Wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, serikali ilijitahidi na kufanikiwa kujenga shule za msingi na sekondari kwa madhumuni ya kutoa elimu kwa vijana. Wakati huo hapakuwa na shule nyingi za binafsi kama ilivyo sasa.

Pia zilikuwapo shule chache zilizomilikiwa na taasisi za dini, mashirika binafsi, hivyo idadi  kubwa ya wanafunzi walisoma katika shule za umma kuanzia msingi, sekondari hadi chuo kikuu.

Wanafunzi walioshindwa kujiunga na sekondari za umma, hasa wale wazazi wao waliokuwa na kipato cha juu ndio walijiunga na shule za sekondari za binafsi, kwa kuwa na uwezo wa kulipa ada na enzi hizo serikali ilitoa elimu bila malipo.

Mei 14, 1967 akihutubia walimu juu ya umuhimu wa elimu ya kujitegemea mkoani Mbeya, Nyerere, anasema na kuongeza: “Tunafundisha watoto wetu katika  shule za msingi shabaha yetu ilikuwa ni kuwaingiza katika sekondari. Ilikuwa shule nzuri ni shule inayofaulu kupeleka watoto wengi  katika  shule ya sekondari.

“Mwalimu mzuri ni anayewezesha wanafunzi  wake kufaulu mtihani wa kuingia katika darasa la sekondari. Mtoto mzuri ni anayeleta sifa kwa shule yake, ni yule anayefaulu mtihani kuingia katika darasa la sekondari.”

Nyerere alikuwa anawakumbusha walimu kazi yao pamoja na kufundisha maadili na uzalendo kwa wanafunzi shuleni na jukumu lao kubwa ni kufundisha wanafunzi na kuwawezesha kufaulu  mitihani yao vizuri ili kuendelea na masomo katika  ngazi nyingine.

Kuanzia miaka ya 1990, mwamko wa elimu uliongezeka kwa kasi kubwa, shule za binafsi  ziliendelea kujengwa kwa wingi kwa ngazi ya msingi na sekondari. Hali hiyo ilisababisha wazazi  wengi kupeleka watoto katika shule za binafsi  kwa kuamini kwamba ndizo hutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete ilijenga shule nyingi za kata hapa nchini lengo likiwa ni kuwapunguzia wazazi gharama za kusomesha watoto wao mbali na nyumbani na kwamba zimelenga wapate elimu ya sekondari katika hatua ya kukuza nguvu ya taifa na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Pamoja na malengo hayo mazuri, wazazi wengi, hasa wale wenye kipato cha juu, huwapeleka watoto wao katika shule za kulipia hata kama wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za serikali, kwa madai kwamba za kulipia hufundisha vizuri na kutoa elimu bora zaidi kwa wanafunzi.

Miaka ya hivi karibuni serikali imeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto zinazokwamisha upatikanaji na utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa sekondari wakiwamo wa shule za kata.  

Baadhi ya maeneo miundombinu imeboreshwa ikiwamo kujengwa kwa maktaba, maabara, vyumba vya madarasa, nishati ya umeme, kuongeza idadi ya walimu na kujenga nyumba za walimu. Hatua zinazoelezwa kuanza kutoa matunda katika baadhi ya shule kuanza kufanya vizuri hasa za kidato cha sita.

Mwaka 2019 katika matokeo ya mtihani wa kitaifa kidato cha sita kati ya shule 100 bora kitaifa shule 54 zilikuwa ni za kata ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa shule hizo kufanya vizuri na kuingia katika ushindani kitaifa. 

Katika matokeo hayo shule mbili za kata za Kisimiri na Mwandeti zote za mkoani Arusha zilifanikiwa kuingia katika orodha ya 10 bora kitaifa na kuandika historia.

Kwa mfano Kisimiri, kati ya wanafunzi 63 waliohitimu kidato cha sita mwaka huo wanafunzi 50 walipata ufaulu wa daraja la kwanza na wanafunzi 13 waliobaki walipata daraja la pili.

Mwenendo huo wa shule za umma haukuishia hapo, Agosti 21, 2020 aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde, alitangaza matokeo ya mtihani wa kitaifa kidato cha sita na kusema kuwa kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 0.03 kutoka asilimia 98.32 mwaka 2019 hadi 98.35 kwa mwaka 2020.

Akitangaza matokeo hayo mjini Unguja, Msonde,  anasema ufaulu umezidi kuimarika kwa watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la kwanza, la pili na la tatu umeongezeka kwa asilimia 1.13 kutoka asilimia 96.61 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 97.74 mwaka 2020.

Katika shule 10 bora kitaifa, nane zilikuwa za umma huku shule mbili zikiwa ni za binafsi na shule hizo na mikoa yake kwenye mabano.

Shule ya kwanza Kisimiri (Arusha), ya pili Kemebos (Kagera), ya tatu ikichukuliwa na Ahmes (Pwani) na Mzumbe (Morogoro) ikiwa nafasi ya nne.

Shule nyingine katika 10 bora zilikuwa ni Tabora Girls (Tabora), Tabora Boys (Tabora), Ilboru (Arusha) na Kibaha (Pwani).

Shule ya Mwandeti (Arusha) ilishika nafasi ya tisa na nafasi ya 10 ilishikwa na Shule ya Dareda (Manyara).

Dk. Msonde anataja watahiniwa 10 bora kwa masomo ya sayansi huku watahiniwa watatu  wakitoka katika shule za serikali.

Jumla ya watahiniwa 82,440 sawa na asilimia 98.35 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo Juni na Julai, 2020 walifaulu huku wasichana wakiwa ni 35,486 sawa na asilimia 99.07 wakati wavulana wakiwa ni 46,954 sawa asilimia 97.81.

Julai 10, 2021 matokeo ya kidato cha sita yalitangazwa huku yakionyesha kuongezeka kwa ufaulu kwa asilimia 0.31. 

Dk. Msonde anasema ubora umezidi kuimarika kwa idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la kwanza hadi la tatu. Anasema kuna ongezeko la asilimia 0.99 kutoka asilimia 97.74 mwaka 2020 hadi asilimia 97.93 mwaka 2021.

Katika matokeo shule za umma zimeendelea kutamba kwa kushika nafasi za juu zaidi huku shule nane kati ya 10 katika orodha ya shule bora kitaifa lakini ni rekodi ya kipekee kwa Kisimiri kuendelea kushika nafasi ya kwanza kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2019.

Rekodi nyingine katika matokeo hayo imejionyesha kwa Dareda iliyopanda kutoka nafasi ya 10 mwaka 2020 hadi nafasi ya tatu mwaka 2021.

Shule za serikali zimeendelea kung’ara kwa mara nyingine tena katika matokeo ya mtihani wa kitaifa  ya mwaka 2022 kwa sababu katika 10 bora kitaifa, saba ni za serikali.

Julai 5, 2022 matokeo ya mitihani ya kidato cha sita yanaonyesha ufaulu wa asilimia 99.87 ukiwa umeongezeka huku wa wasichana ukizidi kidogo  wa wavulana kwa asilimia 0.08.

Akitangaza matokeo hayo Kaimu Katibu  Mtendaji  wa NECTA, Athuman Amas, anasema ufaulu wa mwaka huu  umepanda kidogo kwa asilimia 0.25 kutoka asilimia 99.87 ya mwaka jana.

Jumla ya watahiniwa 95,826 waliosajiliwa kufanya mtihani huo  kati ya hao wasichana ni 41,517 sawa na asilimia 43.33 na wavulana ni 54,309 sawa na asilimia  56.67.

Akitangaza matokeo hayo, anasema jumla ya watahiniwa 83,877 sawa na asilimia 99.24 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu wakiwamo wasichana 37,170 sawa na asilimia  99.34 na wavulana 46,707 sawa na asilimia 99.16.

Anataja shule 10 bora kitaifa kuwa ya kwanza ni  Kemebos (binafsi), ya pili Kisimiri (serikali), na ya tatu Tabora Boys (serikali). Nyingine ni Tabora Girls (serikali), Nyaishozi (binafsi), Mzumbe (serikali), Mkindi (serikali) na Ziba (serikali).

Sababu za ufaulu mzuri umeelezwa kuwa ni motisha kwa walimu na wanafunzi, ushirikiano mzuri kati ya wazazi na shule, wanafunzi kujituma  na kujifunza kwa bidii na walimu kufundisha kwa bidii na kuwajenga katika maadili mema.

Sababu zingine zinaelezwa kuwa ni mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia, kamati na bodi za shule kutoa ushirikiano mzuri kwa walimu na shule kwa ujumla katika jukumu zima la kutoa elimu kwa wanafunzi.

Mtaalamu wa Elimu ya Uraia, Mwalimu Leonard Kitindi, wa Sabasaba Manispaa ya Morogoro anasema ushirikiano wa wazazi kufuatilia taaluma na nidhamu ya watoto wao ni chachu katika  matokeo mazuri ya wanafunzi kitaaluma.

Kitindi anakwenda mbali na kusema serikali imefanya jitihada kubwa kukarabati baadhi ya shule kongwe na kuboresha miundombinu katika  shule mbalimbali na hatua hiyo imekuwa na tija kubwa.

“Taaluma bora kwa wanafunzi inatokana na nidhamu nzuri za wanafunzi, wazazi kushirikiana na walimu kufuatilia watoto katika nidhamu na taaluma, serikali iendelee na jitihada za kuboresha miundombinu ya shule,” anasema Kitindi.

0755-985966