Bunge linanuka rushwa. Baadhi ya wabunge wanapokea rushwa ili kutetea maslahi ya wanaowatuma. Lakini wapo wabunge jasiri walioamua kupambana na wenzao wala rushwa kama inavyothibitishwa na Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, ilikuwa moto. Akitambua kuwa kuna wabunge waliohongwa kuvuruga utendaji kazi ndani ya Wizara hiyo na Tanesco, Mnyika akipasua jipu kwa kuwasema wazi wabunge waliohongwa. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo, neno kwa neno…
Kashfa ya ununuzi wa mafuta ya kufua umeme
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulitahadharisha kwamba mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kufua umeme, usitumike kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha “Richmond nyigine”.
Inaelekea kansa hii ndani ya Serikali inayoongozwa na CCM ya kuachia dharura ziendelee kwa manufaa ya wachache, imesambaa kwa kiwango cha kuwa vigumu kutibika isipokuwa kwa mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala.
Katika siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wazabuni ambao wamekosa zabuni ya kuiuzia Tanesco mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL, kutokana na uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kuipatia zabuni kampuni ya PUMA Energy (Tz) Ltd. (zamani ikiitwa BP (Tanzania) Ltd) ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 50.
Licha ya malalamiko ya wazabuni hao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa imefanywa na inaendelea kufanywa ndani na nje ya Bunge hili tukufu, ili uamuzi huu wa
Katibu Mkuu Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya makampuni hayo na wapambe wake wa ndani na nje ya Bunge lako tukufu.
Aidha, wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu Mkuu Maswi ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, tarehe 10 Juni 2011, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, alimwandikia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) – iliyokuwa inasimamia ufilisi wa IPTL – kumtaka aendeshe mitambo ya IPTL ili kufua MW 100 za umeme ili kuweza kuondoa mgawo wa umeme uliokuwa unaendelea sehemu mbalimbali nchini.
Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba mara baada ya kupata barua hiyo, tarehe 24 Juni 2011, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) akimwomba mwongozo na ushauri juu ya utaratibu wa manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa dharura.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alitoa mwongozo kwa RITA kwa barua yake ya tarehe 28 June, 2011 alipoielekeza RITA itumie mamlaka yake chini ya kanuni ya 42 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma zinazohusu bidhaa, kazi na huduma zisizokuwa na ushauri elekezi na mauzo ya mali za umma kwa tenda, Gazeti la Serikali Na. 97 la mwaka 2005 (Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of Public Assets by Tender) Regulations, Government Notice No. 97 of 2005).
Kanuni hiyo inamruhusu Afisa Masuhuli kuamua namna ya kufanya manunuzi kwa dharura, bila kujali mipaka ya mamlaka yake endapo kwa kufanya hivyo kutahakikisha uchumi na ufanisi wa manunuzi hayo na endapo ataona ni kwa manufaa ya umma kwamba bidhaa au kazi zenye thamani inayozidi mamlaka yake zinunuliwe kama suala la dharura.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupata mwongozo huo wa PPRA, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia Katibu Mkuu Maswi barua ya tarehe 18 Julai 2011 kumweleza kwamba katika makampuni matano yaliyoonyesha nia ya kuiuzia IPTL tani 500 za mafuta kwa siku zilizokuwa zinahitajika kuendeshea mitambo yake kwa mwezi Julai, 2011, kampuni za OilCom na Shell hazikuwa na akiba ya mafuta wakati Kampuni ya Mogas ilikuwa na lita laki tatu tu.
Kwa upande mwingine, Kampuni ya Oryx ilikuwa na tani 6,000 lakini ilikuwa inauza mafuta hayo kwa dola za Marekani 1,069.30 au shilingi 1,668,456.02 kwa tani. Aidha, kampuni ya BP (sasa Puma Energy) ilikuwa na tani 9,000 na ilikuwa tayari kuuza mafuta hayo kwa dola za Marekani 901.02 au shilingi 1,405,864.77 kwa tani.
Kwa kuzingatia maelezo hayo, Katibu Mkuu Maswi alitoa ridhaa kwa RITA kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa kampuni ya BP kwa bei iliyotajwa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yalikuwa na bei ndogo ikilinganishwa na bei ya Oryx, tarehe 27 Septemba 2011 Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco alisaini mkataba wa kununua mafuta kutoka Oryx kwa bei ya dola za Marekani 926.98 au shilingi 1,501,707.60 kwa tani.
Aidha, wiki moja kabla ya hapo, yaani tarehe 21 Septemba, Mkurugenzi Mtendaji huyo alikwishasaini mkataba mwingine na kampuni ya Camel Oil kwa bei ya dola za Marekani 905.24 au shilingi 1,466,488.80 kwa tani.
Kama inavyoonekana, mikataba yote miwili ilikuwa na gharama kubwa zaidi kwa tani kuliko bei ya BP. Hata hivyo, mkataba wa BP ulikatishwa na Tanesco ikaanza kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa makampuni ya Oryx na Camel Oil.
Mheshimiwa Spika, kitu cha ajabu ni kwamba licha ya mikataba ya makampuni ya Oryx na Camel Oil kuonyesha bei za shilingi 1,501.70. na shilingi 1,466.49 kwa lita, Tanesco ilianza kununua mafuta ya makampuni hayo kwa shilingi 1,850 kwa lita! Kwa maana hiyo, kwa mikataba ya kununua jumla ya lita 16,110,000 kwa mwezi kutoka kwenye makampuni hayo, Tanesco ilikuwa inayalipa makampuni hayo jumla ya shilingi 29,803,500,000 kwa mwezi.
Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa na BP kwa mkataba na RITA yaliigharimu Serikali shilingi bilioni 13,140,000,000 kwa bei ya shilingi 1,460 kwa lita.
Hii ndiyo kusema kwamba kama Tanesco ingeendeleza mkataba na BP badala ya kuuvunja, gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ingekuwa shilingi 23,520,600,000 na hivyo Tanesco ingeliokolea Taifa shilingi 6,282,900,000 kila mwezi!
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine kumekuwa na taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kwamba Mkurugenzi Mtendaji Mhando hakutendewa haki aliposimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi juu ya utendaji kazi wake.
Nyingi ya taarifa hizo zimetolewa bila kuwa na faida ya kuangalia nyaraka zinazohoji uadilifu na uaminifu wa Mkurugenzi Mtendaji Mhando.
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi Mkuu Mhando ni mkurugenzi na mwanahisa wa kampuni binafsi inayoitwa Santa Clara Supplies Co. Ltd. ya Dar es Salaam.
Wakurugenzi wengine ni mke wake, Eva Martin William, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji, na watoto wao. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, mnamo tarehe 20 Desemba 2011, Santa Clara Supplies iliingia mkataba na Tanesco ambapo Santa Clara Supplies ilikubaliwa kuwa mgavi wa vifaa vya ofisini vya Tanesco kwa gharama ya shilingi 884,550,000.
Mkataba huu ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando kwa niaba ya Tanesco na mkewe, Eva Martin William kwa niaba ya Santa Clara Supplies. Aidha, barua ya Tanesco iliyoitaarifu Santa Clara Supplies kwamba imepatiwa zabuni hiyo iliyoandikwa tarehe 24 Novemba, 2011 ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza kwamba “… kiongozi wa umma hatajiweka katika hali ambayo maslahi yake binafsi yatagongana na wajibu wake kama kiongozi wa umma.”
Aidha, “… kuhusiana na uwazi kwa wananchi, viongozi wa umma watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi na umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.”
Vile vile, “… kuhusiana na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu wao kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma.”
Zaidi ya hayo, “… kuhusiana na maslahi binafsi, viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya.”
Mwisho, “… kuhusiana na maslahi ya umma, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, viongozi wa umma watapanga masuala yao kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma.”
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushahidi huu wa maandishi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mbunge yeyote wa chama chochote cha siasa chenye uwakilishi ndani ya Bunge lako Tukufu, anayefuata imani yoyote ya dini aseme kama, kwa mujibu wa vifungu hivi vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkurugenzi Mtendaji Mhando ana sifa za kuitwa kiongozi mwadilifu wa umma.
Hivyo, pamoja na uchunguzi wa kawaida unaoendelea, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka aamuru hatua za uchunguzi wa kijinai zichukuliwe dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Spika; hata hivyo hatua hizo dhidi ya Mkurugenzi wa Tanesco na watendaji waliohusika zisigeuzwe kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa Serikali kwa ujumla wake, kwa kuwa taarifa za utendaji wa Tanesco kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika, zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na hata vikao vya Baraza la Mawaziri.
Hivyo, ili ukweli wa kina uweze kujulikana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa Bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme.
Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme.
Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu “… kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….”.