Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Nanyumbu

KUTOKANA na bei ya zao la mahindi kupanda mara dufu kutoka Sh.6,000 hadi kufikia sh.14,000 kwa debe moja katika wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara,mkuu wa wilaya hiyo Zainabu Chaurembo,amepiga marufuku kufanyika kwa shughuli za jando na unyago kama hatua ya kudhibiti matumizi mabaya ya chakula.

Amesema,shughuli za jando na unyago zinapofanyika katika jamii zinatumia kiasi kikubwa cha chakula na iwapo serikali haitadhibiti mapema shughuli hizo kuna hatari kubwa ya kutokea kwa njaa kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Chaurembo amesema,kupanda kwa bei ya zao la mahindi na baadhi ya mazao mengine ya chakula imetokana na upungufu mkubwa wa mvua za masika katika msimu wa kilimo 2021/2022 hali iliyosababisha wakulima kushindwa kuzalisha chakula kwa wingi mashambani.

Chaurembo amesema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Namijati kata ya Mkanona akiwa katika ziara yake ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo katika vijiji mbalimbali wilayani humo.

Amewataka wananchi kukumbuka kujiwekea akiba ya chakula, badala ya kuingiwa na tamaa ya kutaka fedha kwa kuuza chakula chote ili kuepuka familia zao a kukumbukwa na janga la njaa.

Katika hatua nyingine,Chaurembo amewahimiza wakazi wa wilaya hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kuendelea kupata chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Chaurembo ni kwamba,Ugonjwa wa Covid-19 bado upo na kamwe wananchi wasipuuze kwenda katika vituo vilivyotengwa na Serikali na kusisitiza kuwa,serikali ina wataalam wa kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

“nawaomba sana ndugu zangu kamwe tusipuuze ugonjwa huu,tunendelee kujitokeza kuchanja katika vituo vilivyowekwa na Serikali kwani kuna wataalam wapo kwa ajili yenu”alisema.

Mkazi wa kijiji cha Njisa wilayani humo Shaibu Breki,amepongeza uamuzi wa mkuu wa wilaya wa kuzuia shughuli za jando na unyago kwani utasaidia sana kudhibiti matumizi ya mabaya ya chakula.