4.+Nape+akihamasisha+kwenye+mkutano+huo,+Kushoto+ni+Mlezi+wa+mkoa+wa+Dar,+Abdulrahman+KinanaKamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC-CCM), mwishoni mwa wiki iliyopita, imetangaza rasmi kumalizika kwa adhabu dhidi ya wanachama wake sita waliodaiwa kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.
 Uamuzi huo wa Kamati Kuu ya chama hicho ulitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma.


 Nape anasema hatua hiyo ya CC imetokana na mapendekezo iliyoyapokea kutoka kwa Kamati ya Usalama na Maadili iliyokuwa ikichunguza tuhuma dhidi ya wahusika hao tangu ilipowasimamisha Februari 18, mwaka jana.
 Nape amenukuliwa na vyombo vya habari akisema CC inatangaza kuwa adhabu dhidi ya wanachama hao sita sasa imemalizika rasmi, na sasa wanaruhusiwa kuendelea na shughuli zao kama kawaida pasipo kukiuka taratibu za chama hicho.


  Pamoja na hayo, anasema kwamba endapo wanachama hao watakiuka tena masharti ya chama, taarifa za ukiukaji wao zitatumika wakati wa kuchuja wagombea. Angalizo hilo ni kwa ajili ya wanachama waliokiuka na watakaokiuka masharti ya chama.
  Wanachama wa CCM walionufaika na kumalizika kwa kifungo hicho ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba.


  Wengine waliotolewa katika kifungo hicho ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, na Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
  Tunasema uongozi wa CCM umeendekeza unafiki na ndiyo maana umekosa hoja za msingi za kuwaadhibu makada wake waliodaiwa kuanza kampeni mapema na kuwaletea usumbufu wanachama wake.


  Kuwatia kifungoni makada na kukwepa kuwaadhibu kama kilivyoahidi chama hicho, kunatokana na udhaifu mkubwa wa kiuongozi wa CCM, kwani adhabu zao zilitakiwa kumalizika Februari mwaka huu, lakini kwa kukosa hoja ilitangaza kuendelea kwa muda usiojulikana hadi CC itakapoamua vinginevyo.
 Uamuzi huo kwa upande mwingine umewafurahisha makada hao ambao tangu awali waligundua kwamba uongozi dhaifu wa chama hicho hauwezi kuthubutu kufanya uamuzi mgumu dhidi yao, na wengine waliendelea kujinadi kwa mbinu nyingine bila kuonywa.


  Kwa unafiki huu uliojengeka ndani ya CCM, inaonesha ndani yao kulikuwa na chuki binafsi dhidi ya baadhi ya makada walioibuka na kuanza kujinadi kuwania urais kabla ya muda.
  Kutokana na unafiki ambao umedumu kwa kipindi kirefu huku viongozi waandamizi wa chama hicho wakikosa ujasiri wa uamuzi mgumu, kunaweza kuibua zaidi makundi ndani ndani ya chama.