Kampuni ya Ujenzi ya Tanpile Ltd ya China inalalamikiwa na wananchi waishio katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa uchafuzi wa mazingira na kelele usiku kucha, zinazosababisha washindwe kupumzika, JAMHURI inaripoti.
Kampuni hiyo licha ya kupewa amri ya Mahakama (stop order) kusitisha shughuli zake za uchanganyaji wa zege katika kiwanda chake kilichofunguliwa katika makutano ya barabara za Samora, Aggrey na Mosque jijini hapa, wamekaidi na hivyo kuendelea na uzalishaji nyakati za usiku.
Baada ya kubainika hayo, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, aliamua kufanya ziara ya ghafla kwenda kushuhudia kinachofanyika kiwandani hapo mwezi uliopita, na kukutana na adha ya kukunjwa shati na Wachina hao.
Silaa ambaye alikuwa ameongozana na baadhi ya Mgambo wa Manispaa ya Ilala, aliokolewa na walimzunguka kabla ya kutoa amri kwa Wachina hao kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.
Meya alithibitisha kufanyiwa vurugu na Wachina hao, lakini aliamua suala hilo liamuliwe kisheria baada ya kufika polisi ambao pia walithibitisha kulipokea na kwamba wangali wakilichunguza.
Wakazi wa maeneo hayo wameieleza JAMHURI kuwa kero kubwa wanayoipata ni kukosa usingizi kutokana na kelele za mitambo ya kuchanganyia zege, malori yanayoingiza mchanga kiwandani hapo na wafanyakazi wanaopiga kelele usiku kucha.
Wanasema athari nyingine zinazotokana na uchafuzi huo wa mazingira ni kusambaa kwa vumbi la saruji na kokoto katika makazi yao na kusababisha wapatwe na maumivu ya vifua na kikohozi.
“Hii ni kero kubwa mno, hatupati usingizi kwa muda mrefu ni kelele tu za malori yanayoleta kokoto na honi zinapigwa usiku kucha na vumbi la saruji linaingia katika makazi yetu, Serikali imeziba masikio pamoja kufikishiwa malalamiko yetu,” anasema Daud Mushi, mkazi wa Mtaa wa Samora katikati ya jiji.
Mushi anasema wamefikisha malalamiko yao muda mrefu katika Ofisi ya Kata ya Mchafukoge na Manispaa ya Ilala, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa na kinachoendelea ni wamiliki wa kiwanda hicho kufanya uzalishaji wa zege nyakati za usiku.
Anasema kinachoshangaza ni viongozi wa jiji kuruhusu Wachina kufungua kiwanda cha kuchanganya zege katikati ya jiji na kwenye makazi ya watu, bila kujali athari za uchafuzi wa mazingira unaotokana na kiwanda hicho.
Mkazi mwingine wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, anasema ni kinyume na sheria za ardhi kubadili matumizi ya ardhi kwa kuruhusu kiwanda kama hicho kuwekwa katikati ya jiji.
Anasema kinachoshangaza ni wamiliki wa kiwanda hicho kupuuza amri waliyopewa ya kusitisha shughuli zao za uchanganyaji wa zege katika eneo hilo.
“Nchi haina utaratibu kabisa, raia wa kigeni wanafanya lolote wanalotaka na ujeuri wao unatokana na rushwa zinazoendekezwa na watendaji nchini,” anasema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mchafukoga, Hassan Mkwawa, anasema uongozi wa kiwanda hicho cha Wachina umekaidi kusitisha shughuli zake licha ya kupewa amri kufanya hivyo kwa zaidi ya wiki mbili.
Mkwawa ameieleza JAMHURI kuwa uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho kilichoko katikati ya makazi jijini haukubaliki kabisa, lakini taasisi zinazohusika zimeshindwa kuchukua hatua dhidi ya kampuni hiyo ya Tanpile Ltd.
Licha ya kelele na vumbi linaloleta kero kwa wakazi wa maeneo hayo, Mkwawa anasema barabara zimekuwa zikichafuliwa kwa kokoto zinazomwagika na kuleta usumbufu mkubwa watu wanaosafisha barabara hizo.
Naye, Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Ilala, Abdon Mapunda, alipohojiwa na gazeti hili kuhusu kero hiyo ya uchafuzi wa mazingira unayotokana na kiwanda hicho, anasema wahusika hawana kibali cha kuendesha shughuli zao katika eneo hilo.
Mapunda anasema wamewapa nakala ya amri ya kusitisha shughuli zao wiki mbili zilizopita, lakini wamekaidi na kuendeleza shughuli zao za kuchanganya zege katika eneo hilo nyakati za usiku.
“Pamoja na kuwapa nakala hiyo, bado wanaendeleza uchafuzi wa mazingira unaoambatana na vumbi la kokoto, saruji na kelele ambazo ni kero kwa wakazi hao, na tunachosubiri ni hatua zitakazochukuliwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC),” anasema Mapunda.
Meneja Uhusiano wa NEMC, Ruth Mgwaza, anasema wanakusudia kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wa kiwanda hicho kwa kuwa hawana kibali chochote kinachowaruhusu kuweka mitambo ya kukoroga zege katikati ya jiji.
Anasema uchafuzi wa mazingira unaoendeshwa na kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia hao wa nchini China, haukubaliki na kwamba hata wahusika wanapoitwa wamekuwa wakikaidi wito mara kwa mara.
Imeelezwa kwamba zege linalochanganywa katika kiwanda hicho linatumika kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kigamboni na jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) linalojengwa mkabala na Ofisi za Jiji la Dar es Salaam.