Ni hivi karibuni, Watanzania tumeshuhudia kuanzishwa na kupokelewa vyama viwili vipya vya siasa nchini. Vyama hivyo ni Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) na Chama Cha Kijamaa na Uzalendo (CKU-Tanzania).
Vyama hivyo vimepokewa na kusajiliwa rasmi na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, baada ya kuridhishwa na maombi ya wanachama wa vyama hivyo. Kimsingi wanachama na baadhi ya Watanzania wanaunga mkono kuwapo kwa vyama hivyo, huku wakiwa na matumaini ya kuwa na hali sawa za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Kabla ya kuangalia sababu za kuwapo vyama hivyo, sina budi kutoa kongole zangu kwa waasisi na viongozi wa vyama hivyo akiwamo Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, na Mwenyekiti wa CKU-Tanzania, Ramadhani Semtawa, kwa ujasiri na umahiri wao katika kupigania kupata haki na fursa sawa kwa vijana nchini.
Chama ACT-Wazalendo na CKU-Tanzania vyote vinazungumzia na kutetea misingi ya utu, haki, usawa, umoja na ushirikiano. Picha hiyo inatokana na maneno yaliyotumika katika majina ya vyama. Itashangaza na kusikitisha endapo viongozi hawatasimamia kauli na ahadi zao za kuwavusha wananchi kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye utajiri. Ukweli, waasisi na viongozi wa vyama hivyo kwa zaidi ya asilimia 90 ni vijana. Vijana hawa wana sababu za msingi za kuanzisha vyama vya siasa katika muktadha wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa nia ya kuwainua vijana wenzao na wananchi baada ya kukumbwa na wawimbi makubwa mazito ya umasikini, rushwa na ufisadi.
Sisemi vyama vya siasa vilivyopo kabla ya vyama hivi havijaangalia na kushughulikia masuala ya ujenzi wa uchumi imara wala kuweka usalama madhubuti kwa wananchi, la hasha, nakiri na kusema vyama vilivyopo vimeangalia na vinaendelea kujenga uchumi na kushughulika na masuala usalama. ACT-Wazalendo na CKU-Tanzania vinaonesha dalili za kutaka mabadiliko katika masuala ya msingi ya kijamii.
Vijana wanataka mabadiliko katika maeneo makuu matatu. Kwanza kupata haki na fursa sawa za maendeleo ya kiuchumi kwa maana ya kazi na ajira za uhakika, kwa lengo la kukuza pato la mtu na pato la Taifa.
Hivi sasa vijana wanaona hawapati nafasi za kazi na ajira kwa kufuata na kuzingatia misingi halali ya mtu kuwa na elimu, taaluma na uwezo wa kufanya kazi. Badala yake vigezo vya upendeleo, nasaba, udini, ukabila na jinsia ndiyo vigezo na sifa za kupata ajira. Kwa mtaji huu, vijana wanaona ipo haja ya mabadiliko katika jamii yetu.
Pili, vijana wanataka kuaminiwa na kupewa madaraka na uongozi katika utumishi wa umma na kwenye vyombo vya mamlaka vya uamuzi na usimamizi wa haki sawa kwa wananchi na kwenye mipango ya maendeleo ya Taifa letu. Leo, vijana wengi hawana wala hawapewi madaraka na uongozi kwa kuzingatia vigezo vya mamlaka hayo, bali wanapewa kwa kuzingatia sifa za kifamilia, kutoa rushwa na kuwa na uwezo wa kutetea na kulinda njia za ufisadi za wakubwa.
Ndiyo maana katika majira yetu haya tuna wapambe na wapiga debe wengi wanao ‘wafagilia’ viongozi waliopo madarakani. Na tatu, vijana wanaeleza kuwa wamechoshwa na mfumo uliopo wanaouita ‘mfumo kandamizi wa maendeleo ya wananchi’ ambao unawanyima haki wananchi wa hali ya chini na kuwapendelea wananchi wa hali ya juu kimaisha.
Mitazamo na maelezo ya vijana katika ‘mfumo’ huo uliopo inatokana na baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wakubwa wanavyotetewa na kulindwa na mali zao katika vyombo vya kusimamia haki hata kama ukwasi na mali hizo zimepatikana nje ya uhalali.
Sababu hizo na nyinginezo; vijana wanaona ipo haja ya kuanzisha na kuendeleza mijadala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kupitia katika vyama vyao vya siasa na katika majukwaa ya haki za binadamu na majukwaa ya kutoa na kupata habari nchini, bila kuvunja sheria za nchi.
Naweza kusema kuwa vyama hivi viwili vya siasa vimejichomoza wakati maridhawa kabisa ambako Watanzania wamo katika mchakato wa kuelimishana, kufafanuliana na kuelewana kuhusu KATIBA INAYOPENDEKEZWA imebeba misingi ya kupata haki na usawa, kuzingatia maadili na miiko ya uongozi, ulinzi na usalama, tunu za Taifa na utawala bora.
Katiba inayopendekezwa imeweka wazi masuala ya vijana kuhusu haki ya kufanya kazi ibara ya 44, haki ya wafanyakazi na waajiri ibara ya 45 na haki na wajibu wa vijana ibara ya 54.
Kuhusu maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma juu ya dhamana ya uongozi wa umma, inapatikana ibara 28 na kununi za uongozi wa umma ibara ya 29 na utii wa miiko ya uongozi wa umma ibara ya 30 bila kusahau – marufuku kwa baadhi ya vitendo ibara ya 31.
Kwa ujumla masuala ya vijana yamepewa uzito stahiki katika Katiba inayopendekezwa ikiwa ni lengo la kukidhi maslahi ya vijana na wasio kuwa vijana. Ni matarajio yangu kuona vyama vya ACT-Wazalendo na CKU-Tanzania chini ya viongozi wake vijana, vinaweka DIRA ya maendeleo, taratibu bora za uongozi na heshima kwa wasiokuwa vijana.
Iwe ni mwiko na ni dhambi kuwabagua vijana wenzenu waliopo katika vyama vilivyowatangulia, wala kuwanyanyasa chipukizi na watoto wadogo na kuwapa visogo wazee. Kwani vijana ni maji ya moto; na vijana ni madanzi yenye ladha kali. Pimeni na mjaze.