Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amemtaka mkandarasi anayejenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kuhakikisha anakamilika kwa wakati na kwa ubora.

Ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma, alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho ambacho kinatekelezwa na Kampuni ya kikandarasi ya Sinohydro Corporation kwa kushirikiana na M/s Beijing Sino – Aero Construction Engineering na M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation.

Mhandisi Mkazi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato, Ayele Yirgo, akielezea mchoro wa taswira ya Kiwanja cha Ndege cha Msalato kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, mara baada ya kukagua mradi huo Jijini Dodoma.

“Niwasisitize wale waliopata fursa ya kusimamia ujenzi wa Kiwanja cha Ndege hichi ikwemo Mhandisi Mshauri, TANROADS na TAA lazima tuhakikishe kwamba mkandarasi anajenga kwa viwango vinavyotakiwa na ikiwezekana hadi kufikia mwezi Juni 2025 mradi uwe umekamilika”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameahidi kuwa atautembelea mradi huo mara kwa mara ili kuona hatua mbalimbali za utekelezaji kuanzia mwanzo hadi mwishoni mwa utekelezaji wake lengo ni kuona kuwa mkandarasi anafanya kazi kulingana na yale waliokubaliana kwenye mkataba.

Aidha, Profesa Mbarawa amefafanua kuwa kiwanja hicho kinajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, Apron, Tax way na kufunga taa na kwa awamu ya pili ujenzi wa jengo la abiria na miundombinu mingine.

Waziri Mbarawa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ili kuleta maendeleo kwa Taifa kwa ujumla.

Amewataka wananchi kumpa ushirikiano wakandarasi hao ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo unaisha kwa haraka na kuweza kuleta tija kwa jamii na Taifa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kushoto), akiangalia taswira ya muonekano wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake mwezi Juni, 2025.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Mhandisi Leonard Chimagu, amesema kuwa kwa sasa mkandarasi anaendelea na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

Naye, Mkazi wa Msalato, Juma Aheri, amesema kuwa wanatarajia kupata ajira nyingi katika mradi huo pia mradi ukikamilika eneo hilo litaendelea kiuchumi kwani biashara pamoja na hoteli zitajengwa kwa wingi.

Ujenzi wa Kiwanja hicho chenye urefu wa kilometa 3.6 unatarajiwa kukamilika mwezi June, 2025 na utagharimu takribani shilingi Bilioni 165