kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Licha ya kasoro hizo, pia kuna hila za kuupitisha kwa haraka kusudi wasitoe mawazo yao juu ya vipengele kadhaa ambavyo vinaminya uhuru wa vyombo vya habari na hata uhuru wa wananchi kupata habari.


 Tunasema muswada huu ukipita, utakuwa ni sheria mbovu ambayo haina manufaa kwa nchi yetu, pia Watanzania watakosa habari za uhakika kwani ikiwa kila ufikapo muda wa taarifa ya habari saa 2.00 usiku wote wanalazimika kutazama Televisheni ya Taifa, ni kutafuta kuwarudisha wananchi katika zama za ujima.
Kupitisha muswada huu wa hovyo ni nia ya Serikali hii kutafuta mbinu chafu za kuwatisha wananchi na kupingana wazi wazi na sera zake za uwazi na ukweli.
Hapa tunachojiuliza; kama muswada huo wa hovyo unaokiuka haki za binadamu na kutafuta kuviua vyombo vya habari kama utapitishwa hata kwa mabavu na wabunge walio wengi wa CCM, je, mapato ya matangazo yatakayoambatana na habari za TBC kwa muda huo yatagawanywa kwa vituo hivyo vya binafsi?


Tunasema huu muswada huu haufai kwa sasa hasa ukizingatiwa kuwa viongozi wanatakiwa kufikiria kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la ufukara kwa muda mrefu ama kwa visasi vyao vya kitoto wanatafuta kila njia kuona amani na utulivu wa Watanzania unatoweka kasi.
Tunaiomba Serikali hii ya awamu ya nne itumie busara kuundoa muswada huu ili kudumisha na kuheshimu haki za binadamu badala ya kuwa sehemu ya kuleta machafuko nchini kwa kuendesha tawala za mabavu.