Najuta kuzaliwa maskini na katika familia ya ukulima, ningelipenda nizaliwe katika familia ya uanasiasa au ufanyabiashara, na kuwa na nafasi ya kuweza  kuwa na maisha bora kama ilivyo kwa familia hizo nyingi pasi na familia zetu za wakulima.
Napenda kuwa  tajiri, tajiri wa mali na si moyo, tajiri wa kujilimbikizia mimi lakini si wao, tajiri wa kurithi na kurithisha lakini si wa kufilisika. Napenda niwe mkwasi wa mali hata kumfikia nusu muumba wa dunia na nchi hii.
Sitapenda kuridhika na nilichonacho kamwe, kwa kuwa kufanya hivyo nakaribisha ufukara katika familia yangu ambayo nataka iwe bora, nitajitahidi kila uzao wangu uwe na kipaji cha biashara au siasa, lengo kuu likiwa ni mafanikio.


Nimewaza haya kwa sababu naona kuwa sasa hivi siasa ndiyo kazi pekee ambayo inaweza ikawa inalipa kuliko kazi nyingine yoyote katika nchi yetu.
Ni siasa tu ambayo inaweza kumkomboa Mtanzania yule ambaye aliaminishwa kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo, ni Mtanzania huyu huyu aliyekuwa na mawazo ya usawa na haki kwa kila Mtanzania ndani ya nchi yetu ya Ujamaa na Kujitegemea.
Siasa ni mfumo wa utawala, hivyo siasa inaweza ikaakisi ukweli wa mfumo wa utawala katika nchi yoyote duniani. Iwapo mfumo wa siasa una kila dalili ya takrima ni vigumu kukemea na kuzuia takrima tukufu katika uendeshaji wa mfumo wa nchi.


Tanzania ni moja kati ya mataifa machache sana ambayo yalibahatika kupata uhuru wake chini ya viongozi waadilifu ambao hawakuwa na tamaa ya ukwasi na kujilimbikizia mali. Mfano mzuri ni Julius Nyerere ambaye aliliongoza Taifa hili kwa miaka zaidi ya ishirini na hakuweza kuwa na mali inayoshikika au kuhamishika.
Julius na wenzake baadhi ambao walikuwa na malengo mwanana kwa taifa hili wameishia kuwa historia katika machapisho kadhaa na siyo katika umiliki wa mali kama walivyo viongozi wengi wa mataifa ya Afrika yaliyopata uhuru sanjari na Tanzania.
Hili ni jambo tunalopaswa kujivunia kama Watanzania na tulipaswa kulienzi kama siyo kulitumia katika vigezo vyetu vya uongozi katika Taifa hili.


Nakumbuka wakati wa Azimio la Arusha tulikubaliana kuwa uongozi na fedha haviwezi kukaa pamoja, kwa dhana hiyo basi wafanyabiashara hawakupaswa kuwa viongozi ndani ya chama chetu, chama ambacho kinatoa mustakbali wa mfumo wa uongozi wa kukataa takrima.
Sasa hivi tunaelekea katika uchaguzi wa viongozi wengine watakaotutawala kwa miaka mingine mitano. Viongozi hawa wengi wao wanataka kugombea tena nafasi zao walizokuwa wanazishikilia kwa miaka yote iliyopita, huku wakijua wazi kuwa katika kipindi cha uongozi wao ahadi nyingi hawajazitekeleza kwa wananchi wao.
Njia pekee watakayotumia ni kuomba kula yao iwe ya uhakika kwa kipindi kingine, na ili wale ni lazima wapate kura yetu sisi wakulima na wafanyakazi ambao tayari tumekwisha tawaliwa kwa kiasi cha kutosha kuthibitisha kuwa maisha bado ni yale yale na ahadi zile zile ila zinaboreshwa kisiasa ili waweze kuibuka kidedea.


Ni kipindi hiki ambacho labda wanasiasa wakweli ndipo watapakwa matope na wanasiasa uchwara, wanasiasa wakweli watabambikiziwa tuhuma za kufoji ili waonekane wachafu na kibaya zaidi mipasho isiyo na tija kwetu wakulima na wafanyakazi tuliokata tamaa ya maisha tutaisikia.
Mipasho hii itatuumiza sana kwa kuwa yote itahusisha ufisadi wa mali yetu ya nchi huku sisi tukiwa maskini wa kutupwa na kuaminishwa kuwa waombaji wa nafasi hizo ni bora zaidi kuliko hao wanaotaka kulikomboa Taifa hili.
Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, viongozi wengi watatumia fimbo ya fedha ya kuturahisishia maisha kwa mwezi mmoja na kisha wao watapata kujirahisishia kula ya uhakika miaka mitano ijayo baada ya kupata kura zetu.


Kwa ufupi, taaluma ya siasa ni nzuri kwa kuwa inahitaji akili kidogo kuendelea kuwapo madarakani na kula kwa uhakika kwa kutumia fimbo ya fedha ambayo imevikwa vazi zuri la takrima ilhali ni rushwa komavu.
Hii ni nafasi nyingine kwa Watanzania kuchagua aina ya maisha tunayotaka kuishi, ama tunataka maisha bora au bora maisha kwa kupokea sahani moja ya pilau na kusahau ugali wa kila siku.
Tusipokuwa makini kuna siku tutajua kuwa misuto ile inatuhusu sisi na umaskini wetu na siyo wao na utajiri wao, chenjelai pambwani uongozi kipaji siyo kazi.
 
Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.