Serikali kupitia Wizara ya afya imesema kuwa Mpaka sasa hakuna mgonjwa aliyetambulika na kuthibitika kuwa na ugonjwa homa ya nyani (Monkeypox) hapa nchini.

Kauli hiyo imebainishwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe leo Mkoani Manyara wakati akitoa taarfa kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Nyani (MonkeyPox) ambapo hivi karibuni Shirika la afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwepo kwa ugonjwa huo katika baadhi ya nchi Duniani.

Amesema,ugonjwa huo unaoambukizwa na virusi vya Monkeypox na dalili za ugonjwa huu mara nyingi huonekana kuanzia wastani wa siku 5 hadi 21 tangu mtu apate maambukizi.

Ameendelea kusema kuwa,dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na vipele ambavyo vinaweza kuwa na majimaji au usaha, kichwa kuuma, homa, mwili kuchoka, na wakati mwingine inaweza kupelekea kifo hasa kwa watoto wachanga na upungufu wa kinga mwilini.

“Mara nyingi ugonjwa huwa si mkali na wakati mwingine hufanana na tetekuwanga, na hupona bila dawa ndani ya wiki chache. Amesisitiza Dkt. Sichalwe.

Aidha, Dkt. Sichalwe amesema, kuwa ugonjwa huu unaambukizwa toka kwa wanyama jamii ya nyani, panya na kindi ambao hubeba virusi vya ugonjwa wa monkeypox, huku akiweka wazi kuwa, mtu mwenye maambukizi anaweza kuambukiza watu wengine pale anapokuwa na dalili.

“Hivyo ni vyema wananchi wakaondoa hofu maana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kufuatilia hali ya ugonjwa huu katika nchi unakotokea”amesema Dkt. Sichalwe.

Sambamba na hilo Dkt. Sichalwe amesema, madhara ya ugonjwa huu ni pamoja na kifo (case fatality rate), huku akiondoa hofu kuwa, madhara ya kifo sio makubwa na kusema wakiugua wagonjwa 100, watatu hadi sita ndiyo wanaweza kufariki na mara nyingi ugonjwa hupona wenyewe.

Aidha, ameeleza hatua ambazo Wizara ya Afya imechukua tangu kuanza kwa visa vya ugonjwa huo maeneo mbalimbali ya dunia hasa DRC na Ulaya ikiwemo kuandaa mpango ndani ya saa 72 wa kukabiliana na ugonjwa huu kama utatokea na kuandaa mwongozo wa matibabu ambapo utatumika iwapo mgonjwa akitokea.

“Wizara imeandaa mipango ndani ya masaa 72 na mpango wa muda mrefu wa kukabiliana na ugonjwa huu kama utatokea, Wizara imeandaa mwongozo wa matibabu ambapo utatumika iwapo tukipata mgonjwa.” Amesema mesema Dkt. Sichalwe.

Pia, Dkt. Sichalwe ameeleza kuwa, kumefanyika jitihada za kuwapatia mafunzo watumishi 180 waliopo katika mipaka yetu na kuhakikisha vitendanishi vya kupima ugonjwa huu vinanunuliwa ikiwa pamoja na kuhakikisha kuwa dawa za kutibia zinakuwepo.

Mbali na hayo, ameeleza juu ya kuimarisha utambuzi wa Kimaabara ambapo tayari Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii imekwisha fanya upimaji wa sampuli kadhaa za wahisiwa wa ugonjwa huo ambapo wote hawakukutwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha ufuatiliaji kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia vituo vyote vya mpakani ambapo watumishi wamepatiwa mafunzo ya namna ugonjwa unavyoambukizwa, namna ya kuzuia, hatua ya kuchukua iwapo msafiri ataumwa na dalili za ugonjwa kwa ujumla.

Poa, Serikali imeendelea kuimarisha ufuatiliaji wa wahisiwa wa ugonjwa nchini katika vituo vyote vya kutolea huduma kupitia mfumo wa kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Magonjwa na kupitia ukusanyaji wa tetesi mbalimbali (Event Based Surveillance).

Mbali na hayo, Dkt. Sichalwe amewataka Wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kutoa taarifa katika vituo vya kutolea huduma endapo wataona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ili Wataalam waweze kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuwafuatilia waliokuwa karibu na mgonjwa.