Wiki iliyopita Serikali iliibua hoja na kufanikiwa kuzuia baadhi ya maneno yaliyokuwamo kwenye hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzanji Bungeni wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Vincent Nyerere, yasisomwe. JAMHURI inakuletea hicho kilichozuiwa kusomwa.

Katika mwaka uliopita wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji matukio mbalimbali ya mauaji ya raia yaliyowahusisha askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wa vyombo vingine vya dola. Aidha, tulihoji matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi wetu hasa katika maeneo yenye migodi mikubwa ya dhahabu kama vile Nyamongo, Arusha na kwingineko katika nchi yetu. Vile vile, tulihoji sababu za Serikali kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria na za kiutendaji watuhumiwa wa makosa haya makubwa.

 

Mheshimiwa Spika,

Wakati anatoa hoja yake ya kuahirisha Mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka jana, Waziri Mkuu aliahidi kwamba Serikali ingefanya uchunguzi wa matukio yote ya mauaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The Inquests Act), Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania. Kwa maneno yake mwenyewe, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema: “Vifo … ambavyo vimetokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono ya vyombo vya dola, ni lazima vichunguzwe.”

 

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hadi wakati tunaandika maoni haya, hakuna Mahakama ya Korona hata moja ambayo imeitishwa kwa lengo la kuchunguza vifo vilivyotokana na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama kauli ya Waziri Mkuu ilitolewa kwa lengo la kuwahadaa Watanzania. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itamke ni lini Serikali itaunda Mahakama za Korona ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya wananchi katika maeneo yote tuliyoyataja mwaka jana.

 

Mheshimiwa Spika,

Kwa sababu ya Serikali kutotimiza ahadi yake ya kuchunguza matukio ya mauaji kwa mujibu wa Sheria tajwa, vitendo vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vimeendelea kutokea katika nchi yetu. Kwa mfano, katika taarifa yake ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2011, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinaripoti kwamba “mwenendo wa matukio ya ukatili wa polisi na mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na vyombo vya dola umeendelea kuongezeka katika nchi yetu. Kati ya Januari na Desemba 2011 tayari watu 25 wamekwisharipotiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa usalama, wakati ambapo watu wengine 50 walijeruhiwa.”

 

Taarifa hii inaungwa mkono na taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu kuhusu Tanzania iliyotolewa mwaka huu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (State Department), inayoonyesha kuwa bado yapo mauaji yanayotokea mikononi mwa vyombo vya dola ikiwamo Jeshi la Polisi, utesaji na wananchi wanaotuhumiwa kujikuta wakipata vipigo kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.

 

MAUAJI YENYE SURA YA KISIASA

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na Serikali kutochukua hatua kukabiliana na matukio ya mauaji yanayohusishwa na vyombo vya dola, sasa limezuka wimbi la mauaji na matukio ya majaribio ya mauji yenye sura ya kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini. Matukio hayo ni pamoja na mauji ya kada wa Chadema, Mbwana Masudi, yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga, na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, mara baada ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.

 

Aidha, Mheshimiwa Spika, kumekuwa na majaribio ya mauaji ambapo wabunge wa Chadema, Mheshimiwa Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela, na Mheshimiwa Salvatory Machemli wa Jimbo la Ukerewe, walioshambuliwa kwa mapanga mbele ya maafisa polisi na watu wanaosadikiwa kutumwa na makada wa CCM mkoani Mwanza. Vile vile, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) alivamiwa na wafuasi wa CCM wanaodaiwa kutumwa na Iddi Chonanga, Diwani wa Kata ya Nduli (CCM) katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

 

Mheshimiwa Spika,

Matukio ya mauaji au majaribio ya mauaji yenye sura ya kisiasa yamewahusu pia watu ambao si wanachama au viongozi wa vyama vya siasa, lakini wanaonekana kupinga matakwa ya watawala. Haya yamemkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, ambaye alitekwa nyara na kuteswa kikatili na watu ambao taarifa za vyombo vya habari zimewataja kuwa maafisa wa vyombo vya dola.

 

Kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iamuru kukamatwa kwa watuhumiwa wote ambao wametajwa kuhusika na utekaji nyara na jaribio la kumuua Dk. Ulimboka, ili kufuta dhana kwamba vyombo vya dola viko juu ya sheria na vinaweza kuua au kutesa wananchi bila mkono mrefu wa sheria kuwaangukia.

 

Mheshimiwa Spika,

Tarehe 14 Julai 2012, mtu anayesemekana kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM katika Kata Ndago, Jimbo la Iramba Magharibi, Yohana Mpinga, ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa Chadema katika Kata ya Urughu, alifariki dunia kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa Chadema katika Kata ya Ndago.

 

Kwa vile tayari baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali ndani ya Bunge hili tukufu wanaelekea kuwa wameshapitisha hukumu kwamba Chadema inahusika na kifo cha Yohana Mpinga, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina haya ya kueleza kuhusiana na tukio hili.

 

Kwanza, mkutano wa hadhara wa Chadema ulihudhuriwa pia na maafisa polisi waliokuwapo wakati wote wa mkutano huo. Pili, licha ya kuwapo kwa maafisa polisi hao, kundi la wahuni wanaodaiwa kukodiwa na makada wa CCM wa Jimbo la Iramba Magharibi walivuruga mkutano huo kwa kupiga mawe watu waliohudhuria mara mbili, lakini mara zote polisi waliokuwapo hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la wahuni.

 

Aidha, mara baada ya wahuni hao kuvuruga mkutano mara ya pili, viongozi wa Chadema walitoa taarifa rasmi katika Kituo cha Polisi cha Ndago na kufunguliwa jalada namba NDG/RB/190/2012.

 

Tatu, mara baada ya kutoa taarifa hiyo kwa polisi, mkutano wa hadhara uliendelea bila fujo yoyote hadi ulipomalizika na msafara wa viongozi wa Chadema kuondoka eneo la Ndago na kuelekea Kinampanda ambako kulikuwa na mkutano mwingine wa hadhara. Wakati huo, kundi la askari polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kutoka Kiomboi walishafika katika eneo la mkutano na kukuta mkutano umemalizika.

 

Nne, kwa vile mkutano wa hadhara wa Chadema ulimalizika kwa amani mbali na matukio ya kihuni yaliyoripotiwa kwa Jeshi la Polisi, na kwa vile kulikuwa na kikosi cha FFU na askari polisi wengine katika eneo la mkutano baada ya msafara wa Chadema kuondoka, ni wazi kwamba watu wanaotakiwa kutoa maelezo ya jinsi Yohana Mpinga alivyofikwa na mauti ni Jeshi la Polisi lenyewe.

 

Aidha, Mheshimiwa Spika, ni Jeshi la Polisi pekee linaloweza kuwaeleza Watanzania kwa nini kikundi cha wahuni waliowarushia mawe viongozi wa Chadema na wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara, hawakuchukuliwa hatua zozote na polisi waliokuwapo kwa muda wote wa mkutano huo au askari wa FFU waliofika baada ya msafara wa Chadema kuondoka.

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa sana na mauaji ya kijana huyo na inatuma salamu za pole na rambi rambi kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu. Hata hivyo, Kambi yetu inasikitishwa na kushangazwa sana na ushabiki wa kisiasa ambao umejitokeza humu bungeni na kauli za kutoa hukumu ambazo zimetolewa na baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali bila hata kusubiri uchunguzi kamili juu ya jambo hili.

 

MASLAHI YA POLISI NA MAGEREZA

Mheshimiwa Spika,

Katika maoni yake ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia utamaduni wa Serikali kupuuza maslahi ya askari polisi na wale wa Jeshi la Magereza. Utamaduni huu ni wa muda mrefu sana. Kwa mfano, katika hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2006/2007, aliyekuwa Waziri wakati huo alikiri kwamba “…Kutokana na kipato kidogo cha askari polisi, inawawia vigumu kukopa katika mabenki nchini kutokana na riba kuwa kubwa na kukosa dhamana za uhakika.

 

Hivyo, askari polisi hawana mahali popote wanapoweza kupata fedha za kujiendeleza kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwa askari bado haikidhi hali halisi ya mahitaji yao na familia zao.”

 

Tangu wakati huo hadi sasa, maslahi ya askari polisi yamekuwa mabaya zaidi kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei hasa za vyakula kupanda wakati mishahara yao haijaongezeka sambamba na ongezeko la gharama halisi za maisha.

 

Aidha, katika hali inayoonyesha kutokujali kabisa masilahi na hali za maisha za askari wetu, Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyotolewa tarehe 17 Novemba, 2011 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Khamis Sued Kagasheki, aliyeliambia Bunge hili tukufu kwamba “… Posho ya askari imepandishwa na … kwamba (inatakiwa) itoke kwenye shilingi laki moja mpaka shilingi laki moja na elfu hamsini…. Ni jambo ambalo tunalo na tumelifanyia kazi na tuna uhakika kwamba, litaweza kutimia….”

 

Ni ukweli usio na mjadala kwamba askari Polisi na Magereza bado wanapokea posho ya kujikimu ya shilingi laki moja badala ya shilingi laki moja na elfu hamsini iliyoahidiwa na Serikali mbele ya Bunge hili tukufu. Aidha, katika mazingira ya kushangaza kabisa, mara baada ya Serikali kutoa ahadi bungeni juu ya posho hiyo, uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi ulituma maelekezo kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa kufanya uchunguzi ili kubaini askari wote waliokuwa wanadai walipwe posho ya shilingi laki moja na nusu kama ilivyoahidiwa ili askari hao wafukuzwe kazi.

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu ni lini italipa malimbikizo ya baki ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi kwa kila askari Polisi na Magereza ambayo haijawalipa askari hao hadi hivi sasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ianze kuwalipa askari Polisi na Magereza posho ya kujikimu ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi kuanzia mwaka huu wa fedha, kwa vile ahadi ya Serikali iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani haijawahi kukanushwa, kubatilishwa au kubadilishwa na Serikali.

 

Si tu kwamba Serikali haitekelezi ahadi inazotoa bungeni juu ya malipo ya askari Polisi na Magereza; Serikali pia imekuwa inawakopa watumishi hao bila ridhaa yao. Kwa mfano, randama ya fungu la 29 inaonyesha kuwa Jeshi la Magereza linadaiwa jumla ya shilingi bilioni 23.65.

 

Kati ya fedha hizo, watumishi wa Jeshi la Magereza wanaidai Serikali jumla ya shilingi bilioni10.34 ambazo ni malipo ya stahili zao mbalimbali kama vile fedha za likizo, uhamisho, mafunzo, n.k. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili kama, na lini, italipa madeni haya ya askari Magereza wetu wanaokesha magerezani usiku na kushinda juani mchana wakiwalinda wafungwa na mahabusu waliojaa katika magereza ya nchi yetu.

 

Kuna hatari kwa askari wa Jeshi la Magereza kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo tumeyaeleza katika maoni haya. Mfano ni katika Jimbo langu la Musoma Mjini. Mbali na makazi duni ya askari Magereza, vile vile kuna umbali mrefu kati ya kambi ya askari Magereza ya Nyasho na Gereza la Mkoa lililopo Kata ya Mkendo na askari Magereza wamekuwa wakitembea kwa miguu usiku wanapokuwa zamu gerezani.

 

Hii inahatarisha usalama wao kwani wanaweza kuvamiwa na kudhuriwa na wafungwa au mahabusu waliokwisha kumaliza adhabu zao, lakini wakawa na visasi na askari hao.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwapatie gari askari wa Kambi ya Nyasho na makazi mengine ya askari Magereza yaliyoko mbali na magereza wanakofanyia kazi ili kunusuru maisha ya askari Magereza wetu.

 

Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka jana, tulipendekeza kwamba “… Utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa shilingi 5,000 kila mwezi kwenye mishahara yao kwa ajili kugharamia mazishi yao na wategemezi wao, ufutwe mara moja kwani unawanyonya kwa sababu vipato vyao ni vidogo. Badala yake, Serikali ibebe jukumu hilo.

 

Hata hivyo, hadi tunaandika maoni haya, Serikali imeendelea kupuuza mapendekezo haya kwa kisingizio kwamba ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ ni wa hiari ilhali askari polisi wanaendelea kukatwa mishahara yao kwa lazima. Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatamka kwamba kukata mshahara wa mfanyakazi bila ridhaa yake wakati hadaiwi chochote na mwajiri wake, ni kinyume cha sheria husika za nchi yetu na kitendo cha Jeshi la Polisi kuendelea kukata mishahara ya askari polisi kwa ajili ya ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ bila ridhaa ya askari polisi wenyewe kikome mara moja.

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba askari polisi wanaofanya kazi za lindo katika mabenki yote ya biashara hapa nchini hulipwa posho ya shilingi elfu kumi kwa siku. Hata hivyo, Serikali haijawahi kutamka hadharani kiasi ambacho mabenki hayo hulipa serikalini kwa ajili ya kazi hiyo ya kulinda mabenki binafsi.

 

Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu kiasi ambacho mabenki ya biashara hulipa serikalini kwa ajili ya huduma ya ulinzi inayotolewa na askari polisi ili Bunge lako lifahamu kama askari polisi wanaofanya kazi hiyo wanalipwa inavyostahili.

 

VITENDEA KAZI VYA POLISI

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa, makosa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi hapa nchini yalikuwa 62,133. Ripoti inasema kwamba kwa mwaka 2011 makosa 63,703 ya jinai yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini. Kwa kiasi kikubwa, ongezeko hili la uhalifu linasababishwa na askari wa doria kushindwa kufika kwenye maeneo ya matukio ya uhalifu kwa haraka wapatapo taarifa kwa kisingizio cha kukosa mafuta kwa ajili ya magari ya doria.

 

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, nyaraka za Serikali zinaonyesha kwamba Bunge lako tukufu limekuwa likiidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi. Kwa mfano, kwa mujibu wa randama ya Fungu la 28 kwa mwaka huu wa fedha, matumizi halisi ya mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha 2010/2011 yalikuwa shilingi bilioni 2.81. Aidha, katika mwaka wa fedha uliopita Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi bilioni 2.61 kwa ajili ya mafuta, wakati kwa mwaka huu wa fedha Serikali inaomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 2.56 kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi.

 

Wakati Bunge limekuwa likiidhinisha mafungu haya makubwa ya fedha kwa ajili ya mafuta, askari polisi wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya doria hivyo kusababisha askari polisi kushindwa kufanya kazi zao hizo ipasavyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze zinakopelekwa fedha za mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kama gari moja la doria linapatiwa lita 5 za mafuta kwa kutwa na/au usiku.

 

IDARA YA UHAMIAJI NA PAKACHA LA MIPAKA

Mipaka yetu na nchi jirani zinazotuzunguka imekuwa pakacha linalovuja. Ndiyo maana katika hotuba yetu ya mwaka jana tuliliambia Bunge lako tukufu kwamba “… kumekuwa na ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje … kiasi cha kujiuliza kama nchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na kudhibiti uingiaji wa wageni hapa nchini.”

 

Tulionyesha jinsi kulivyokuwa na ongezeko la wageni haramu kutoka nchi za Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Pakistan, Nigeria, China, India na Bangladesh “ambao wanaishi Tanzania kwa mfumo usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo.”

 

Tulitahadharisha kwamba “utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia Tanzania na kuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwapo kwake ni hatari kiusalama, hasa katika zama hizi za kusambaa kwa … ugaidi na uharamia wa kimataifa katika masuala ya fedha, biashara za binadamu …” n.k.

 

Maneno na tahadhari zetu yaliangukia kwenye masikio ya Serikali kiziwi. Na sasa yale tuliyoyasema yameanza kutimia kwani ni mwezi mmoja tu umepita tangu wahamiaji haramu zaidi ya arobaini kutoka Ethiopia kukutwa wamekufa ndani ya lori la mizigo ambalo kwa vyovyote vile lilitokea nchi jirani.

 

Watu hawa waliingiaje nchini na kusafiri hadi katikati ya nchi yetu bila kujulikana na maafisa wa Uhamiaji, polisi wa usalama barabarani na Usalama wa Taifa kama kweli nchi yetu iko salama? Ni afisa gani wa Idara ya Uhamiaji aliyewapitisha katika mpaka wetu wa Namanga au Horohoro au Sirari au Kogaja au Borogonja? Na ni askari polisi gani aliyewasindikiza hadi Kongwa? Aidha, ni afisa mizani gani wa TanRoads aliyepitisha lori walimokuwa watu hao bila kulikagua na kujua kilichokuwamo?

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitarajia – kwa kuzingatia ukubwa na uzito wa kashfa hii – viongozi waadilifu katika Wizara, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi wangewajibika kutokana na uchafu huu. Hata hivyo, hakuna hata mmoja ambaye amefanya hivyo.

 

Kwa vile uwajibikaji wa hiari unaelekea kushindikana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuwawajibisha wale wote waliohusika kuanzia viongozi wa Wizara walioko humu bungeni na uongozi wa juu wa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi, ili kuondokana na aibu hii ya nchi yetu kuwa ‘transit route’ ya biashara ya kusafirisha binadamu katika sehemu hii ya Bara la Afrika.

 

Matatizo ya ongezeko la wahamiaji haramu katika nchi yetu linatokana na Idara ya Uhamiaji kuendekeza vitendo vya kifisadi katika kuajiri, kupandisha madaraja au vyeo wa maafisa wa Idara hiyo.

 

Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, ajira katika Idara ya Uhamiaji haizingatii tena elimu, uwezo na weledi wa maafisa husika, bali, kwa mujibu Taarifa ya Utafiti wa Mpango Mkakati wa Mageuzi Katika Utumishi wa Uhamiaji (Immigration Service Reform Programme Strategic Plan Research Report) iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 27 Novemba 2011, “mara nyingi mgawanyo ya kazi (katika Idara) hautegemei sifa bali unategemea upendeleo, rushwa, kujuana na urafiki vitu ambavyo viko kinyume na maana halisi ya mgawanyo wa kazi.” (“Most of the time placement is not based on merits but depends on nepotism, bribery and technical know-who, friendship and favouritism that have been contrary to the whole meaning of placement.”)

 

Ushahidi wa kauli hii unapatikana katika Taarifa hiyo ya Utafiti inayoonyesha kwamba maafisa wengi wa ngazi za juu katika Idara ya Uhamiaji ni watu wenye uwezo mdogo kielimu kulinganisha na maafisa wa ngazi za chini wa Idara hiyo. Kwa mfano, katika ngazi ya Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji kwenda juu hadi kwa Kamishna Mkuu, kuna maafisa 10 wenye shahada ya uzamili (masters degree), wawili wenye postgraduate diploma (PGD), ishirini na nne wenye shahada ya kwanza, tisa wenye stashahada, saba wenye diploma, kumi na moja wenye kidato cha sita na 248 wenye elimu ya kidato cha nne.

 

Katika maafisa hawa wa ngazi za juu, kuna Kamishna mmoja mwenye elimu ya kidato cha nne wakati kuna Makaimu Kamishna 216 wenye elimu hiyo ya kidato cha nne na Kamishna Wasaidizi Wakuu 31.

 

Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Spika, kuanzia ngazi ya Mrakibu Mwandamizi (Senior Superintendent) kwenda chini mpaka koplo kuna maafisa wenye shahada ya uzamili 36, wenye postgraduate diploma wako saba, wenye shahada ya kwanza wako 340, wenye stashahada wako 78, diploma wako kumi wenye cheti (certificate) wako 52, waliomaliza kidato cha sita wako 585 wakati waliohitimu kidato cha nne wako 337.

 

Katika mazingira ambayo maafisa wenye uwezo mkubwa wa elimu hawapewi nafasi za juu katika Idara, badala yake uongozi wa juu umejazwa na wenye elimu za mashaka kama inavyoonyeshwa katika Taarifa ya Utafiti ya Wizara, ni wazi kwamba matukio kama ya maafa ya wahamiaji waliokutwa wamekufa jimboni kwa Naibu Spika wa Bunge hili tukufu, hayawezi kuepukika!

 

Aidha, Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya upendeleo na rushwa katika ajira ya Idara ya Uhamiaji ya aina hii, maafisa Uhamiaji hawawezi kuacha kutumiwa na wanasiasa wa chama tawala kuwatuhumu washindani wao kisiasa kuwa si raia wa Tanzania ili kuwaondoa katika kinyang’anyiro cha chaguzi zetu. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mheshimiwa Ali Mohamed Keissy alipotaka kugombea Ubunge kwa tiketi ya Chadema na kuzushiwa tuhuma kuwa si raia.

 

Hata hivyo, alipojiunga na CCM bila ridhaa yake tuhuma za kutokuwa raia ziliyeyuka na sasa ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini katika Mkoa anakotokea Waziri Mkuu!