Sasa niseme rasmi kuwa mimi nakubali siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kuwa nguzo yetu ya kujitegemea na kututoa hapa tulipo na kutupeleka katika nchi ya ahadi ya kunywa maziwa na asali, nchi ya ahadi ya Eden ambayo kwa hakika ndiyo iliyokuwa Tanzania ya miaka ya 1970.
 Nalaani kwa nguvu zangu zote kufuta Azimio la Arusha, nalaani wote walioshiriki kukataa Azimio la Arusha kwa kuwa limetufikisha hapa tulipo na kwamba umaskini wetu ni chachu ya kuleta mageuzi ya viongozi bora na si bora viongozi.


  Nalaani wapambe wote wanaotumia fursa ya ukaribu kwa viongozi wetu na kuwarubuni na kuwadanganya bila kutoa ushauri mzuri kwa kulinda maslahi yao ya kifisadi na dhuluma kwa Watanzania walio wengi, nawalaani wasaidizi wa viongozi ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kwa kutosema na kufanya yale ambayo wanastahili kufanya kwa manufaa ya Watanzania.


  Nawalaani wote wanaojiita wazalendo huku wakijua nyuma ya pazia ni mafisadi wabaya, wanaofanya dhuluma ya kuharibu maisha ya watu wengine pasi na kujificha nyuma ya mapazia ya viongozi waadilifu walioapa kuwasaidia walalahoi, nimeamua kutoa laana dhahiri bila shayiri.
Leo nina kila sababu ya kulaani matendo maovu yanayofanyika, naweza nikasahau mengine lakini iwapo nitasahau naomba Mwenyezi Mungu asinisahau katika ufalme wake awalaani hao nitakaowasahau mimi.


  Ninawalaani wote wenye akili ndogo ya kufikiri kuwa uchawi na ushirikina ni nguzo ya mafanikio yao katika maisha, nawalaani wanaolinda madaraka yao kwa ushirikina, wanaolegeza nguvu za watendaji wazuri kwa ushirikina pia, wote nawalaani.
Nawalaani wote waliotumia nafasi zao za kimadaraka kutufikisha hapa tulipo katika umaskini mkubwa, nawalaani walioua viwanda vyetu na tukabaki kununua bidhaa zote muhimu na zisizo muhimu kutoka nje ya nchi, nawalaani sana. Naendelea kuwalaani wale wote wanaojua kuwa ugumu maisha niliyonayo unatokana na juhudi zao za kupokea rushwa hata pale ambapo haki yangu ya msingi imekuwa ikipindishwa kwa wao kupokea mlungula, laana na iwe juu yao.  


  Nawalaani wanaotaka madaraka huku wakijua wanafanya hivyo kwa faida zao, kuyashibisha matumbo yao na ya familia zao kwa rasilimali za Taifa letu wote, nawalaani wanaowaunga mkono na laana hii iwe juu ya vichwa vyao.
Nawalaani walioua vyama vyetu vya ushirika, vyama ambavyo vilikuwa vikinunua mazao yetu na kutufanya tulime kwa juhudi sana na kutokomeza adui njaa hapa nchini. Leo wanatufanya tuagize kutoka nje ya nchi hata nyanya za kuunga mboga zetu, lazima laana iwe juu yao.


  Nawalaani wote wanaopinga juhudi za maendeleo kwa kisingizio cha siasa, nawalaani wapenda fedha za siasa ambao kazi yao ni kuimba siasa majukwaani na kutangaza kilimo kwanza huku wakijua dhahiri kuwa kauli zao ni kinyume.
  Nawalaani wote wanaofanya jitihada za kujinufaisha maisha yao huku wakijua kuwa kufanya hivyo kwa kisingizio cha kutukusanya na kutuombea msaada ni makosa, wanatunadi kwa sura za umaskini na wao wanatajirika, laana iwaangukie.


  Najua nafanya makosa kutoa laana lakini nimeamua kufanya makosa na kutoa laana baada ya kuona hakuna njia nyingine mbadala iliyobakia sasa hivi zaidi ya hiyo ya kulaani, labda tutabaki na kizazi ambacho kitakuwa hakina laana na tutafanikiwa kwa kipindi kidogo kilichosalia.
  Nitawalaani wote watakaochukua rushwa ili kupitisha majina ya viongozi haramu katika Taifa letu, rushwa watakayopokea itatupa laana hata sisi wengine kwa kuwa tutakuwa na viongozi ambao mimi nimewalaani kutokana na upatikanaji wao.


  Nitawapa laana zaidi wote watakaoshika kalamu na kuwachagua viongozi ambao wamelaaniwa kwa matendo yao, viongozi ambao si wazalendo, viongozi ambao wanajua wanataka madaraka kwa ajili ya manufaa yao na wenzao.
Nitalaani muhimili ambao utabariki matunda ya viongozi wabadhirifu, viongozi ambao si wawajibikaji, viongozi ambao si mifano kwa tunaowachagua, viongozi ambao wamechaguliwa kwa nguvu ya pesa, viongozi ambao unafiki wa wapambe unawasuta katika mapaji ya nyuso zao.


Nitawalaani wote ambao ni wanafiki wanaoonesha kucheka na kutabasamu mbele ya viongozi waliochagukliwa ambao ni wala rushwa, mafisadi, wazandiki, wanafiki, wanyonyaji, wasio wazalendo, wasiokumbuka Taifa hili limetoka wapi.
Nitawapa baraka viongozi waliochaguliwa kuwa viongozi kutoka katika mioyo yao, waadilifu, wapenda amani na wazalendo kwa Taifa lao, viongozi watakaokumbuka Azimio la Arusha, viongozi watakaokumbuka Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, viongozi watakaoombwa kutuongoza na siyo kuomba kutuongoza.
  Baraka na iwe juu yao na laana itawale kwa wale.

Wasalamu,
Mzee Zuzu
Kipatimo.