Wiki iliyopita kwa mara nyingine taifa letu limeshuhudia majonzi ya aina yake baada ya Watanzania wengine wapatao 150 kupoteza maisha baada ya meli waliyokuwa wakisafiria kuzama.
Meli hii mv Star Gate ambayo wengine wanaiita Skagit, inayomilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Ltd, ni ya pili kati ya meli zinazomilikiwa na kampuni hii kuzama baharini ndani ya muda mfupi. Miaka miwili iliyopita meli yao MV Fatih ilizama kwenye Bandari ya Malindi na kuua watu sita.
Itakumbukwa kuwa Septemba mwaka jana, watu wasiopungua 200 walifariki katika Bahari ya Hindi, wakati meli ya mv Spice Islander ilipozama ikiwa safarini kutoka Unguja kwenda Pemba. Huu pia ulikuwa mwendelezo wa vifo vya watu wapatao 800 – japo wengine wanasema 1000 – baada ya meli ya mv Bukoba kuzama katika Ziwa Victoria Mei 21, 1996.
Tangu 2006 dunia imeanza mchakato wa kuhakikisha inaweka viwango vya uhakika kwa usafiri wa majini. Kimeanzishwa chombo kiitwacho Global Forum on Oceans, Coasts and Islands – Strategic Oceans Planning to 2016. Jukwaa hili linalenga kuratibu mwenendo wa meli zinazokadiriwa kuwa zaidi ya 94,000 ambazo baadhi ni mpya, zenye uwezo mkubwa lakini pia zipo zilizochoka. Ni kwa mantiki hiyo ajali zimekuwa nyingi kwa kiwango kinachotia shaka.
Nikirejea katika meli iliyozama na Watanzania zaidi ya 150 kupoteza maisha juzi karibu na kisiwa cha Chumbe, napata masikitiko ya mwaka. Ukiacha suala la hali ya hewa, inaelezwa kuwa meli hii ya Star Gate ilisitishwa matumizi mwaka 2006 huko Marekani baada ya kuwa imezeeka (condemned). Meli hii ilinunuliwa miaka 15 iliyopita kwa gharama ya dola milioni tano. ‘Mwekezaji’ aliyeileta Tanzania akainunua kwa gharama ya dola 400,000.
Hii inanikumbusha boti za kasi za kampuni ya Mohammed Enterprises zilizobishaniwa kati ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Mark Mwandosya, akitaka zitumie barabara zetu wakati wa kupelekwa Ziwa Victoria, huku Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, akisema hazina faida yoyote kwa wananchi zaidi ya kuharibu barabara na kwamba boti hizo zilikuwa mitumba. Zilizungushiwa Bandari ya Mombasa, nchini Kenya zikaingizwa Ziwa Victoria, lakini uliza zilifanya kazi siku ngapi? Leo hazijulikani hata kama zilipata kuwapo.
Sitanii, tatizo linaloikabili nchi yetu ni kuendesha mambo mengi kwa dili. Sitaki kuamini kuwa meli hii ya mv Star Gate iliingizwa nchini bila kufahamika gharama yake ya ununuzi na hali yake. Kibaya zaidi ni utaratibu unaotumika bandarini Dar es Salaam. Kwa bahati nzuri, ofisi za gazeti letu zipo Mtaa wa Samora mkabala kabisa na ofisi nyingi za usafiri wa meli ziendazo Zanzibar. Tunashuhudia yanayotokea kwa wasafiri waendao Zanzibar.
Ingawa wanatajwa kufariki watu 150 uhalisia wanaweza kuwa hata 400. Tiketi zinazouzwa mkononi bila kuandika majina ya wasafiri ni nyingi kuliko zinazouzwa kwenye ofisi maalumu. Ukiacha kwamba ndugu na jamaa wametafuta zilipo ofisi za meli hiyo bila mafanikio, ukweli unadhihiri kuwa nje ya bandari kuna vijana wengi wanauza tiketi nyingi mkononi kuliko idadi ya wasafiri wanaokwenda dirishani kununua tiketi kutoka ofisi husika.
Sitanii, hili nalo mbali na kuwa tatizo, kero yangu kubwa ni uwezo wa Serikali kushughulikia majanga. Wameokolewa watu 145, lakini kasi ya kuokoa watu inasikitisha. Ukiwasikiliza viongozi wengi wanasingizia hali ya hewa. Wanasema kuna upepo mkali baharini kwa sasa, lakini kweli umbali wa maili sita ilipotokea ajali tumeshindwa kuokoa watu wetu?
Hivi wakubwa hawa wanataka kusema nchi yetu haina uwezo wa kununua helikopta angalau moja ya kufanyia uokozi? Tumeshuhudia helikopta ya polisi ikiruka juu ya eneo ilipozama meli, lakini haina msaada wowote zaidi ya kuchukua taarifa ambazo zingeweza kuchukuliwa kwa mtumbwi. Tumeshuhudia nchi za wenzetu yakitokea mafuriko au vyombo vya majini kuzama, watu wanafungwa mikanda, wananyanyuliwa juu na kuondoshwa kwa helikopta.
Nimejaribu kuangalia bei za helikopta zilizotumika (used) aina ya EC 120B Colibri kuwa zinauzwa kati ya Sh bilioni 2.5 hadi Sh bilioni 3. Bei hizo ni pale unapoamua kununua kutoka Uingereza, ukienda Marekani unaweza kununua hata helikopta kwa wastani wa Sh milioni 700 iliyotumika kidogo, sawa na mashangingi matatu wanayotumia wabunge na mawaziri wetu.
Najua hapa itaibuka hoja kwamba hatutumii vitu ‘used’, ila mimi siielewi nchi hii. Mawaziri na wabunge magari ya ofisi wanasisitiza yawe mapya, lakini wakifika majumbani mwao wananunua magari ‘used’. Hivi tutakuwa tumefanya kosa lolote kununua helikopta hata tatu ‘used’ zikatusaidia kuokoa maisha ya watu wetu wakati wa majanga? Tutaendelea kusingizia hali ya hewa mbaya hadi lini?
Wenye meli nao ni tatizo. Maboya ndiyo nimeona wachache walioyavaa lakini watu wengi waliopoteza maisha na idadi ya maboya yaliyovaliwa kumeacha maswali mengi. Kama maboya yangekuwapo, basi tungeweza kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.
Sitanii, hapa tatizo ni moja tu – usimamizi mbovu. Viongozi wetu hawajifunzi. Nilidhani baada ya mv Bukoba na Spice Islander tungejifunza, lakini nakuhakikishia hata baada ya ajali hii bado itatokea nyingine siku za usoni, na tutaomba wazamiaji kutoka Afrika Kusini na Israel – hivi kweli? Tunao Wakerewe wanaojua kupiga mbizi kama nyambizi, lakini hatujawahi kupata fikira ya kuwapa mafunzo kidogo tu tukawatumia kama waokoaji kwenye Jeshi la Wanamaji.
Inawezekana hadi aseme Mzungu ndiyo mtaamini kuwa ni wazo sahihi. Leo akisema Balile kuwa Watanzania wenzangu hawa wafuga kakira wanao uwezo mkubwa wa kupiga mbizi waongezewe vifaa na kuwa jeshi la dharura, si ajabu wewe unayesoma utasema ni kweli hii, lakini yataishia hapo hadi aje Mzungu.
Sitanii, hatuwezi kuendelea na hali hii. Najua si rahisi kuzuia majanga, japo tunao uwezo wa kuzuia yanayotokana na uzembe, lakini naamini sasa tunapaswa kuongeza kigezo kingine wakati wa kupiga kura. Mgombea urais atwambie kabla hatujampigia kura kuwa akichaguliwa ataliandaaje taifa kukabiliana na majanga kama haya! Jamani eheee, nasema tuondokane aibu hii. Tununue helikopta na Wakerewe wapewe kazi ya kupiga mbizi.