Na Nizar K Visram

Hatimaye wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamemzika rasmi Waziri Mkuu wao wa kwanza, Patrice Lumumba, aliyeuawa mwaka 1961. Wakoloni na vibaraka wao walimuua kisha wakakatakata mwili wake na kuuyeyusha katika tindikali.

Kilichobaki ni jino lake ambalo limerejeshwa kutoka Ubelgiji. Mabaki hayo ndiyo yalizikwa kwa heshima kubwa baada ya kutembezwa maeneo kadha ya nchi hiyo ili kuruhusu wananchi kutoa heshima zao za mwisho.

Kamishna wa Polisi wa Ubelgiji, Gerard Soete, ndiye aliyesimamia mauaji ya Lumumba, naye akachukua meno mawili na vidole viwili kama ‘nyara ya uwindaji’. Soete akafia Ubelgiji na mwaka 2016 binti yake akaonyesha hadharani jino la Lumumba.

Juliana, binti wa Lumumba, akaandika barua rasmi kwa mfalme wa Ubelgiji akitaka jino lirejeshwe. 

Ndipo jino la Lumumba likarejeshwa kwa familia yake Juni 20, 2022 katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels. Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Alexander de Croo, alikabidhi jino huku akikiri kuwa ‘dhuluma kubwa ilitendeka kwa Lumumba aliyeuawa kwa ajili ya mawazo yake na siasa yake.’

Akasema mawaziri wa Ubelgiji waliokuwapo wakati huo wanawajibika kwa mazingira yaliyosababisha kuuawa kwa Lumumba.

“Huu ni ukweli unaoumiza lakini ni lazima usemwe, nami nataka niseme mbele ya wanafamilia wake kuwa kwa niaba ya Serikali ya Ubelgiji naomba radhi,” anatamka Croo.

Wanafamilia wakapokea jino. Mtoto wa Lumumba, Ronald, akasema mazishi ya baba yao sasa yatafanyika baada ya miaka 61 na kipindi cha maombolezo kitamalizika rasmi. Akasema kwa mujibu wa mila za Afrika maombolezo yanaendelea hadi mwili wake uzikwe na sasa jino ni sehemu ya mwili wake.

Serikali ya DRC ikatangaza siku tatu za maombolezo. Jeneza likatembezwa nchini kote ili wananchi watoe heshima zao za mwisho na baada ya hapo akazikwa Kinshasa.

DRC (Congo Kinshasa) ilijipatia Uhuru wake Juni 30, 1960, Lumumba akiwa amechaguliwa kama waziri mkuu wa kwanza. Mfalme wa Ubelgiji Baudouin akaja Kinshasa kukabidhi madaraka. 

Akausifu ukoloni wa Ubelgiji na akamsifu babu yake, mfalme Léopold wa pili kama mtawala ‘mstaarabu.’  Hakusema lolote kuhusu mamilioni waliokufa au walioteswa chini ya utawala wake.   

Lumumba akajibu hotuba ya mfalme. Akaelezea utumwa na udhalimu wa ukoloni wa Kibelgiji.  Akasema Congo imejipatia uhuru si kutokana na ubinadamu au uungwana wa Wabelgiji bali kutokana na jasho, damu na roho za Wakongomani. 

Mfalme na maofisa wake wakapigwa butwaa. Mwandishi Ludo De Witte akasema sijawahi kumsikia Mwafrika akidiriki kuongea maneno kama hayo mbele ya Wazungu. Katika vyombo vya habari vya Ubelgiji, Lumumba, akaonekana mtu hatari kwa masilahi ya Magharibi. 

Ndipo majeshi yakiongozwa na kibaraka Mobutu Sese Seko yakashika madaraka na kuipindua serikali ya Lumumba kisha wakamkamata. Jimbo la Katanga likajaribu kujitenga, chini ya uongozi wa kibaraka Moise Tshombe. 

Lumumba akahamishwa kutoka Kasai alikokamatwa na kupelekwa Leopoldville. Kutoka hapo akapelekwa Katanga akiwa na Waziri wake, Maurice Mpolo na Joseph Okito (Naibu Spika wa Bunge).

Wakiwa Katanga majeshi ya Mobutu wakawatesa wakishuhudiwa na maofisa wa Ubelgiji. Januari 17, 1961 wanajeshi wakawapiga risasi na kuwaua. Mwili wa Lumumba ukafukiwa lakini baadaye ukafukuliwa, ukakatwa katwa na kisha ukayeyushwa katika tindikali. 

Mwaka 1999 mwandishi wa Ubelgiji, Ludo De Witte, aliandika kitabu kiitwacho ‘Kuuawa kwa Lumumba’.  Akasema kuna haja ya kutambua ni nani hasa wanaowajibika kwa mauaji yake kisha hatua zikachukuliwa ili Lumumba apatiwe heshima anayostahili katika historia ya Afrika.

Ndipo watu wakataka kujua zaidi kuhusu mauaji. Maswali yakaanza kuulizwa na hoja ikawasilishwa bungeni. Bunge likafanya utafiti na serikali ikakutwa ilihusika katika mauaji ya Lumumba.

Baada ya uchunguzi wa kibunge ndipo mwaka 2002 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Louis Michel, akaonyesha ‘masikitiko ya dhati’ kutokana na jinsi nchi yao ilivyohusika katika mauaji ya Lumumba.

Mapema Juni, 2022 Mfalme Philippe wa Ubelgiji alitembelea DRC na akasema ‘anasikitishwa sana’ na jinsi nchi yake ilivyoitendea DRC wakati wa ukoloni. Akasema ukoloni wa Ubelgiji ulikuwa wa kibaguzi na wenye madhara yasiyoelezeka. Baada ya miaka 60, wakoloni sasa wanaungama kuwa utawala wao ulikuwa wa kidhalimu.

Walijaribu kuficha ukweli wakashindwa. Ukweli wenyewe ni kuwa Mfalme Leopold aliigeuza Congo kuwa shamba lake la mpira. Akawageuza raia kuwa watumwa wakifanya kazi ya kumlimia zao la mpira uliopelekwa Ubelgiji. 

Watumwa hao wa mfalme wapatao milioni 10 walikufa kutokana na njaa na magonjwa. Waliobaki walilazimishwa kuzalisha kiasi cha kutosha na walioshindwa walikatwa mikono.  Huo ndio ukoloni wa Kibelgiji nchini Congo.  

Miaka 40 baada ya kuuawa kwa Lumumba ikapatikana habari nchini Marekani kuwa aliyekuwa Rais Dwight Eisenhower alihusika na mauaji hayo. Aliyekuwa Katibu Muhtasi wa rais huyo, Robert Johnson, aliandika kumbukumbu zake kuhusu mazungumzo baina ya Eizenhower na washauri wake walipokuwa wakizungumzia suala la Congo. 

Johnson alieleza jinsi Eisenhower alivyomgeukia Allen Dulles aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la  Ujasusi (CIA) la Marekani, akamwambia ni vizuri kama Lumumba ‘angemalizwa.’ Kwa muda wa nukta 15 kila mmoja akapigwa bumbuwazi kuhusu maagizo ya Rais wa Marekani ya kummaliza Lumumba.

Wakati wa uhuru, Juni, 1960, uasi ukazuka miongoni mwa majeshi. Hiki kikawa kisingizio cha Ubelgiji kutuma majeshi yake. Hatua hii ikalaaniwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dag Hammarskjöld, aliyeandaa mipango ya kutuma majeshi nchini Congo.

Wakati majeshi ya Ubelgiji yanawasili hali ikazidi kuchafuka na Katanga kwenye madini mengi ikatangaza kujitenga kutoka Congo. Aliyeongoza hatua hiyo ni Moise Tshombe ambaye aliungwa mkono na Ubelgiji na Marekani.

Februari 17, 1961 Gazeti la Daily Telegraph la nchini Uingereza likatangaza kuwa ndege ya usafirishaji Boeing C-97 kutoka Marekani ilikuwa ikisafirisha kwa siri ndege tatu aina ya Fouga hadi Katanga. Ndege hizi ziliweza kutumika katika vita.

Kitendo hiki kilikuwa kinasaliti azimio la Baraza la Usalama la UN. Kwa hiyo ikatumika mbinu ya kuficha usafirishaji huo. Boeing ikaruka kutoka Luxembourg ikadai inakwenda Johannesburg. Wakati ikiwa hewani rubani akasema ameishiwa mafuta na anahitaji kutua Ndjamena, Mji Mkuu wa Chad. Kutoka hapo ikaelekea Mji Mkuu wa Katanga, Elisabethville (leo inaitwa Lubumbashi).

Ndege ilipowasili Katanga ilishuhudiwa na David W Doyle aliyekuwa Mkuu wa CIA huko Katanga. Katika kitabu chake cha ‘True Men and Traitors’, Doyle alielezea jinsi ndege za Fouga zilivyosafirishwa kutoka Marekani na marubani wa Kimarekani ili kumsaidia Tshombe. 

Anaongeza kuwa lengo la Fouga lilikuwa kuzidungua ndege za UN nchini Congo.

Nyaraka zilionyesha kuwa ndege za Fouga zilinunuliwa na CIA na kazi ya usafirishaji ikapewa Kampuni ya Seven Seas. Doyle, akiwa Mkuu wa CIA jimboni Katanga, alifika uwanja wa ndege kuzipokea.

Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah, alikasirishwa sana na mauaji ya Lumumba aliyekuwa na uhusiano naye wa karibu. Aliilaumu Marekani na nchi za Magharibi. 

Aidha, akapata habari za Fouga tatu zilizowasili Katanga kutoka Marekani kwa ajili ya Tshombe na kuna nyingine sita zinatarajiwa kuwasili.

Mara moja waziri wake wa Mambo ya Nje akawasilisha risala kali kwa Balozi wa Marekani mjini Accra. Rais Kennedy wa Marekani akajaribu kumpoza Nkrumah kwa kumwambia kuwa serikali yake haikuwa na habari za Fouga. Nkrumah akajibu kuwa hana imani na jibu hilo.

Baada ya Tshombe kupokea Fouga, nguvu zake zikaongezeka kwa vile majeshi yake yakawa yanatawala anga wakati majeshi ya UN hayakuwa na uwezo huo. Hammarskjöld akaomba nchi wanachama wachukue hatua za haraka. Ethiopia ikawa tayari kusaidia lakini Uingereza ikakataa kuruhusu ndege zake zipitie anga za makoloni yake ya Afrika Mashariki kuelekea Congo.

Ndipo usiku wa  Septemba 17 kuamkia 18, 1961 ndege iliyokuwa imembeba Hammarskjöld ikadunguliwa karibu na mpaka wa Congo na Zambia (wakati huo Rhodesia Kaskazini). Hammarskjöld akauawa pamoja na abiria wengine 15. Tukio hili lilitokea miezi minane baada ya kuuawa kwa Lumumba.

Kama alivyouawa Lumumba, Hammarskjöld naye aliuawa wakati nchi za Magharibi na kampuni zao zilikuwa zikimezea mate maliasili za Congo. Ardhi ya Katanga ilikuwa na akiba kubwa ya madini pamoja na urani iliyotumika katika kuunda mabomu ya atomiki yaliyotumiwa na Marekani huko Japan. 

Tshombe akatangaza kujitenga kwa Katanga, akiungwa mkono na mataifa ya Magharibi na kampuni za madini. Hammarskjöld akajaribu kuokoa jahazi, akachukua ndege na kuelekea Katanga kuanza mazungumzo ya upatanishi. Alipanga kukutana na Tshombe lakini maadui wakamuua.

Nchi ikatawaliwa na Mobutu kipenzi cha Marekani, hadi mwaka 1971. Huyu sajini wa jeshi akawa jenerali na akatumia utawala wake kuibia nchi zaidi ya dola bilioni saba za Marekani. 

[email protected] 

+1 343 204 8996 (whatsapp)