UNGUJA
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka manispaa kubadilika na kutofanya kazi kizamani na badala yake zitafute fedha kwa ajili ya miradi katika maeneo yao hasa ya mijini.
Kauli hiyo ameitoa mjini hapa juzi akiwa katika mwendelezo wa ziara zake za wilaya aliyoianza hivi karibuni baada ya kuweka jiwe la msingi katika jengo jipya la wajasiriamali wa vifaa vya umeme na elektroniki zilizotumika (used) lililopo Mombasa, Shehia ya Kwa Mchina, Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar.
Amezitaka manispaa hizo kutafuta mikopo ili watekeleze miradi ya maendeleo kwa kujenga majengo ya kibiashara na kumalizia ujenzi wa jengo hilo.
Amezihakikishia manispaa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itachukua dhamana kuhakikisha linawezekana kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali ili wasiuze bidhaa zao katika maeneo yasiyohusika yakiwamo katika hifadhi za barabara.
“Nimeamua kujenga miradi hiyo kwa kuona kwamba Zanzibar haina maeneo maalumu ya kufanya shughuli za wajasiriamali na kueleza lengo la ujenzi huo ni kuwa na maduka ya kisasa,” amesema.
Pia ameeleza azima ya SMZ kufanya ukarabati wa barabara zote za mjini ikiwamo kujenga njia za wapita kwa miguu, baiskeli zenye taa, bustani pamoja na kujenga barabara za juu (flyover) katika mzunguko wa barabara ya Mwanakwerekwe na Amani.
Amesema serikali ina nia nzuri ya kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali kwa kuwajengea majengo yenye hadhi na yenye kuweza kufanya shughuli zao kisasa.
Katika hatua nyingine, ameipongeza JKU kwa kutekeleza vema miradi ya ujenzi waliyopewa na licha ya uwezo wa kikosi hicho pamoja na kiwango kidogo cha gharama za ujenzi ndiyo sababu ya serikali kuwapa zabuni hiyo.
Ameweka jiwe la msingi katika Shule ya Msingi ya Mwanakwerekwe inayojengwa na Kampuni ya Estim Enteprises Company Ltd kupitia fedha za Uviko-19 na kumtaka mshauri elekezi kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi huo unamalizika kwa muda uliopangwa.
Amesema hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea bila ya watu wake kuwa na elimu nzuri.
Amesema shule hiyo ya msingi ni ya kipekee, ina maabara, chumba cha kompyuta, ofisi ya mwalimu mkuu ya kisasa na kuwataka walimu kuendelea kufanya kazi zao vizuri.
Hata hivyo, ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha baada ya kumaliza kwa ujenzi wake iwekewe vifaa vyote muhimu.
Awali, akiweka jiwe la msingi la Hospitali ya Wilaya, Shehia ya Jitimai Mwanakwerewe, amesema lengo la serikali yake ni kuzifanya huduma za afya kuwa bora zaidi.
Amesema serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha inajenga hospitali zenye hadhi katika wilaya zote kwa lengo la kuimarisha huduma za afya na kueleza kwamba hospitali hiyo itakuwa ikitoa huduma zote muhimu za afya zitakazokuwa za kisasa zikiwamo huduma za upasuaji.
Amemtaka mkandarasi kuhakikisha Septemba, 2022 anakabidhi jengo hilo na kumtaka afanye kazi usiku na mchana huku akiiagiza wizara hiyo kuhakikisha mazingira ya nje ya hospitali hiyo yanawekwa vizuri pamoja na kuwepo kwa huduma ya maji ya uhakika.
MWISHO
Waombaji mikopo elimu ya juu
watakiwa kusoma mwongozo
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewataka waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa 2022/2023 kusoma na kuuzingatia mwongozo wa utoaji mikopo ili kuwasilisha maombi kwa usahihi.
Kauli hiyo ameitoa Dar es Salaam hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo.
“Kuanzia Julai 12, 2022 mwongozo huu utapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na ya wizara (www.moe.go.tz) katika lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza na kuwapa fursa waombaji kuusoma.
“Dirisha la kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao linatarajiwa kufunguliwa Julai 19 hadi Septemba 30, 2022,” amesema.
Mkenda amesema dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo wa 2022/2023 litakuwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30, 2022 na kuwataka wanafunzi wanaoomba wasome mwongozo kabla ya kuomba mkopo kwa kuwa ndio unataja sifa, vigezo na utaratibu wa kuomba mikopo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe, amewakumbusha waombaji mikopo kuzingatia maelekezo yaliyomo katika mwongozo huo ili kuondokana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Uzoefu unaonyesha kuwa wanafunzi waombaji wamekuwa hawazingatii taratibu wakati wa kufanya maombi. Tunawasihi wazingatie maelekezo ya mwongozo. Wakati wa dirisha la maombi kumekuwapo changamoto nyingi zinazojitokeza kwa waombaji,” amesema Mdoe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru, amesema Julai kila mwaka wanaanza kupokea maombi ya mkopo kwa mwaka wa masomo unaofuata na mwongozo huo hutoa maelezo ya kina kuhusu sifa na utaratibu wa kupanga mikopo kwa mwaka husika.
“Mwongozo huo umekamilika na kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi. Kuanzia wiki hii tutaanza kuendesha programu za elimu kwa umma kupitia redio, televisheni, mikutano katika kambi za JKT na mitandao ya kijamii,” amesema.
Katika mwaka wa masomo 2022/2023, serikali imetenga Sh bilioni 573 kwa ajili ya kutoa mikopo na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.