Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Liberata Mulamula ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika jijini Pretoria,Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai, 2022.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 23 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Tathmini ya Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt.Naledi Pandor amesema hali ya usalama katika kanda kwa ujumla inaridhisha na kwamba Nchi Wanachama wa SADC ziendelee kujitolea katika masuala ya ulinzi na usalama kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi hizo.
Kadhalika amesisitiza nchi wanachama kuendelea kupambana na ugaidi na vitendo vyote vya kigaidi katika Kanda huku akipongeza Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya nchini humo ambapo wamefanikiwa kurejesha hali ya amani na usalama katika Jimbo la Cabo Delgado.
Kuhusu utekelezaji wa maazimio yatokanayo na Mkutano wa 23 wa Kamati hiyo ya Mawaziri,Dkt. Pandor amezipongeza Nchi Wanachama na Sekretarieti ya SADC kwa kutekeleza maazimio hayo kwa takriban asilimia 81.
“Utekelezaji huu bila shaka unadhihirisha dhamira ya dhati iliyopo miongoni mwetu ya kuhakikisha tunafikia lengo la kuimarisha amani na utulivu katika kanda”, amesema Pandor.
Akizungumzia masuala ya demokrasia katika nchi wanachama,Pandor amesisitiza nchi wanachama kuendelea kuendesha chaguzi zake kwa kufuata miongozo ya kidemokrasia ya SADC na ile ya nchi husika ili chaguzi hizo zikamilike kwa amani na utulivu.
“Katika kujenga amani na utulivu katika kanda, SADC itaendelea kuzingatia misingi ya demokrasia ili kuzuia migogogoro kwa maslahi mapana ya wananchi katika kanda. Kwa kuzingatia misingi hiyo SADC kama kanda itaendelea kuendesha chaguzi kwa kufuata misingi ya demokrasia, uwazi, amani na ukweli. Serikali za Angola na Lesotho zitakuwa na uchaguzi mkuu mwezi Agosti na
Oktoba mwaka huu mtawalia. Tunawatakia wanachama wenzetu uchaguzi wa amani” alisisitiza Pandor.
Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi.
Pia amempongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Pandor kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia na kumwahidi ushirikiano.
Mbali na Balozi Mulamula, Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman,Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa
Polisi Salum Hamduni, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.
Kupambana na Rushwa,Kamishna wa Polisi Salum Hamduni na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.