Kuna ule msemo wa “vita ya panzi, furaha ya kunguru”.

Vyama vya siasa vya upinzani, kama kweli vina dhamira ya dhati ya kupata uhalali kutoka kwa Watanzania, mwaka huu wa 2015 ni mwaka sahihi kabisa wa kutimiza azma hiyo.
Endapo vyama hivyo, kupitia umoja wao wa Ukawa vitashindwa kutumia fursa hii, basi huenda Watanzania wakaendelea kushuhudia miaka mingine mingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kutamba.
Wana CCM walishawasaidia wapinzani kujiimarisha. Kuna kata na majimbo mengi yaliyotwaliwa na wapinzani kwa msaada au baraka zilizotokana na mparaganyiko ndani ya CCM.


Harakati zinazoendelea sasa ndani ya chama hicho za kuwapata wagombea, hasa kwenye nafasi ya urais, zinatosha kabisa kuwa chanzo cha mavuno kwa wapinzani.
Hatudhani, na kwa kweli hatutarajii, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kuwaona wana CCM wakiendelea kuwa wamoja.
Mnyukano unaoendelea miongoni mwa wana CCM wenyewe unatosha kabisa kuwa fursa na faraja kwa wapinzani kupenyea hapo hapo.


Sioni mwana CCM anayeutaka urais, ubunge, udiwani au hata ujumbe wa Baraza la Wawakilishi anayehangaishwa na Ukawa!
Vita inayoendelea ni ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM. Uchaguzi wa mwaka 2005 ulikuwa na makovu, lakini nadhani wa mwaka huu utavunja rekodi.
Ukisoma magazeti, ukisikiliza redio na televisheni, au ukipita kwenye mitandano ya kijamii unawaona CCM wanavyonyukana. Sioni ni kitu gani kinaweza kuwaweka pamoja Edward Lowassa na Paulo Makonda. Sioni ni muujiza gani unaoweza kuwasahaulisha uhasama wao watu kama Dk. Harrison Mwakyembe dhidi ya Lowassa; au mwana CCM kama Bernard Membe na Hussein Bashe.


Ni jambo la kawaida kabisa kwa watu wanaotoka chama kimoja cha siasa kutofautiana wakati kama huu wa Uchaguzi Mkuu. Mara zote tofauti za waungwana huwa za kimsimamo na hata kiuwezo. Ndani ya CCM si hivyo. Tofauti zao ni za mtu na mtu-chuki kwa chuki.
Kinachoendelea ni kana kwamba wakishampata mgombea urais, basi mambo yote yatakuwa yameishia hapo! Ni kama hawatalazimika kumnadi ili apambane na wapinzani.
Napata shida sana kuamini kuwa endapo Lowassa atapitishwa na chama chake kuwania urais, mtu kama Stephen Wasira atasimama jukwaani kumpigia debe.


Sioni ni kwa namna gani mwana CCM kama Lowassa anaweza kusimama jukwaani kumnadi Dk. Mwakyembe, au kinyume chake.
Ingawa tulizoea kuona uadui wa wanasiasa ni wa muda, kuna dalili zote kwamba uadui huu wanaojengeana wenyewe kwa wenyewe hauwezi kukoma.
Juzi mjini Arusha Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru aliwaasa wana CCM kufanya maridhiano (reconciliation) baada ya harakati zao za kuingia Ikulu kufikia tamati. Sioni kama hilo litafanywa. Hata likifanywa, itakuwa ni kukenua meno tu lakini mioyoni hakuna msamaha.


Wana CCM wananyuka kweli kweli. Wamekamiana mno. Wanachofanya ni kama wameshajua hakuna uchaguzi mwingine huko tuendako. Au pengine unaweza kudhani wameshajua CCM haiwezi kudumu katika madaraka kwa hiyo ni kama vile ‘wanagawana mbao’.
Kwenye uchaguzi mara nyingi wagombea huviziana kwenye udhaifu. Huutumia udhaifu kama fimbo ya kunyukana. Anayelemewa, hushindwa. Huridhia kushindwa kwa kutambua kuwa kama ni udhaifu wake uliosababisha akashindwa, ulikuwa udhaifu wa kweli; na si wa kutungwa.
Hapa kwetu tunaweza kuaminishana kuwa fulani ni fisadi, na watu wakaamini hivyo. Tunaweza kusema fulani ni mzee, kwa hiyo watu wakaaminishwa kwa uzee wake hawezi kuwa kiongozi bora. Lakini wapo wanaouaminisha umma kuwa vijana hawana uzoefu wa kuongoza. Wamejawa tamaa za ujana kwa hiyo si watu wa kufaa kupewa madaraka makubwa. Ghiliba hizo zimetumika kuwanyima vijana nafasi za uongozi.


Hakuna anayeweza kuibuka na hoja za kisayansi za kuwaaminisha watu kuwa fulani ni mwizi, na wizi wake ni huu na ule. Hakuna mwenye uthibitisho wa kina au wa kisayansi kuwa vijana si wa kupewa madaraka makubwa; au uzee ni umbumbu wa kumfanya alionao asifae kuwa kiongozi.
Haya yanaendelea. Yanawatafuna. Wana CCM wenyewe wameuaminisha umma kwamba miongoni mwa wanaoutaka urais, kuna wagonjwa. Wanaosema hivyo, ukiwauliza ni lini wagombea walipanga foleni kupima afya na hatimaye kuubaini ugonjwa, wanakuwa hawana majibu zaidi ya kusema, “Kwani wewe huoni kwa macho?” Tunahukumu kwa kutumia macho. Kumaliza utata wa fitna za aina hii, wapo walioomba wagombea wote wapimwe afya zao. Sidhani kama hilo litawezekana. Kama litawezekana, basi tujiandae kushuhudia mengi mwaka huu.


Mwito wangu kwa wapinzani wa CCM ni kuhakikisha wanautumia mwanya huu kujiimarisha. Hii ni fursa nzuri mno kwao. Wanachopaswa kufanya ni kujiandaa kwa staili ya kunguru kula kwa sababu tayari panzi wanagombana!
Huu ndio wakati mzuri kwao kupata siri zote muhimu kutoka ndani ya CCM. Ni wakati wa kuwavuta wana CCM wasioona umuhimu wa kuendelea kuwa wafuasi wa CCM. Kwa kufanya hivyo wanaweza kusaidia kutimia kwa kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kwamba “upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM.”


Lakini tunapouangalia udhaifu na hatari hii, tunapaswa kujua chanzo chake. Wapo wanaoamini kuwa haya mambo ya mitandao yaliyoanza mwaka 1995 na kushamiri mwaka 2005 ndio chanzo cha haya ya sasa. Hakika, hawapo mbali na ukweli.
CCM ilianza kuporomoka zaidi mwaka 2005 wakati mgombea wake, Jakaya Kikwete, akihaha huku na kule kuingia madarakani.
Eti leo kuna Watanzania wanashangaa matumizi ya fedha kwa wagombea! Mbona hawakushangaa mwaka 2005? Kama mwaka huo fedha zilitumika, na aliyezitumia yupo, leo atakuwa na ujasiri gani wa kuwazuia wengine wanaoutaka urais kuzitumia?


Je, kama mwaka huo Watanzania hawakuelezwa zilikotoka hizo fedha, leo Mwenyekiti wa CCM atakuwa na nguvu ipi ya kuwataka wagombea kueleza walikotoa mabilioni waliyonayo? Je, ana moral authority?” Hana. Ndio maana hata ule mpango wa kujivua gamba ulishindikana. Rushwa inakemewa majukwaani ili kuwahadaa wananchi. Katibu Mkuu wa CCM pekee hawezi maana kapewa kazi wakati chama kikiwa kimeshaumizwa mno.
Wasiokumbuka ni vema tukawakumbusha. Timu ya Ndugu Kikwete haikutumia mfumo halisi wa CCM kuhakikisha inaingia madarakani. Kila kitu kilihamishwa kutoka Mtaa wa Lumumba, na kupelekwa ofisi binafsi Mtaa wa Mindu. Kwenye ofisi hizo ndipo walipokuwa wana CCM kama Stephen Wasira, Ludovick Mwananzila, Henry Shekifu na wengine wengi.


Mwaka 2010 utaratibu huo ulipungua nguvu kutokana na desturi ya CCM ya kutotaka rais aliye madarakani ‘asumbuliwe’ na mwanachama mwingine kuwania nafasi hiyo. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza, tukashuhudia urais ukigeuzwa kuwa si shughuli ya chama tena, bali ya kifamilia. Tukamuona mtoto wa mgombea urais akikabidhiwa kazi ya kuongoza harakati zote za kumwezesha baba yake kurejea madarakani. Makada wakawekwa kando. Ofisi ya kifamilia ikaipiku ofisi ya taasisi kubwa- CCM.
Makada walipohoji, baba akatetea uamuzi wake na wa familia yake. Akasema kilichokuwa kikifanywa na mwanae kilikuwa halali kwa vile hilo jambo lilikuwa la binafsi! Fikiria, wenye chama wanawekwa kando. Kazi walizopaswa kuzifanya za kusaka wadhamini na mambo mengine zinafanywa na familia, halafu ndoto za hao na wengine eti ni kuona CCM inaendelea kuwa kitu kimoja! Haiwezekani. Hata kupungua kwa kura za mgombea wa CCM mwaka 2010 moja ya sababu zake kuu ni hii maana makada kadhaa walisema ‘familia yenyewe ihangaike’.


Mara nyingi mtu kama kiongozi wa chama kikubwa aina ya CCM anapofanya jambo, hata kama si la kiungwana, ni wachache wanaopata uthubutu wa kumhoji. Baba alipotetea uamuzi huo pale Dodoma, si kwamba wana CCM wote walikubaliana naye. Kimya chao kilitokana, ama na woga, au unafiki. Hawakutaka kumuudhi bwana mkubwa.
Matokeo yake mitandao ikazidi kuongezeka. U-sisi ukawa umepata msingi. U-familia likawa jambo lisiloepukika tena. Hiki tunachokishuhudia leo ni matokeo ya ‘ubunifu’ uliofanywa na Mwenyekiti wa CCM mwaka 2005 na 2010.
Ndio maana wenye kumbukumbu za mambo haya wanajua Mwenyekiti huyu huyu hawezi kuwa na ujasiri wa kuwazuia wenzake kutumia fomula aliyoitumia yeye kuyapata madaraka.


Anajua urais wa sasa si suala la chama kama taasisi, bali ni la mgombea, ndugu, jamaa na wapambe wake. Matokeo ya aina hii mpya ya kusaka madaraka ndio haya ya wagombea wa chama kimoja kusimama hadharani na kwenye vyombo vya habari kuvuana nguo.
Hatuhitaji mtaalam wa kututhibitishia kuwa CCM si wamoja tena. Mtu anaweza kuuliza, kama si wamoja, kwa nini wanaendelea kuwa kwenye genge hilo moja linaloitwa CCM? Jibu ni rahisi. Nalo ni kwamba wapo pamoja kimaslahi tu kwa sababu wengi wanaamini nje ya CCM hakuna maisha. Wanaona heri waendelee kuwa wanafiki ndani ya CCM ili maisha yao yaendelee kuwanyookea. Siasa za Tanzania ni za maslahi zaidi.


Uthibitisho wa haya unaweza kupatikana kutoka kwenye mchezo wa kisiasa alioushiriki Fredy Mpendazoe. Alishirikiana na wenzake (wakubwa kabisa) kuasisi chama cha CCJ. Akapewa matumaini makubwa. Akalewa njozi hata akaamua kuuachia ubunge na mafao yake yote. Akawa tayari kusafisha njia akiamini wenzake wangemfuata! Wakamtosa. Amekwama kisiasa. Haitashangaza siku moja akionekana akiwa kwenye jukwaa la CCM akikabidhiwa kadi na kuvikwa jezi za chama hicho.
Leo wapo wanaowashangilia kina Membe, Lowassa, Wasira, Dk. Magufuli, Pinda, Profesa Mwandosya na wengine wengi wanaoutaka urais. Wapo wanaodiriki kuwahadaa kwa kusema, “Hata ukiamua kuhamia upinzani, tuko tayari kuhama na wewe.” Siamini kama hilo litatokea.
Sijaona wapinzani wakijiandaa kufaidi mavuno haya. Wanaweza kusema hawataki ‘makapi’, lakini ukweli ni kwamba kusubiri watoto wakue au kuendelea kuomba wapinzani wazaliwe, kutachukua muda mrefu. Mpango wa muda mfupi wa sasa ni kuhakikisha wanatumia mwanya huu wa mkanyagano ndani ya CCM kujijenga.


Aliyewapa wapinzani fursa hii murua ni Mwenyekiti wa CCM ambaye fomula yake ya kuyapata madaraka imekiumiza chama hicho. Imeibua makundi. Imesababisha utovu wa nidhamu kiasi kwamba wenyewe kwa wenyewe sasa hawaheshimiani na hawapendani tena.
Haya makovu na maumivu wanayosababishiana sasa hayawezi kuwaondoka wakati wa kupambana na wapinzani majukwaani utakapowadia. Kwa maneno mengine, wapinzani wakijipanga vilivyo mwaka huu wanaweza kuvuna viti vingi.
Waliosoma kitabu cha Mzee Chinua Achebe cha Things Fall Apart, wanaona yaliyomo humo ndiyo yanayoendelea CCM. Anguko la CCM ni matokeo ya Mwenyekiti wake maana wanaoutaka uongozi wanatumia fomula aliyoibuni na ambayo ilimpa alichokitaka. Simuoni wa kuibatilisha fomula hii. Wana CCM kuwa wamoja ni majaliwa. Wapinzani wa CCM Mungu awape nini?