Jumapili iliyopita ya Aprili 26, Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar ulitimiza miaka 51 tangu ulipoasisiwa mwaka 1964 na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, na hatimaye kuungwa mkono na wananchi wa nchi hizo mbili.
Muungano huo wa Jamhuri ya Tanzania, hadi kufikia leo umesafiri katika barabara yenye neema, imeabiri kwenye bahari ya misukosuko na sasa inaelea kwenye anga ya mashaka hadi kusababisha Watanzania kugawanyika katika makundi mawili.
Kundi linalotaka uendelee kuwapo muungano na kundi linalotaka kuvunjika muungano. Katika barabara ya neema wananchi wa nchi hizo mbili waliupokea na kuufurahia muungano huo, huku wakiwa na matarajio makubwa ya kuboreshewa hali za maisha yao na kuondokana na dhuluma, uonevu, ujinga, maradhi na umaskini.
Misingi ya makubaliano kati ya nchi hizo iliwekwa kwa kuzingatia udugu uliopo kati ya nchi hizo na ishara ya kujenga, kuboresha na kulinda uhuru wa nchi, njia na miundombinu ya uchumi, elimu, afya na tamaduni za watu wote wa Tanzania.
Ni ukweli taratibu za mawasiliano na ushirikiano zilianza na kushika kasi, za umoja kuanzia kwa viongozi wa Serikali, vyama vya siasa hadi kwa wananchi kupitia kwenye sekta zao za kilimo, viwanda, biashara na huduma za jamii.
Shule hadi vyuo vya elimu, zahanati hadi hospitali, ujenzi wa barabara za kudumu na za lami, viwanda vidogo hadi vikubwa, visima na malambo ya maji, viwanja vya michezo na kumbi za burudani; vyote hivyo vilijengwa, viliboreshwa na kupanuliwa kwa maslahi ya wana-Muungano.
Masuala ya uchukuzi, mawasiliano, usafirishaji na utalii yalipewa uzito wake wa kujengwa na kupanuliwa viwanja vya ndege, bandari, reli, ofisi za posta na simu bila kupuuza ushuru na forodha.
Taasisi za fedha na benki za wananchi zilianzishwa. Wanamuungano walipewa heshima ya kumiliki maeneo ya ardhi kwa shughuli za kilimo na ufugaji na vyombo vya uvuvi. Mwisho wa barabara ya neema Muungano ukaingia kwenye bahari ya misukosuko. Hapo nilianza kuwasikia baadhi ya viongozi wa Serikali na wa vyama vya siasa, wakitoa kauli za kueleza kuwa Muungano huu siyo halali kwa sababu haukutokana na maoni ya wananchi. Hauna maslahi kwa baadhi ya wana-Muungano, hatimaye viongozi hao kutiwa misukosuko na kupoteza nyadhiifa zao. Ingawa viongozi wengine waliendelea kuwasisitiza wananchi wasikubali kuvunja Muungano, joto la kuvunja Muungano tayari lilikwishapanda na kuweka mvuke mzito uliosababisha Muungano kupaa juu angani na kuelea kwenye anga ya mashaka. Hapo ndipo ulipo Muungano wetu na sisi kuwa mashakani.
Kauli “hatutaki Muungano tunataka uhuru na nchi yetu. Tumechoka kuonewa” kutoka kwa baadhi ya wananchi ni kauli nzito. Inakolezwa na misemo mbalimbali isemayo Serikali mbili HAPANA. Serikali tatu NDIYO. Lakini kwanza kura ya maoni iwepo kudhihirisha kuwapo au kutokuwapo kwa Muungano.
Kusudio la kutaka kwanza kuwa na kura ya maoni tayari limeanza kuashiria kuikataa KATIBA INAYOPENDEKEZWA kutokana na sababu kadhaa zikiwamo za muungano uliopo siyo maoni na makubaliano ya Watanganyika na Wazanzibari.
Kauli za baadhi ya viongozi wa Serikali ya Muungano zinaeleza kuwa Zanzibar si nchi. Kama Zanzibar si nchi Tanganyika iliungana na nchi gani hata kuunda Tanzania? Wanahoji Wazanzibari na kudai uhuru na nchi yao zirejeshwe kwao.
Wakati huu Watanzania wanasherehekea na kuadhimisha mwaka wa 51 wa Muungano wetu, baadhi ya wananchi hawana shamra-shamra na wengine wamo kwenye nderemo na furaha za Muungano. Huu si muamala mzuri kwa nchi zilizoungana kidugu, kimila na kitamaduni.
Nasema si muamala mzuri kwa sababu watu walio ndugu na walioafikiana kujenga taifa moja lenye nguvu za kiuchumi, kiulinzi na kitamaduni, kufarakana wakati wamo kwenye ujenzi huo ukweli halipendezi na halikubaliki. Kufanya hivyo ni kujisaliti wenyewe.
Jambo kama hilo halikubaliki ndani ya jamii yoyote yenye nia ya kujikomboa kiuchumi na kustarabika kitamaduni kwa sababu ni njia ya kutoa ishara mbili mbaya. Ishara ya kutoelewana ambayo huzaa chuki, uhasidi na mfarakano.
Ishara ya pili ni kutoa mwanya kwa wageni kuvamia nchi na kufanya machafuko na kupora mali na rasilimali za nchi. Umoja wa nchi huparaganyika na kuurudisha huwa ghali na mgumu. Maelezo niliyotoa daima huwa ni matokeo; na matokeo yana asili au chanzo chake. Watanzania hawa kwa maana ya WATANGANYIKA NA WAZANZIBARI, kwa umoja wao, lazima kuna jambo au majambo yanayowakwaza katika shughuli za kiuchumi, kiutawala na kijamii. Ni busara kwa Serikali ya Muungano kujali na kuangalia kwa makini hoja zinazojengwa na kutolewa na upande unaotaka haki na uhuru wa nchi yao. Si suala la kupuuza na kujipa imani eti wanaotaka kuvunja Muungano ni kikundi cha watu wachache. Watu wachache maana yake ni nini?
Wachache wapokewe na wasikilizwe kwa upana wake. Hitilafu zilizopo zitanzuliwe. Huo ndiyo utawala bora.
Na viongozi waandamizi ndani ya Serikali na ndani ya vyama vya siasa, jaribuni kuepuka upambe katika suala zito kama hili.
Chura mzee ndani ya kisima cha maji aliwahi kuwaambia vijana binadamu waliokuwa wakicheza kwa kutupa mawe majini; “furaha ya mchezo wenu kwetu sisi ni mauti.”