Nafuatilia kwa karibu matamshi na maandishi ya makundi mbalimbali ya kisiasa yanayounga mkono wagombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Mahususi ni kusisitiza kwao sifa za msingi za mgombea urais. Napata maswali mengi, majibu machache.
Kwa sababu ya hitilafu ya mfumo uliopo wa kupata wagombea urais, swali la msingi la kuuliza lisibaki kuwa ni nani anazo sifa za kuwa rais ajaye Tanzania. Swali jingine la msingi ni; wale wenye dhamana ya kutuchagulia wagombea urais ndani ya vyama vya siasa wanazo sifa za kuwa na dhamana hiyo?
Sifa moja ya msingi ni kupima iwapo wanatuchagulia wagombea kwa manufaa ya wote, au kwa manufaa ya wachache. Matarajio ya wapiga kura ni kuwa kundi hili, katika kusimamia mchakato wa kupitisha wagombea urais, liongozwe na kanuni ya kutanguliza maslahi ya walio wengi. Ni rahisi zaidi maslahi ya waliyo wengi kuwa njozi kuliko kuwa kusudio halisi.
Katika kila chama tunazungumzia kundi dogo la viongozi ambalo lipo madarakani kwa muda mrefu. Ukubwa au udogo wa kundi siyo jambo la msingi sana ilimradi tu uwepo uhakika wa kutangulizwa mbele kwa maslahi ya wengi. Lakini hatari ya udogo wa kundi unaongeza uwezekano kwa maslahi ya wachache kufanywa kipaumbele cha wengi.
Kwa utaratibu tunaotarajiwa kutumika ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tunazungumzia wajumbe 32 wa Kamati Kuu ya CCM kupendekeza majina matano ya wagombea, ambayo watayawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya CCM yenye wajumbe wapatao 378. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM watawapigia kura wajumbe hao watano na majina matatu ambayo yana kura nyingi zaidi yatapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM wenye wajumbe wapatao 2,100 na kupigiwa kura, na hapo ndipo akapotaibuka mgombea urais wa CCM.
Kundi hili linajumuisha watu wenye matarajio yanayotofautiana, na siyo lazima kuwa yote yawe yenye manufaa kwa Watanzania walio wengi. Tunayoweza kusema kwa CCM tunaweza pia kusema kwa vyama vingine vya siasa. Kwamba uamuzi utakuwa mikononi mwa kundi dogo la viongozi linalosukumwa na mchanganyiko wa maslahi finyu na mapana.
Ni kundi ambalo limeshaonja posho na marupurupu makubwa yanayoambatana na uongozi kwenye nyakati tunazoishi sasa. Kwa wengi wao jambo la kwanza na muhimu kuliko hata maslahi ya Taifa ni kuhakikisha kuwa wanaendelea kushika nafasi ambayo wanayo kwa sasa kama viongozi waliochaguliwa, au kuhakikisha wanateuliwa kwenye uongozi wa rais ajaye.
Rais ana mamlaka makubwa ya kuteuwa Watanzania kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Kwa uzoefu, wagombea wa urais tayari watakuwa wamepanga mabaraza ya mawaziri, nafasi za uwakilishi kwenye balozi za Tanzania nje ya nchi na kwenye mashirika ya kimataifa, wakuu wa mikoa na wilaya, na nafasi nyingine nyingi ambazo zinasababisha wengi wanaotaka kunufaika nazo kufikiria kwanza wao, na Tanzania baadaye. Ongeza fursa za kiuchumi na kibiashara ambazo zinanyemelewa na wale wasiotaka vyeo, na utaona jinsi gani maslahi binafsi yanavyokuwa kichocheo kikubwa cha kupitisha mgombea urais.
Athari moja kubwa ya hali hii ni kuibuka hatari ya kupata mgombea ambaye atapitishwa kwa sababu alikuwa machinga mzuri zaidi; yaani alikuwa mgombea ambaye alitoa ahadi nzuri zaidi kwa wale wanaounga mkono uteuzi wake.
Wanasiasa wanakubaliana kuwa lugha ya biashara kwenye kupanga uongozi ni jambo la kawaida kabisa: “Nitakufanya waziri mkuu iwapo utaniunga mkono.” Na wapiga kura isingetupa shida kubwa iwapo rais, na waziri mkuu wake watakuwa mfano bora na wa kuigwa katika uongozi.
Kwa bahati mbaya umachinga kwenye siasa za leo umetuletea mifano mibovu kabisa ya uongozi ambayo Tanzania imepata kushuhudia. Na hatuoni dalili kama utaratibu huu umesitishwa kwenye mchakato unaoendelea wa kutafuta rais wa tano wa Tanzania.
Wale wajumbe wa Mkutano Mkuu au kikao chochote cha mamlaka wanaomuunga mkono mgombea mmoja, huwa ni nadra kujitosheleza ndani ya kundi la mgombea wao bila kuungwa mkono na kundi la ziada, ambalo hapa nitaliita la ‘upepo’.
Mwanasiasa mmoja mkongwe aliniambia anafahamu idadi kamili ya wajumbe wanaomuunga mkono, wale ambao hawawezi kuacha kumuunga mkono katika mazingira yoyote yanayomkabili. Na alifahamu idadi ya wale wanaomuunga mkono mpinzani wake jimboni.
Alisema kuwa siku zote mapambano yapo katika kushawishi wajumbe ambao wao huangalia nguvu ya kisiasa inaangukia wapi na wataunga mkono upande huo. Na kama nilivyosema, ni nadra kwa nguvu hii kupimwa kwa misingi ya maslahi mapana ya jamii, au uadilifu na sifa za utawala bora.
Kwa wanasiasa, wale wa kufuata upepo na wale wanaopingana nao, kuunga mkono mgombea ambaye hatashinda urais ni sawa na kujihukumu kifungo. Anayetenda kosa hilo anaweza kujikuta taabani kwa kila hali kwa miaka kumi mfululizo wakati wa vipindi viwili ya uongozi wa rais ambaye hakumuunga mkono. Atanyimwa vyeo, atanyimwa fursa, na anaweza hata kuandamwa kwa kutolipa kodi, pamoja na kuwa Mamlaka ya Kodi siyo kitengo cha chama cha siasa.
Mwezi Oktoba wapiga kura tutawapigia kura wagombea urais waliopitishwa na kundi hili dogo la watu wenye sifa zinazopaswa kutukosesha usingizi. Hawa hatuwazungumzii, tunazungumzia wale watakaowapitisha pekee. Na kama bado tunapata usingizi, hatujazungumzia pia sifa na ushawishi wa makundi kutoka nje ya nchi yenye malengo yasiyoleta manufaa kwetu.
Kwa mtaji huu, na kujibu swali ambalo nimeuliza hapo awali: wale tuliowapa uwezo wa kutuchagulia wagombea urais hawapati alama nzuri kwenye kipimo cha sifa za kuwa na dhamana hiyo. Rais tutampata, lakini kama ambavyo mchambuzi mmoja wa siasa alivyotamka: ni nadra kwa mgombea bora kuchaguliwa kuwa rais.