TIMU ya Wanawake ya Simba Queens ambayo ni sehemu ya Wekundu wa Msimbazi ya jijini Dar es Salaam imetinga Nusu Fainali ya Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Ni kutokana na ushindi wa mabao 2-0 iliyopata timu hiyo dhidi ya SHE Corporates kutoka nchini Uganda.

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamanzi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Licha ya mchezo huo kuonekana kuwa mgumu kutokana na timu zote kushambuliana kwa zamu, Simba Queens walionekana kuwa bora zaidi kwa mabingwa hao wa Uganda.

Vivian Corazone alitupatia bao la kwanza dakika ya 21 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Joelle Bukuru.

Kipindi cha pili Simba Queens walirudi kwa kasi ambapo Pambani Kuzoya alitupatia bao la pili dakika ya 61 na kuwahakikishia ushindi.

Katika mchezo wa kwanza wa kundi B walipata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Garde Publicaine ya Djibouti hivyo ushindi huu unatufanya kutinga hatua inayofuata.

Kocha Sebastian Nkoma aliwatoa Philomena Abakah, Asha Djafar, Diana William na Vivian Corazone na kuwaingiza Olaiya Barakat, Aisha Juma, Silvia Mwacha na Sarrive Badiambila.