Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Taasisi 10 zimeandikiwa wito wa kuhudhuria mjadala wa kupitisha sheria za habari zinazolalamikiwa kuhusiana na mabadiliko ya vifungu mbalimbali vya habari ambayo wadau wanavipigia kelele kwamba, vinaminya uhuru wa habari nchini.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa serikali kuitisha mjadala ili kupitia sheria za habari zinazolalamikiwa na kuonesha dhamira ya kweli kuelekea mabadiliko hayo.
Akizungumzia hatua hiyo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile,jijini Dar es Salaam amesema kuwa serikali inatarajia kukutana na wadau wa habari nchini.
Hivi karibuni,erikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeitisha mkutano wa wadau wa habari kuzungumzia vipengele mbalimbali vya habari vinavyoonekana kuminya tasnia hiyo.
Balile amesema, mchakato umeanza kuzaa matunda “wiki hii tumepata mwaliko kutoka serikalini ambapo tutakuwa na mkutano wa pamoja kati ya serikali na wadau wa habari utakaofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere.
“Kuna mwelekeo sasa kwamba, kama tunakwenda kwenye huu mkutano wa tarehe 11 na 12 Agosti mwaka huu, tunaweza kuona hii sheria inapelekwa bungeni Septemba mwaka huu kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza.
“Sasa tusiende kusoma sheria ambayo kwamba tutaenda na mivutano, tumeishakubaliana na Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye, tumeishakubaliana na mheshimiwa rais (Rais Samia Suluhu Hassan), kwa hiyo tunaamini kwamba, watatusikiliza kwenye mkutano na tutalizungumza ili tupitie yote ili tusipeleke vipande vipande.
Amesema, mjadala huo unahusu kujadili vifungu vya sheria za habari ili kuona jinsi gani tunarekebisha kifungu kwa kifungu, ili ziwe nzuri kama wadau walivyoomba.
Amesema, mchakato wa mabadiliko umepiga hatua kubwa tangu ulipoanza na kwamba, hatua ya serikali kuitisha mkutano wa wadau kujadili vipengele vya sheria hizo, unaashiria kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuwasilishwa kwenye Bunge la Septemba mwaka huu.
Balile amesema, kwenye mapendekezo yao miongoni mwa vipengele wanavyotaka kufanyiwa kazi ili kulinda uhuru wa habari ni pamoja na kuondoa utitiri wa vyombo vinavyosimamia tasnia ya habari.
Na kwamba, muundo wa vyombo vilivyoelekezwa na sheria iliyopo, unaweza kuvunjwa na kuunda chombo kimoja ambacho kitakuwa imara na kusimamiwa kisheri kama ilivyo katika taaluma nyingine nchini.
“Sisi hatupingi Bodi ya Ithibati ila tunasema kwamba, kutenga Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Vyombo vya Habari, unakuwa umeleta shida kwasababu, ukiwa na Baraza la Ithibati halafu Baraza Huru la Habari, unakuwa na vyombo viwili vinavyofanya kazi ile ile.
“Lakini tunasema, kama wanasheria wanayo Tanganyika Laws Society; Hiyo hiyo inafanya kazi ya ithibati (inawapa vitambulisho), inasuluhisha pale mwanasheria anapokwenda kinyume. Hivyo, tunataka chombo kimoja (Baraza la Habari) litakaloundwa kwa mujibu wa sheria liwe na mamlaka yote hayo,” amesema Balile na kuongeza;
“Baraza tunalotaka litakuwa na kazi ya kufanya ithibati; kwamba litawapa waandishi vitambuliisho, litashughulikia kesi zinazohusu tasnia ya habari lakini kama ilivyo sasa.”
Amehoji, ikiwa taaluma nyingine kama madaktari, wagavi pia mainjinia wamekuwa na bodi zao ambazo zinashughulikia kila kitu kinachowahusu, lakini kwenye tasnia ya habari igawanywe vipande vipande.
Amesema, kuna vipengele vingi ambavyo vinapaswa kuguswa kwenye maboresho hayo, hata hivyo ameisifu serikali kwa hatua ya kukutana na wadau ili kuingia katika hatua nyingine ya mabadiliko ya sheria kandamizi za habari nchini.
“Katika tasnia ya habari imegawanywa vipande vine; imegawanywa kwenye Baraza Huru la Vyombo vya Habari, imegawanywa kwenye Baraza la Ithibati, imegawanywa kwenye Mfuko wa mMafunzo na imegawanywa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.
“Sisi tunasema, hatuna shida na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, anaweza kuendelea kuwepo na akafanya shughuli zake ambazo zimeanishwa chini ya sheria, lakini hivi viwili; Mfuko wa Mafunzo na Baraza la Ithibati viunganishwe kwenye Baraza Huru la Vyombo vya Habari.
“Labda watueleze kama wanamaslahi ya ziada, kwanini wanataka waendelee na mfumo huu ambao ni wa serikali kuthibiti vyombo vya habari? basi watueleze, tutaelewani pengine,” amesema.