Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,amekagua miradi ya maendeleo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha afya cha Iglanson, Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta na Hospitali ya Wilaya ya Ikungi vyote vikiwa wilayani humo mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja.

Akikagua ujenzi wa kituo cha afya Iglanson na kuweka jiwe la msingi la kituo hicho jana Waziri Mkuu,Kassim aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho kilichopo jimbo la Singida Magharibi unakamilika ifikapo mwishoni mwa Agosti mwaka huu ili kiweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Iglansoni katika ziara yake ya kukagua miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo hicho ambacho Serikali ilishatoa zaidi ya Sh.milioni 500.

“Mhandisi simamia kumalizia jengo ili mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti huduma zianze kutolewa mara moja ili wananchi waondokane na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za matibabu Singida mjini na Itigi,” amesema.

Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi, pamoja na kwamba rais ametoa kibali cha ajira za madaktari watakaoletwa kwa ajili ya Wilaya ya Ikungi waletwe moja kwa moja katika kituo cha afya Iglansoni.

“Jengo nimeliona limekamilika kwa asilimia 98 sasa huduma za upasuaji zitafanyika hapa hapa hakutakuwa na sababu ya kutembea umbali mrefu kwenda Singida au Itigi kufuata huduma,” amesema.

Waziri Mkuu amesema serikali italeta fedha nyingine Sh.milioni 250 kwa ajili ya kujenga wodi ya wanaume na wanawake,mochwari na kujenga nyumba za kuishi madaktari watakaokuwa wakitoa huduma katika kituo hicho cha afya.

Aidha,alisema katika magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) ambayo serikali itahakikisha moja linaletwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambalo litakuwa linatoa huduma kwenye kituo cha afya Iglansoni kwa wagonjwa wanapewa rufaa kwenda hospitali ya wilaya Ikungi.

Kuhusu ombi lililotolewa na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu,la kutaka jimbo hilo lipewe Halmashauri kwa kuwa ni kubwa kwani wananchi wamekuwa wakitembea urefu za zaidi ya kilometa 200 kufuata huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Majaliwa aliwagiza viongozi kufuata taratibu zote zinazotakiwa kwa kuitisha vikao kuanzia ngazi za chini hadi juu na kupeleka mapendekezo na ikimpendeza rais ambaye ndiye mwenye mamlaka na hilo atatoa maelekezo ya kuanzishwa halmashauri mpya katika jimbo la Singida Magharibi.

Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),David Silinde, alisema serikali imeshatoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 234 nchi nzima.

Amesema katika mkoa wa Singida serikali ilitoa Sh.bilioni 13.3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 667 katika shule za sekondari na msingi.Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi,Justice Kijazi, alimweleza Waziri Mkuu kuwa Serikali imetoa Sh.milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kitatoa huduma kwa wananchi 13,608 wa vijiji vya Iglansoni na Mnyange.

Amesema changamoto iliyojitokeza katika utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na upatikanaji wa vifaa ambavyo vilikuwa vinapatikana katika umbali wa zaidi ya kilometa 100 na tatizo la maji smbapo pipa moja lilinunuliwa kwa Sh.500 hali ambayo imesababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro,amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vinne vya afya pamoja na ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambayo imepewa Sh.milioni 800.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa fursa kwa wabunge wa maeneo ilipo miradi hiyo kuzungumzia miradi hiyo inayotekelezwa kwa kutolewafedha nyingi na Rais Samia Suluhu Hassan.

Wabunge waliopata fursa hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu ambako kimejengwa kituo cha Afya cha Iglanson, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambako kimejengwa chuo cha Ufundi Stadi cha VETA na Hospitali ya Wilaya.

Wabunge wngine waliopata fursa hiyo ni pamoja na Mussa Sima Mbunge wa Singida mjini na Mbunge wa Viti Maaalum Mkoa wa Singida, Martha Gwau na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, JUuma Killimbah.