UJUMBE wa Benki ya Dunia umetembelea Ofisi za Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, zilizopo jijini Dodoma na kufanya mazungumzo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Honest Njau akizungumza wakati ujumbe wa Benki ya Dunia wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali walipotembelea Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Xavier Daudi

Ujumbe huo umeongozwa na kiongozi wa ujumbe huo Dkt. Tim Kelly, wakiambatana na Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Honest Njau pamoja na watumishi wanaotumika chini ya mradi huo.

Lengo la ugeni huo ni kukagua maendeleo ya utekelezaji wa maeneo yaliyoainishwa kwenye mradi huo ambapo walifanikiwa kutembelea Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na kupokea taarifa ya maendeleo ya utengenezaji wa mifumo ya tehama inayotengenezwa kupitia mradi huo.

Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Honest Njau (kushoto) akiteta jambo na Bw. Xavier Daudi, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora baada ya Ujumbe wa Benki ya Dunia wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kutembelea na kufanya mazungumzo na watendaji wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amezungumzia mifumo mitatu ya tehama inayotengenezwa kupitia mradi huo ambayo itarahisisha upimaji kazi wa watumishi na taasisi pamoja na kumsaidia mwananchi kuzifahamu taasisi za Serikali na taarifa zake kuhusu huduma zinazotolewa.

Aidha, ameitaja mifumo hiyo kuwa ni mfumo wa upimaji kazi wa watumishi (PEPMIS) mfumo wa upimaji kazi kitaasisi (EPIPMIS) na mfumo wa daftari la huduma za Serikali na taarifa zake (Government Servises Directory).

Bw. Daudi amesema kuwa lengo la kutengeneza mifumo hiyo ni Serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa urahisi kupitia mifumo ya kisasa ya tehama na kutimiza dhamira ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Kidijitali.

Kwa Upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali mamlaka hiyo itafikisha mawasiliano ya mtandao wa Serikali kwenye wilaya na halmashauri zote nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Sambamba na hilo amezungumzia maeneo mengine yanayotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya kuhifadhi mifumo katika sehemu za kuhifadhi mifumo pamoja na kuongeza uwezo wa matumizi ya intaneti yenye kasi katika taasisi zote za umma

Amesema kuwa lengo la mradi ni kuboresha huduma za mtandao kwa urahisi na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kiuchumi kwa njia ya mtandao kama vile mawasiliano baina ya wafanyabiashara (wauzaji na wanunuzi)

Akiongea kwa niaba ya ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia, Dkt. Tim Kelly, Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia wa Mradi wa Kidijitali Tanzania amesema ziara ya ujumbe huo imelenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yote ya utekelezaji toka ulipoanza kutekelezwa mwezi wa Septemba, 2022