Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mbeya

NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, ameitaka BoT kuongeza uhamasishaji kwa wananchi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, pamoja na shughuli zingine za kilimo, kuwekeza katika dhamana za serikali.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, alipofika katika banda la BoT kwenye Maonesho ya Wakulima ya Nanenane kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Serikali wa Kushirikisha Vijana katika Kilimo Biashara. (Picha na Benki Kuu)

Dkt. Kayandabila ameyasema hayo alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Wakulima – Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya mapema leo.

“Hamasisheni zaidi wananchi wa Kanda ya Nyanja za Juu Kusini kuwekeza katika dhamana za Serikali,” alisema Naibu Gavana wakati alipotembelea meza ya Masoko ya Fedha, ambapo alielezwa kwamba wananchi wamekuwa wakifika kupata elimu kuhusu uwekezaji katika dhamana za serikali.

Dkt.Kayandabila pia ameagiza kuongezwa kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kutoa elimu kwa wananchi ili kurahisisha uelewa badala ya maelezo pekee.

Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, akifafanua jambo kuhusu sekta ya fedha kwa wakaguzi wa mabenki alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane jijiini Mbeya. Kushoto ni Mkaguzi wa Mabenki Mwandamizi, Bw. Gwamaka Charles, Afisa Sheria BoT, Bw. Ramadhani Myonga na Afisa kutoka Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Bi. Joyce Shala

Akiwa katika meza ya Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi katika banda hilo la BoT, Naibu Gavana ameagiza takwimu za bei za mafuta katika soko la duni kuchakatwa na kutoa matarajio kwa wananchi kuhusu bei za bidhaa hiyo muhimu katika siku za usoni.

“Angalia takwimu za mafuta kwa kipindi cha miezi na wiki kadha. Toa matumaini kwa wananchi kuhusu mwelekeo wa bei hizo kwa siku za usoni,” amesema Dkt. Kayandibila.

Kuhusu masuala ya mifumo ya malipo ya taifa, Naibu Gavana ameitaka Benki Kuu kufanya kazi na wadau wengine, ikiwemo Wizara ya Fedha na Mipango ili kupunguza malalamiko ya wananchi ambayo yanajitokeza mara kwa mara.

Benki Kuu ya Tanzania inashiriki katika Maonesho ya Nanenane kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo utafiti na sera za uchumi, namna ya kuwekeza katika dhamana za serikali, namna BoT inavyosimamia mifumo ya malipo ya taifa na sekta ya fedha nchini, Bodi ya Bima ya Amana, Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, namna dawati la kutatua malalamiko ya wateja za mabenki linavyofanya kazi pamoja na elimu ya utambuzi wa alama za usalama katika noti zetu