Ningali nakumbuka siku niliposikia neno hili “MPARAGANYIKO”. Mara ya kwanza, sikulielewa. Ilikuwa mwaka 1979 kama mwezi Aprili hivi, nikiwa nafanya kazi Visiwani Zanzibar katika vikosi vya SMZ. Niliwajibika kuwamo katika misafara ya ziara za Rais visiwani.
Siku ya siku, kulikuwa na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Kisiwa cha Pemba. Tulishazuru sehemu kadhaa, kwa siku mbili na siku ya tatu ilikuwa tunakwenda kisiwa kimoja katika Bahari ya Hindi kwa kutumia boti.
Jioni, tukiwa Ikulu Ndogo Chake Chake tunapanga safari ya kesho yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mheshimiwa Ally Mzee (sasa ni marehemu) alipigiwa simu na aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ndugu Timothy Apiyo (naye sasa ni marehemu), ikimweleza kuwa asubuhi inayofuata kutakuwa na kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri Dar es Salaam na Rais wa Zanzibar aliombwa kuhudhuria kikao kile saa 4 asubuhi.
Mara moja ratiba ya siku ile iliyoandaliwa kule kisiwani Pemba iliahirishwa. Asubuhi tulikwenda Uwanja wa Ndege wa Chake Chake kumsindikiza Rais, hadi saa 4 asubuhi hapakutokea ndege ya Serikali kuja kumchukua Rais wa Zanzibar. Muda kidogo baada ya saa 4, Mheshimiwa Ally Mzee alipokea simu kutoka Ikulu, Dar es Salaam kumwarifu kuwa hawakuwa na ndege asubuhi ile hivyo aombwe radhi Rais kwa tukio lile lisilotarajiwa.
Mheshimiwa Rais wa SMZ alihuzunishwa na taarifa ile na alikasirika kupoteza siku ile. Tukiwa pale VIP (sehemu ya wageni mashuhuri) ya Uwanja wa Ndege wa Chake Chake nilimsikia Mzee Aboud Jumbe, Rais wangu, akitamka “lahaula MPARAGANYIKO” gani huu. Hii nini sasa? Ziara yangu ya hapa Pemba nilifuta, haipo na kikao cha Baraza la Mawaziri kule Dar es Salaam siendi. Loh! Huu ni “MPARAGANYIKO mtupu”. Haya twendeni mjini leo tena siku imepotea! Mambo haya yanaudhi sana; alisononeka Rais wa SMZ.
Mimi kwa kutokuelewa neno lile “mparaganyiko” nilimfuata Waziri mmoja wa SMZ nikamwuliza, “afande pale mzee ametumia neno nisilolifahamu – kuparaganyika, alikuwa na maana gani?” Nikaelezwa vizuri hapo nikaelewa kumbe mparaganyiko ni mvurugiko au mvunjiko wa mpangilio wa utaratibu, au kwenda ovyo kwa mpangilio uliokusudiwa. Kwa maana nyingine ni kuvunjika kwa utaratibu uliopangiliwa kufuatwa ili mambo yaende sawa.
Leo hii nami ninaweza kusema kwa usahihi kabisa kuwa hapa nchini neno hili “MPARAGANYIKO” linastahili kutumika katika suala zima la utaratibu uliokusudiwa wa kupiga KURA YA MAONI kwa Katiba Pendekezwa tunayotarajia kuitolea uamuzi wetu.
Kwa muda wote tangu Bunge Maalum la Katiba likabidhi Katiba Pendekezwa ya nchi hii kwa viongozi wetu, yametolewa matamshi ya kuwataarifu wananchi kuwa kura ya maoni kwa Katiba Pendekezwa itapigwa Aprili 30, 2015. Viongozi wakuu wa nchi hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu wa Serikali wametamka wazi wazi kwa wananchi wajiandikishe kwa wingi na kuhimiza wakapige kura ya maoni kwa Katiba Pendekezwa ifikapo hiyo tarehe 30 Aprili.
Katika kikao cha 19 cha Bunge kilichomalizika wiki chache hivi zilizopita, kumetokea fujo zisizotazamiwa na wananchi. Tumeona katika runinga, tumesoma kwenye vyombo vya habari namna wabunge wa upinzani walivyodai maelezo kutoka serikalini juu ya tarehe ya kupiga kura ya maoni kwa Katiba yetu mpya.
Halikuwa jambo la kupendeza kuona yaliyofanyika bungeni juu ya hili. Haya yalitokea pale Mbunge wa Ubungo, Mheshimiwa John Mnyika, alipogangamala kudai jibu kutoka kwa Waziri Mkuu. Tumesoma maneno haya, nanukuu: “Jambo hili ni la dharura kwa sababu ilikwishatolewa hoja ya dharura juu ya jambo hili katika Mkutano uliopita wa Bunge, ukaagiza Kamati ya Bunge ilishughulikie majibu yatolewe kwenye Mkutano huu wa Bunge, leo mkutano unakwenda kufungwa bila majibu kutolewa…”
Aidha, Mheshimiwa Mnyika aliendelea kuomba kwa Mheshimiwa Spika kwa maneno haya: “Tusitishe shughuli zote, tuhakikishe tunajadili hili, majibu yapatikane leo katika Mkutano huu wa Bunge. Nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara mbili na mara zote Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, naamini umeipa maelekezo ya kutoa majibu, lakini inakwepa kutoa majibu…”
Kwa utulivu kabisa Mama Spika akasimama na kusema: “Hoja hii inafanana na hoja ya kwanza ya Mheshimiwa Jafo (Mbunge wa Kisarawe aliyeomba mwongozo wa Spika akitaka chombo hicho kisitishe shughuli zilizokuwa zimepangwa…) Baada ya majibu hayo ya Spika, tulivyoona kwenye runinga, waheshimiwa wabunge wa upinzani, hawakuridhika na wakakosa uvumilivu, kila mmoja alisimama akawasha kipaza sauti na kuongea bila ruhusa ya Spika. Hii siyo kawaida ya kuongea ndani ya Bunge. Walianza kukosoa majibu hayo ya Spika kwa kudai eti haukuwa utaratibu uliozoeleka mle ndani ya Bunge.
Kwa kuona hali ya makelele na jazba ya wabunge wale wa vyama vya upinzani ndipo Spika alisimama na kutamka… “Njooni ninyi mkae wote hapa muendeshe Bunge… kanuni ya 47 inasema, iwapo Spika ataridhika kwamba jambo hilo ni la dharura na lina maslahi kwa umma basi ataruhusu hoja itolewe kwa muda wa dakika tano na mjadala wa hoja utawezekana, kama Spika ataridhika, sasa kwa sababu Waziri Mkuu anafunga hotuba yake leo, hatujadili hili suala, nawaomba msome kanuni na kuwepo na uvumilivu.”
Licha maombi na maelezo au maelekezo hayo ya Spika, haikutokea ile hali ya utulivu iliyotarajiwa. Wabunge wa upinzani waliombwa watoke nje kama wanataka ili wengine waendelee na kikao. Kwa mshangao wetu sisi watazamaji wa runinga siku ile, tuliona waheshimiwa wale wakipiga makelele na kudai kwa sauti za juu. “Tumesema hatutoki na hakiendelei kitu hapa!” Basi katika hali namna ile ndipo Spika alipolazimika kuahirisha kwa muda kikao kile wakati ule. Hali ya “sintoelewa” haikutokea mle ndani ya Bunge tu, lakini mimi nafikiri hali namna ile iliwakumba wananchi wengi. Tumekuwa na fikra kwa mawazo ya kawaida tu tunajiuliza kama mpaka mwishoni mwa mwezi Machi Tume ya Uchaguzi bado inaboresha Daftari la Wapiga Kura katika mkoa mmoja tu wa Njombe, kweli tutajiandikisha wahusika wote wa mikoa 29 iliyosalia katika kipindi cha wiki nne tu? Itawezekana kweli sisi Watanzania tupige kura yetu ya maoni nchi nzima tarehe hiyo ya 30 Aprili ukichukulia kuna siku nne za mapumziko mwezi huu wa Aprili? (Kuna Ijumaa Kuu, Jumamosi, Jumatatu ya Pasaka na Karume Day, Jumanne) ukiondoa siku za Jumapili nne hapo siku za kazi zinakuwa 22 tu. Utakuwa muujiza kweli sisi wapiga kura watarajiwa wote tuwemo katika hilo Daftari la Wapigakura lililoboreshwa kabla ya tarehe 30 Aprili hii.
Kuna mambo kadhaa muhimu hapa ya kuyafikiria. Yote ni ya msingi kabisa kabla ya kupiga hiyo kura ya maoni. Mosi, Daftari la Wapigakura watarajiwa lazima likamilike ndipo watu waweze kupiga hiyo kura yao ya maoni.
Pili, sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 sura ile ya 5 kifungu cha 3 cha sheria kinasema wazi wazi; Tume ya Uchaguzi itatoa elimu ya uraia na kuhamasisha wadau kwa muda wa siku 60 yaani miezi 2 kabla ya kupiga hiyo kura ya maoni. Je, ikiwa leo hii ni tarehe 10 Aprili hiyo miezi miwili ya kuelimisha wadau itapatikanaje?
Tatu, sheria inasema litolewe tangazo katika Gazeti la Serikali kuonesha tarehe elimu ya uraia itakapoanza kutolewa na kumalizika; mimi hadi leo sijaona wala kusikia kama Tume imetoa tangazo namna hiyo. Sijui wenzangu nyie na kama halijatolewa ni lini Tume hiyo itatangaza?
Basi, kwa ukosefu wa mambo hayo yote matatu ya msingi ni dhahiri tarehe 30 Aprili kwa vyovyote vile haingewezekana wadau wa nchi hii kupiga kura yao ya maoni kwa Katiba Pendekezwa. Hapo sasa tunajiuliza kwa upungufu wa msingi namna hiyo bado Serikali inasita kutamka uahirisho wa KURA ILE YA MAONI? Hali namna hiyo tu inatosha kuitwa MPARAGANYIKO!
Tume ya Uchaguzi imeliona hilo na imekuwa na sababu, tunaamini, za msingi zilizochelewesha huu uandikishaji wa wapigakura katika daftari linaloboreshwa ili tujue ni wangapi wana haki ya kupiga hiyo kura ya maoni. Kama mkoa mmoja tu wa Njombe uandikishaji unasuasua na bado haujakamilika ni zaidi ya mwezi mmoja sasa, sembuse uandikishwaji katika mikoa 29 iliyosalia utachukua muda gani?
Ninafurahi kuona Tume imegutuka na kutambua hali halisi. Kwa hilo Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva, aliweza kuchukua hatua sahihi na kwa wakati mwafaka kutueleza hali halisi ilivyo. Katika maelezo yake mwenyekiti amekiri upungufu kadhaa uliyoikumba Tume yake katika utekelezaji wa jukumu hili nyeti katika Taifa.
Kwanza, hawakuwa na ujuzi wa kutosha katika kutumia hivyo vifaa vipya vya mfumo wa kielektroniki (BVR). Wamepata matatizo kuvitumia na sasa nafikiri wamezoea kuvitumia (kwa kilatini tunasema EXPERIECIA DOCET, na kwa uzoefu huo wanaweza kuharakisha uandikishaji sasa.
Jingine lilikuwa ni upungufu mkubwa sana wa vifaa vya kazi hiyo. Sasa lakini Mwenyekiti wa Tume amesema Serikali imeshanunua vifaa 248 zaidi na vitatumika kwa awamu ya pili katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara. Na kwa kukamilisha uandikishaji wa mikoa 25 ya mwisho vimeagizwa vifaa 1,600 kutoka China.
Vifaa peke yake tumeambiwa vimetumia dola milioni 72 za Marekani. Ni fedha nyingi sana, hapo. Tusiiharakishe Tume, tuipe muda ikamilishe kazi na iwe nzuri, bora na yenye thamani ya fedha zetu nyingi hizo zilizokwishalipwa.
Kwa mtazamo wangu, nafikiri Mwenyekiti wa Tume alikuwa sahihi kulitangazia Taifa kuahirishwa kwa tarehe ya kupiga kura ya maoni katika nchi hii. Basi ni vizuri na vema kuishukuru Tume kwa kusema ukweli wa hali ilivyo. Kwa tangazo la Tume kuwa kazi ya msingi ya kuboresha Daftari la Wapigakura bado haijakamilika wametupoza nyoyo zetu. Maana hakuna sababu sasa ya watu kujiuliza hiyo kura ya maoni Aprili 30 itapigwa na akina nani? Sasa tuna hakika sote tutaweza kuandikishwa na hivyo sote mamilioni ya wananchi tutapata ile haki yetu ya kupiga kura.
Mimi nashukuru kitendo cha Tume kutangaza kuwa daftari litakamilika Julai. Kama haya yangejulikana kabla sidhani kama kungekuwa na fujo zile zilizotokea bungeni wakati wa kikao kilichopita. Haki ya kupiga kura ni haki ya msingi ya kila raia anayestahili kwa mujibu wa sheria. Lakini haki hiyo inaendana na wajibu wa kila mhusika kujiandikisha kwanza katika daftari.
Katika maandiko ya vitabu vya dini ipo methali inasema hivi: Kura hukomesha mashindano, hukata maneno ya wakuu (Methali 18 aya 18). Haki hiyo ya kukomesha tambo za vyama vya siasa ni yako wewe kwa kutumia utashi wako kuamua kwa busara hatima ya nchi yako Tanzania. Lakini wajibu wako wa kwanza na mkubwa ni KUJIANDIKISHA katika Daftari la Kudumu Wapigakura wa nchi hii.
Nakushauri kupunguza au kuondoa kabisa mparaganyiko unaotokea hivi sasa wewe ndugu yangu kwanza kajiandikishe. Sote tunahimizwa kutenda, basi badala ya kulalamika, maandiko matakatifu yanasema “INUKA” maana shughuli hii inakuhusu wewe na sisi tu pamoja na wewe, uwe na moyo mkuu, UKATENDE (Tazama Ezra sura 10 mstari wa 4). Basi Watanzania tusiwe wasemaji, tuwe watendaji.
TUJIANDIKISHE kwanza ndipo tutaweza kupiga kura ya “ndiyo” au “hapana” kwa Katiba Pendekezwa. Kura inakomesha mabishano ya wanasiasa na vyama vyao. Hii kura ni haki yako ya msingi kikatiba. Ni budi utumie haki hii mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu.
Rafiki yangu mmoja, mgeni kutoka nchi ya nje aliwahi kusema; “Watanzania, mnaweza sana kulalamika. Mnaongea kama yule ndege chiriku. Lakini mbona mu wazito wa kutimiza mipango yenu mizuri? Ubunifu mnao, wasomi mnao, lakini kwa nini mu wazito kutenda?” Sikuwa na jibu. Sasa maadam tarehe ya kupiga kura ya maoni imesogezwa mbele na itatangazwa mara tu Daftari la Wapigakura likikamilika, nadhani tumepata muda wa kutosha kutoa uamuzi mwafaka kwa hiyo Katiba Pendekezwa.
Mataifa ya nje wanatuona Watanzania kama walimu kwa nchi mbalimbali za Afrika. Tuwe walimu wa matendo na si wa maneno tu katika kurekebisha huu mparaganyiko uliotokea katika nchi wakati huu. Sote tuwe kitu kimoja. Tusigeuke nyuma kuangalia hayo yaliyotokea; lililopita si ndwele, tugange yajayo, yaani tujiandae kwa kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura kisha tarehe itakayotangazwa ikifika twende kwa wingi tukapige kura yetu ya maoni. Ninawasihi sana, wananchi wote tuwe Wazalendo. Tusahau yaliyopita tukaze macho na mioyo yetu kwenye kupiga kura wakati ukifika. Ndiyo Utanzania wenyewe huo.
Mungu ibariki Tanzania, dumisha Uhuru na Umoja, wake kwa waume na watoto. Sote tunaimba daima maneno haya. Maneno hayo sasa tuyatekeleze kwa vitendo. AMINA.
Mwandishi wa Makala hii kitaaluma ni Mwalimu wa darasani, alikuwa Mkurugenzi wa Elimu Jeshini na alikuwa Mwalimu wa Siasa JKT na JWTZ. Ni mkereketwa wa elimu.