Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Mwanza
Daraja la JP Magufuli linalojengwa Mwanza na kuziunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema kupitia Ziwa Victoria linatarajiwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati na la sita kwa urefu barani Afrika kwa takwimu za sasa.
Kauli hiyo imetolewa jijini hapa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund Board), Joseph Haule, wakati walipokagua utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo.
“Kama mnavyoona Tanzania sasa tunazidi kupaa, tumeona madaraja mengine mengi makubwa na mazuri yakichukua rekodi lakini sasa daraja hili ndilo litakalovunja rekodi nchini, Afrika Mashariki na Kati, na kwa kweli mradi huu utakapokamilika tutajivunia sisi Watanzania, ” amesema.
Ameyataja madaraja marefu zaidi Afrika kwa takwimu za sasa kuwa ni Daraja la 6th October (Misri) lenye urefu wa kilomita 20.5, Daraja la Third Mainland (Nigeria) lenye urefu wa kilomita 11.8, Daraja la Suez Canal (Misri) lenye urefu wa kilomita 3.9, Daraja la Kisiwa cha Msumbiji lenye urefu wa kilomita 3.8 na Daraja la Dona Ana (Msumbiji) lenye urefu wa kilomita 3.67.
“Tumeambiwa kwamba itakapofika mwaka 2024 daraja hili litakabidhiwa kwa serikali kama ilivyo katika mkataba wa ujenzi wake, licha ya changamoto za Uviko-19, maji kuongezeka, pamoja na uwepo wa miamba chini ya maji.
“Lakini inafurahisha zaidi kwamba vifaa kama nondo na simenti zinazotumika katika mradi huu zinatoka hapa nchini,” amesema.
Haule amesema bodi hiyo imetembelea mradi huo kwa kuwa ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha daraja hilo linatunzwa wakati wote na wameridhika na teknolojia inayotumika.
Naye Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Yooshin Engineering Corporation, Abdulkarim Majuto, amesema kasi ya utelelezaji wa mradi huo ni nzuri na hadi sasa umefikia asilimia 48.9, na jumla ya nguzo 22 kati ya 67 zimeshainuliwa na tayari wameanza kulaza bimu kisha wataanza kumwaga zege na kuweka lami.
Kuhusu gharama za mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose, ameiambia bodi hiyo ujenzi wa daraja hilo unagharimu Sh bilioni 716.3 na unafadhiliwa na serikali kwa asilimia 100.
Amesema hadi kufikia Julai, 2022 tayari mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 223 na mhandisi mshauri ameshalipwa Sh bilioni 3.29 huku Sh bilioni 3.1 zimelipwa kama fidia kwa jumla ya waathirika 165 waliopisha mradi huo.
Awali, Meneja Msaidizi (Ufundi) wa bodi hiyo, Rashid Kalimbaga, amesema kazi yao ni kukusanya fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara zote Tanzania Bara pamoja na madaraja yake ili kuhakikisha yanakuwa katika ubora wake kwa vipindi vyote vilivyokadiriwa.
Mkazi wa Busisi, Lameck Masunga, amesema ujenzi wa daraja hilo umeleta neema kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo hasa vijana wamepata ajira 764 kati ya zote 820, pia biashara za usafirishaji kwa kutumia bodaboda zimeimarika kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka eneo la mradi.
Mkazi mwingine wa Busisi, Esta Jumanne, ameishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huo kwa sababu utakapokamilika utaondoa adha kubwa ya kusubiri kivuko cha kwenda Misungwi, kwa sababu sasa hivi inawachukua zaidi ya saa moja kuvuka kwenda upande wa pili wakati kwa kutumia daraja itakuwa ni chini ya dakika tano.
Daraja hilo litakapokamilika litaziunganisha Misungwi na Sengerema zinazotenganishwa na Ziwa Victoria katika barabara kuu ya Usagara kupitia Sengerema hadi Geita.
Barabara hiyo pia ni sehemu ya barabara zilizoko katika Ushoroba wa Ziwa Victoria inayoanzia Sirari mpakani na Kenya hadi Mutukula mpakani na Uganda (urefu wa kilomita 792.5).